Friday, April 1, 2011

MTOTO WA MKULIMA HALI YA MAISHA YA WATANZANIA WENGI NI MBAYA HAKUNA HAJA YA UTAFITI

Kweli Waziri Mkuu hajui hali ngumu inasababishwa na nini!  Send to a friend
Thursday, 31 March 2011 21:21
0diggsdigg
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
JUZI Waziri  Mkuu, Mizengo Pinda,  aliitaka Taasisi ya Kuondoa Umaskini  nchini (Repoa) kufanya utafiti wa kina kujua ni kwa nini wananchi wa kawaida wanalalamikia hali ngumu ya maisha wakati kitaifa uchumi unakua. Kwa maana nyingine ni kwamba, Pinda kama Waziri Mkuu na msimamizi wa shughuli za Serikali hajui kwa nini Watanzania wanaendelea kuwa maskini wakati mazingira ya kiuchumi yanatoa fursa ya watu kuondokana na tatizo hilo, ambalo kadiri siku zinavyozidi kwenda ndivyo linavyozidi kukua.

Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa 16 wa  Repoa, Pinda alieleza kuwa Serikali inatumia tafiti zinazofanywa na taasisi hiyo kupata ufumbuzi wa tatizo hilo na mengine yanayolikabili taifa.

Hii ni changamoto nzuri kwa Repoa ambayo imethaminiwa na kwamba inafanya kazi nzuri inayoweza kuisaidia Serikali kupata ufumbuzi wa matatizo yanayoihangaisha nchi yetu katika nyanja za uchumi na maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Kwa maana hiyo basi, Repoa inatakiwa kufanya kazi ya ziada kuvumbua tatizo la umaskini uliotopea unaoendelea kuongezeka miongoni mwa wananchi wa kawaida ili Serikali ichukue hatua, kwa kuwa mpaka sasa inaamini kuwa uchumi wa nchi unakua hata kama bei za bidhaa zinaendelea kupaa kila wakati.

Hata hivyo, tunadhani jukumu kubwa liko mikononi mwa Serikali kwa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa taarifa na ripoti za tafiti zilizofanyika kitaalamu na kuwasilishwa kwake.

Tunasema hivyo kwa sababu, kama hakuna dhamira ya dhati katika kutekeleza na kusimamia hakuna kitakachobadilika, hata kama Repoa watafanya kazi nzuri na kuandaa ripoti inayotoa mwongozo na njia ya kukabiliana na umaskini  hakuna kitakachofanyika.

Tuna kila sababu ya kusema hivyo, kwa vile hatuamini kama kweli Serikali yenye vyanzo vingi vya kupata taarifa, ikiwamo kukua na kuanguka kwa uchumi haijui kwa nini wananchi wanalalamikia hali ngumu ya maisha.

Lakini, je ni kweli Serikali haijui sababu ya watu wa kawaida kukabiliwa na umaskini? Je, ni kweli Waziri Mkuu hajui kuwa kuna mfumuko wa bei kwa bidhaa zote? Kama anajua kuwa bei za vyakula na bidhaa nyingine muhimu ziko juu yakiwamo mafuta ya petroli, inakuwaje ashangae wananchi kulalamikia hali ngumu ya maisha pamoja na umaskini unaowaandama?

Inashangaza kusikia kwamba wakati wananchi wa kawaida ambao ndiyo wengi wanalalamika,  Serikali inasema uchumi wa nchi unakua na haijui kwa nini imekuwa hivyo! Katika hali  halisi, uchumi wa nchi unakuwaje na nguvu wakati wananchi wa kawaida ambao ndiyo wengi wana hali ngumu?

Hoja yetu inasimama katika msingi kwamba, pato la taifa la ndani linagawanywa na idadi ya watu.  Sasa kama watu wengi ni maskini, uchumi unakuaje?  Unakuwaje imara na bei zikiwa juu ambazo wananchi hawawezi kuzimudu?

Tunachojua ni kwamba kama kweli uchumi wa nchi unakua, kwa tafsiri ya uwiano wa mapato na wananchi wake maana yake hivi sasa utajiri uko mikononi mwa watu wachache wanaomiliki njia zote za uchumi.

Pia inamaanisha utajiri wa nchi hii unashikiliwa na watu wachache, jambo ambalo ni hatari kwa ustawi wa jamii na taifa letu kwa ujumla.  Maana yake ni kwamba, ikiwa uchumi wa taifa uko mikononi mwa watu wachache ubepari umekomaa na ni hatari kwa taifa kwa sababu kwa kawaida bepari huangalia mazingira ya kibiashara kama yanaruhusu yeye kuendelea kuwepo, vinginevyo anaweza kuhamisha biashara zake  na kila kitu alichowekeza na kupata hapa nchini.

Mambo mengi yanayoweza kutokea katika hali hii ni kushamiri kwa rushwa na ufisadi, ukwepaji wa kodi ambalo pia limekuwa tatizo kubwa hapa nchini.  Haiwezekani uchumi wa taifa ukue wakati Mamlaka ya Mapato (TRA) inashindwa kuvuka malengo ya kukusanya kodi na wakati huohuo Serikali ikishindwa kutekeleza miradi ya maendeleo ya jamii  kwa kukosa fedha, mpaka zitoke kwa wafadhili.Tunamshauri Waziri Mkuu na Serikali kusema ukweli juu ya mambo yanayochangia hali ngumu ya maisha inayowakabili wananchi wake.

No comments:

Post a Comment