Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (kushoto) akimwonyesha Waziri
wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk David Mathayo baadhi ya ushaidi
aliokuwa nao wa hoja yake binafsi inayoitaka serikali kuchukua hatua
dhidi ya watanzania walioficha fedha haramu nje ya nchi, mjini Dodoma.
Picha na Edwin Mjwahuzi
NGUVU za Serikali za kutaka kuifuta hoja
binafsi ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Kabwe Zitto ya kuitaka
Serikali kuchukua hatua dhidi ya Watanzania walioficha fedha haramu nje
ya nchi, jana zilishindwa baada ya wabunge kadhaa kumgomea Mwanasheria
Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema kufanya hivyo.
Dalili za
Serikali kutaka kuzima hoja hiyo zilianza baada ya Jaji Werema kusimama
na kutoa mapendekezo ya kufuta vipengele muhimu.
Hatua hiyo ilizusha
mvutano mkali, huku baadhi ya wabunge wakisema Serikali inataka kuifuta
hoja hiyo muhimu kwa mustakabali wa taifa.
Mapendekezo ya Werema
Katika
mapendekezo yake, Jaji Werema alipendekeza kufanyika kwa marekebisho
kwenye kipengele katika hoja hiyo ya Zitto ambacho kiliitaka Serikali
iwasiliane na Benki ya Dunia ili kupitia Kitengo cha Assets Recovery
Unit irejeshe nchini mabilioni ya fedha yanayomilikiwa na Watanzania
katika benki za Uswisi na maeneo mengine yote ambayo hufichwa fedha ili
kukwepa kodi.
Jaji Werema alitaka pendekezo hilo liondolewe kwa
maelezo kuwa mamlaka za uchunguzi ikiwamo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (Takukuru) na Usalama wa Taifa zinalifanyia kazi suala hilo.
Eneo
jingine katika hoja ya Zitto ambalo Jaji Werema alipendekeza lifanyiwe
marekebisho ni kuwapiga marufuku viongozi wa Serikali na watoto wao
pamoja na Watanzania wengine kufungua akaunti nje akisema suala hilo
litashughulikiwa kwa mujibu wa sheria ya fedha za kigeni.
Pia alitaka
pendekezo lililomo katika hoja ya Zitto cha kutaja akaunti za watu
wenye fedha benki za nje na kuzichapisha katika vyombo vya habari
lifanyiwe marekebisho kwa kuondolewa.
Alisema suala hilo ni gumu na linakwenda kinyume na sheria za benki zinazotaka kutunza siri za wateja wao.
Kuhusu
pendekezo la kuitaka Serikali katika Bajeti ya mwaka wa fedha wa
2013/13 kuanzisha kodi maalumu ‘Financial Transaction Tax’ ya angalau
asilimia 0.5 ya thamani ya ‘transaction’ ili kuweza kuwa na rekodi za
uhakika fedha za ndani na zinazotoka nje ya nchi, Werema alitaka lifutwe
akisema hiyo inahitaji utafiti wa kutosha.
Alisema ofisi yake
imechukua siku nyingi kufanya uchunguzi kuhusu fedha hizo ikiwemo kwenda
Uswisi na kwingineko na kwamba itashirikiana na vyombo binafsi vya
uchunguzi kufanya kazi hiyo.
Pendekezo jingine lililopingwa na Jaji
Werema lilikuwa ni kuitaka Serikali kuwabana Watanzania wenye fedha nje
ya nchi waeleze walikozipata akisema kazi hiyo inaweza kufanywa na
Takukuru.
Wabunge wamshukia
Baada ya kutoa mapendekezo hayo,
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alisema anamshangaa
Mwanasheria Mkuu kwa kufanya marekebisho ambayo yanaizima hoja ya Zitto.
Huku
akinukuu vifungu vya Kanuni za Bunge, alisema Mwanasheria Mkuu anataka
kuua hoja hiyo na kwamba mapendekezo yake yanakwenda kinyume na kanuni
ambazo zinataka kila badiliko katika hoja liwiane na jambo
linalojadiliwa.
“Hoja ya mabadiliko ya Mwanasheria Mkuu kuondoa
mapendekezo hayo, kwa maoni yangu yanakinzana na Kifungu 53 (3) (4) cha
Kanuni za Bunge, kinachopendekeza kuwapo kwa mabadiliko na siyo kufuta
hoja.
Alisema hatua ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya kupendekeza
mabadiliko hayo ni kufuta hoja jambo ambalo alisema ni kinyume cha
kanuni. Kwa mujibu wa kanuni za Bunge, mtu ambaye anaweza kuiondoa hoja
ni mtoa hoja na si mtu mwingine yeyote.
Alimtaka Spika kutumia busara yake kumzuia Mwanasheria Mkuu kufuta hoja hiyo muhimu kwa mustakabali wa nchi.
Baada
ya maelezo hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na
Bunge), William Lukuvi alisimama na kuunga mkono mapendekezo ya
Mwanasheria Mkuu, huku akielekeza ‘makombora’ kwa Lissu kuwa
anachokisema kinapingana na mtoa hoja Zitto, ambaye anakubaliana na
Mwanasheria Mkuu.
Hata hivyo, Zitto alisimama na kutoa ufafanuzi kuwa
hakubaliani na mapendekezo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa sababu
yanazima hoja yake.
Baadaye Lukuvi alisema anaunga mkono pendekezo
moja katika hoja ya Zitto la Serikali kuwasilisha bungeni ripoti ya
uchunguzi katika Bunge la 11 na kwamba ili kasi hiyo iende vizuri
yashirikishwe pia kampuni binafsi ya uchunguzi.
Mbunge wa Kisesa,
Luhaga Mpina (CCM), alipinga pendekezo la kuiondoa hoja hiyo na kuunga
mkono azimio kwamba Bunge liiagize Serikali kufanya uchunguzi huo na
ripoti yake iwasilishwe katika Bunge la 11 na ikishindwa, Bunge liunde
kamati ndogo ya kufanya kazi hiyo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu, (Tamisemi), Hawa Ghasia, aliuanga mkono mapendekezo ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali akisema vyombo vya uchunguzi viachiwe kuchunguza
mabilioni ya fedha yaliyopo nje ya nchi.
Mbunge wa Simanjiro,
Christopher Ole Sendeka (CCM), alipinga akisema mapendekezo ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali yalikuwa na lengo la kuua hoja hiyo akisema
wabunge watafanya dhambi kubwa kuiondoa hoja hiyo ya msingi.
Sendeka
alitaka hoja hiyo iboreshwe kwa kumtaka Zitto awataje hadharani watu
ambao wameficha fedha nje ya nchi ili Watanzania wawafahamu...
“Ukiwataja hawa hoja yako itakuwa na mashiko, tusaidiane na wala siyo
fedheha kuwataja.”
Alitaka kamati iundwe kuchunguza jambo hilo ili ukweli ujulikane.
Baada
ya kubanwa na wabunge, ndipo Jaji Werema alisimama na kulegeza msimamo
wake kwa kurejesha pendekezo la Serikali kushirikiana na vyombo vingine
vya uchunguzi vya nje pamoja na wachunguzi binafsi kufanya kazi hiyo.
Alikubali pia pendekezo la kuitaka Serikali kuja na mkakati wa kueleza nini imekifanya katika Bunge la 11.
Aliwataka wabunge wote wenye majina ya watu walioficha fedha nje ya nchi kuyapeleka Takukuru au wamkabidhi yeye.
Baada
ya hapo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisimama na kusema hoja ya Zitto
haikuwa mbaya na kusema Mwanasheria Mkuu pia alikuwa na nia njema.
Alisema
Serikali haiwezi kumficha mhalifu akisema kama mtu ameiba atachukuliwa
hatua bila ya kumwonea haya. Aliungana na Mwanasheria Mkuu kutaka
Serikali iachiwe jambo hilo ilifanyie kazi.
Akihitimisha mjadala huo,
Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema hoja ya Zitto haijatupwa bali,
inaingia kwenye utaratibu wa Serikali wa kuyatekeleza maazimio hayo.
Alisema
Serikali itapaswa kutoa taarifa ya utekelezaji wa hoja ya Zitto katika
Bunge la 11 la Aprili) mwakani na kama ikishindwa, Bunge litaunda kamati
kufanyia uchunguzi maazimio hayo.
Msimamo wa Zitto
Akizungumza baada ya uamuzi huo wa Bunge, Zitto alisema ameridhishwa na hatua hiyo akiamini kwamba itafanyiwa kazi.
Alisema amefurahi pia kwa kuwa hiyo ni mara yake ya kwanza kwa hoja yake kufanyiwa kazi na Bunge.