Saturday, September 10, 2011

FAINALI ZA MASHINDANO YA MISS TANZANIA NI LEO JUMAPILI TAREHE 11, 2011


KITENDAWILI cha nani ataibuka kuwa Vodacom Miss Tanzania 2011 kitateguliwa leo usiku ambapo warembo 30 kutoka mikoa mbali mbali ya Tanzania wakichuana kuwania taji hilo.

Ni ukweli usiofichika kuwa mashindano ya mwaka huu ambayo ni ya 18 tokea kuanzishwa kwake mwaka 1994 ni ya kihistoria kutokana na sababu mbali mbali. Mbili kubwa ni mashindano ambayo yatakuwa moja ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru na pili ni mshindi wa mwaka huu atazawadiwa zawadi nono tokea kunzishwa kwa mashindano hayo.

Mwaka huu mrembo atapewa zawadi ya Jeep Patriot model ya mwaka huu yenye thamani ya shs. Milioni 72 huku akipewa fedha taslimu sh. Milioni 8. Hii ni zawadi ya kihistoria kwani imevunja rekodi ya mwaka 2003 ya Sylvia Bahame ambaye alizawadiwa gari aina ya Nissan Hardbody yenye thamani ya shs milioni 55 na fedha taslimu shs. 7 million.

Ikumbukwe mwaka jana ambapo mrembo anayemaliza muda wake, Geneieve Mpangala alipewa gari maarufu kwa jina la Mkoko na fedha taslim shs milioni 10 na kufanya jumla ya zawadi zote kufikia milioni 20.

Hii ni hatua kubwa kwani tofauti ya shs milioni 60 si haba na zawadi ya kwanza imewafanya warembo wengi kupagawa kwani hawakuamini macho yao kile walichokuwa wanakiona.

Zawadi nyingine za washindi ni sh. Milioni 6.2 kwa mshindi wa pili, sh. 4 millioni kwa mshindi wa tatu na sh. Milioni 3 kwa mshindi wane. Mshindi wa tano atapewa sh. Milioni 2.4.

Warembo watakaoshika nafasi ya sita mpaka 15 watapewa sh. Milioni 1.2 na waliobaki (16-30) watapewa kifuta jasho cha sh. 700,000.

ìTunatarajia kuwa mashindano magumu sana, hii inatokana na zawadi ya mshindi wa kwanza ambayo warembo wengi wameelekeza nguvu zao huko kwa sababu ya ukubwa wake na vile vile kiu ya kuiwakilisha nchi katika mashindano ya Dunia (Miss world) mjini London,î alisema meneja masoko wa kampuni ya kuuza magari ya CFAO zamani DT Dobie, Alfred Minja.

Minja alisema kuwa wametambua na kuamua kurudisha hadhi ya mashindano hayo ili kuleta mvuto wake wa awali kwani mwaka 2005, Nancy Sumari alizawadiwa nyumba iliyojengwa kule Tabata.

Tofauti na miaka ya nyuma, mashindano ya mwaka huu ni yana ugumu wa aina yake kutokana na ukweli kuwa imekuwa vigumu kujua nani ataibuka mshindi tofauti na mwaka jana, juzi na miaka ya nyuma.

Genevieve Mpangala ambaye atalivua taji lake alionekana wazi wazi kuwa hana mpinzani na hata wakati wa Miriam Gerald na Nasreem Karim. Ukali wa warembo hao ulikuwa wa aina yake na kupewa nafasi hata kabla ya kupanda jukwaani.

Ni vigumu kutabiri nani mshindi, nimefuatilia maonyesho mbali mbali ya televisheni wakiwa kwenye nyumba na mengine, ushindani ni mkubwa sana, lakini mshindi ni mmoja tu,alisema Rodrick Mwambene ambaye kupitia duka la Mama Tike aliwahi kudhamini mashindano mbali mbali ya vituo.


WALIOINGIA TOP 15:
Mwajabu Juma (Temeke, Miss Top Model), Rose Hurbert (Kaskazini, Vipaji), Alexia Williams (Ilala, Miss Personality), Tracy Mabula (Kanda ya Ziwa, Miss Photogenic), Loveness Flavian (Kanda ya Mashariki, Mrembo bora wa michezo).


WANAOWANIA TOP 15:
Weirungu David, Neema Mtitu (Chuo Kikuu Huria), Cynthia Kinasha (Temeke), Zerulia Manoko, Christina Mwenegoha (Kanda ya Kati), Jeniffer Kakolaki, Salha Israel (Ilala), Dalila Ghribu, Maua Kimambo (Kanda ya Kati), Blessing Ngowi, Glory Lory (Elimu ya Juu), Stacey Alfred, Zubeda Seif (Kanda Kaskazini), Stella Mbuge, Husna Maulid, Hamisa Hussein (Kinondoni), Princess Chiaro Masonobo (Udsm), Atu Daniel, Leila Juma, Christine William (Nyanda za Juu Kusini) , Mariaclara Mathayo, Asha Saleh (Mashariki), Irene Karugaba, Glory Samwel (Kanda ya Ziwa).


Warembo wanaoiwakilisha Dar es Salaam:

Weirungu David, Neema Mtitu (Open University), Mwajabu, Cynthia Kinasha, Husna Twalib (Temeke), Alexia Williams, Jeniffer Kakolaki, Salha Israel (Ilala), Blessing Ngowi (Institute of Social work), Glory Lory (IFM), Stella Mbuge, Husna Maulid, Hamisa Hussein (Kinondoni), Princess Chiaro Masonobo (Udsm).


KIINGILIO: SHS. 100,000

BURUDANI
Diamond, kidumu, Juliana, Akili the Brains, Bob Junior maarufu kama Rais w Sharobaro,

MAJAJI WA MWAKA HUU:
Prashant Patel, Crescentius Magori, Victoria Lukindo, Cynthia Masaki, John Njoroge, Benard Mlunya , Javier Diz Rio, Martin Ngadada, Pratma Shah.

WAREMBO WA MIAKA YA NYUMA:
1994 -Aina Maeda,
1995- Emily Adolf
1996- Shose Sinare
1997 - Saida Kessy
1998- Basila Mwanakuzi
1999- Hoyce Temu
2000 - Jacqueline Ntuyabaliwe
2001- Happiness Magese
2002- Angela Damas
2003- Sylvia Bahame
2004- Faraja Kotta
2005 - Nancy Sumari alishinda taji la Miss World Africa
2006- Wema Sepetu
2007- Richa Adhia
2008- Nasreen Karim
2009- Miriam Gerald
2010 - Genevieve Emmanuel

TALAKA SI SURUHISHO LA MATATIZO YA UHUSIANO, SURUHISHO NI KUONGEA NA MWENZA WAKO

Watu bwana, wakikwaruzana ‘Nenda kwenu mbwa wee’…wengine ‘Nipe talaka hunifai!”
“MBWA wewe, najuta sijui kwanini nilikuoa, yaani kati ya wanawake, wewe si lolote, pumbavu kabisa….” Ni kati ya kauli ambazo wanawake wamekuwa wakikumbana nazo kwenye ndoa.

Kama wewe mwanamke uko kwenye ndoa ambayo haina majuto na kero, ni suala la kumshukuru Mungu. Ukweli ni kwamba kuna wanawake wengi wanateswa na wanaume.

Usione wanaume mitaani, usifikiri mwanaume ambaye unakwenda naye gesti na kuachana, ndivyo anavyokuwa kwenye ndoa, wengi ni kero. Si wengi ambao wanawaheshimu wake zao.

Baadhi ya wanaume ni wasomi, ni watu maarufu, lakini kwenye nyumba zao ni takataka. Hawana heshima kwa familia, ndio unaweza kuona kwa mfano baba mtu mzima, anakataa kutoa huduma kwa watoto, eti kisa kagombana na mkewe. Akili iko wapi ndugu yangu kama sio upumbavu?

Kuna wanaume, eti mkewe haruhisiwi kupanda kwenye gari, anapandisha machangudoa…huu ni upumbavu. Dalili kwamba huna akili ni kuendekeza vitu ambavyo haina maana katika maisha. Kuna wanaume wengi hawana akili. Wanachojua wao ni kutembea kwenye nyumba nzuri za starehe na makahaba.

“Mke wangu amekuwa kero, dawa yake naona ni ndogo tu kumchukua nyumba ndogo” ndivyo wengi wanavyojidanganya. Wanafikiri kwamba nyumba ndogo ni mali, lakini nyumba ndogo hawa ni wafanyabiashara, wanachokifanya ni kwamba anakusikiliza eeeh mke wangu hana maana, hanipi raha, eeeh ooh na ujinga mwingine mwingi unamwambia.
Yeye yuko kibiashara zaidi, kwamba anaangalia matatizo uliyonayo kisha anajitahidi kufanya kila linalowezekana kuhakikisha unapata raha, hasa kwa sababu anaamini yuko kibiashara kwa maana kuwa utampa fedha na mambo mengine kama haya.
Nyumba ndogo ni wezi, ni majambazi, na ni wafanyabiashara, baadhi yao huwa wanakuwa bize kujifunza namna ya kuwanasa wanaume. Kuna wengine wanasoma vitabu mbalimbali vya mahaba, ili kumnasa mwanaume asikumbuke kwao.
Kwa wanaume wasio na akili, wanafikiri wanayofanyiwa ni kwa upendo, kumbe hakuna lolote la maana. Bali kinachofanywa na nyumba ndogo ni kusaka njia za kuishi kupitia migongo ya hao wanaume.
Mwanaume mwenye akili timamu ataangalia namna ya kuondoa kasoro zilizoko kwenye nyumba yake. Ndugu zangu tunapokuwa na shamba kama kwa mfano umepanda mahindi na kumeota magugu, kinachofanyika sio kwamba huwa tunang’oa mahindi na kwenda kuyapanda kwenye shamba jingine, bali tunasaka dawa ya kuua magugu ili mahindi yaweze kuota vizuri.

Kuna wanawake pia wana kauli za ujeuri, eeeh kuna wengine kama ulimgusa jana, ukimwambia na leo tena nataka ‘tupigane’ anaanza kulalamika “aaah bwana eeeh nataka kupumzika, aaah jana umetaka na leo unataka kwani mimi ng’ombe, hata ng’ombe huwa wanapumzika’.

Kauli chafu hazitakiwi katika suala zima la ndoa. Kama kweli unaumwa au una jambo linakusumbua, ni suala la msingi kuzungumza taratibu. Acha kuwa mwenye kauli chafu kwa mkeo, acha kuwa na kauli chafu kwa mumeo.
Kuna watu wengeine, wakikwaruzana kidogo ‘Nenda kwenu mbwa wee’…wengine utawasikia wanasema ‘Nipe talaka hunifai!” Ndoa nzuri huwa inajengwa kwa maneno na fikra za kila mtu kuamini kuwa hata kama kunatokea migogoro, cha msingi ni kuangalia chanzo cha mgogoro na kuumaliza. Utaachana na wangapi?
Kuringa kwenye ndoa kwa sababu eti una mwanamke mwingine nje ya ndoa ni upumbavu…kuringa labda una mwanaume mwingine nje ya ndoa ni ujinga.Mtu mwenye akili sahihi na iliyo timamu, baada ya ndoa anachokiangalia ni namna ya kuboresha maisha yake.

Kuna wanaume wanawapiga sana wake zao, wanasema maneno mabaya. Lakini mwanaume kama kichwa cha familia, anapaswa kuwa na akili nzuri, anapaswa kuwa mfano wa kuigwa, kwa kuwa na kauli nzuri, sio ndio jamani?

Sasa kwabahati mbaya kuna watu ni vichwa, lakini matendo yao ni sawa na unyayo sijui maana hata nikisema ni sawa na kiuno bado hawafai. Je wewe mwanaume unaishije na mkeo au watoto kwenye familia yako? Eti kuna wanaume wanaamini nyumba ndogo ni kila kitu katika maisha…eti akigombana na mkewe ndio atakwenda kupata faraja!!!

Ndugu yangu mbona unakuwa huna akili kiasi hiki. Unapotoka nje, kwanza ni kwamba uniaibisha mwenyewe, yule ambaye uko naye kwa asilimia kubwa hata kama anakuchekea, kwanza anajua yuko kibiashara, lakini katika nafsi yake anaamini wewe ni mwanaume usiyefaa, kama uliyeweza kumdharau mkeo na watoto, utashindwa nini kumdharau yeye ambaye hauna naye mikataba yoyote?

Kama ni suala ni migogoro ndio inakumbikiza nyumbani, kwani unafikiri ni mtu gani ambaye unaweza kuishi naye bila kukwaruzana? Wewe umeishi kwenye tumbo la mama yako kwa miezi sijui tisa au chini ya hapo, na bado kuna wakati mnakwaruzana, iwe mtu tu mmekutana mitaani?

Migogoro ni jambo la kawaida katika uhusiano wa kimapenzi au ndoa. Cha msingi ni kufungua milango ya kujadiliana. Tatizo kubwa kuna watu wana kiburi kichafu kabisa, kwamba hawezi kusema nimekosa nisamehe….hata kama kweli amekosa. Ndoa haiwezi kwenda kokote kama watu wake hawako tayari kusameheana au kuomba msamaha

MELI YAZAMA ZANZIBAR, WATU ZAIDI YA 190 WAFA


WATU 160 wamefariki dunia na wengine 521 kujeruhiwa baada ya meli ya abiria LCT Spice Islanders, iliyokuwa ikisafiri kutoka Unguja kwenda Pemba, kupinduka na kuzama baharini.

Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa meli hiyo iliyokuwa imebeba abiria zaidi ya 600, ilizama usiku wa kuamkia jana kwenye Bahari ya Hindi kati ya Nungwi na Pemba, kilomita 20 kutoka Bandari ya Zanzibar.

Kwa mujibu wa habari hizo, meli hiyo iliyotokea Unguja kwenye Bandari ya Malindi, ilipata hitilafu ikiwa njiani, kisha ikapinduka na kuanza kuzama taratibu. Ilikuwa na makoti ya uokoaji 200 tu.

Mwandishi Mkongwe nchini, Salim Salim, aliambia gazeti hili kwamba juhudi za kuoka zilianza kufanyika mapema kwa ushirikiana wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), KMKM, Jeshi la Polisi na wananchi kutoka eneo la Nungwi.

Salim alisema saa tata baada ya ajali hiyo kutokea jeshi la polisi lilifika katika eneo la polisi pamoja na wananchi walitoka sehemu mbalimbali. Polisi walitumia helikopta mbili na wananchi asilimia kubwa akiwa wavuvi walitumia mashua.

Pia boti za uokoaji za Azam na Express Zakhir zilifika katika eneo la tukio mapema na kuifanya kazi kubwa ya uokoaji.


Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP, Said Mwema alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo jana na kwamba chanzo cha ajali hiyo bado hakijajulikana.

Alisema mpaka kufikia jana mchana watu waliokolewa katika ajali hiyo wakiwa hai walikuwa 525 na waliofariki 62.

Mwema alisema imeunda kamati maalum ya kufuatilia tukio hilo ambayo pia itahusisha Usalama wa Taifa.

“Hivi sasa Jeshi la Polisi, JWTZ, Usalama wa Taifa, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na KMKM ndio wanashughulikia suala zima la upelelezi ili kujua chanzo cha ajali hiyo,” alisema Mwema

Aliongeza: “ Eneo la Usimamizi wa mawasiliano na uratibu itakuwa chini ya Kamishna wa Polisi Zanzibar, pia kuna kikosi kazi cha uokoaji na kikosi cha kukusanya taarifa na upelelezi wa tukio hilo,”.

Alipoulizwa idadi kamili ya watu waliofariki katika ajali hiyo pamoja na uwezo wa meli hiyo kubeba abiria na mizigo Mwema alisema: “Hivi sasa ndio tunaendelea na uchunguzi ili kubaini idadi kamili ya waliofariki, ila kwa sasa kinachofanyika ni uokoaji”.

Rais Shein

Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, alifika kwenye eneo la tukio na kushiriki kikamilifu kutoa huduma ya kwanza kwa walinusurika katika ajali hiyo.

Akizungumza katika kijiji cha Nungwe, Dk Shein aliwataka Wazanzibari kuwa wavumilivu katika kipindi hiki wakitiana moyo kwa yote yaliyotokea.

"Huu ni mtihani wa Mwenyezi Mungu. Wazanzibari tuwe wavumilivu, Serikali itakayogharimia shughuli zote za mazishi," alisema Dk Shein.

Dk Shein alisema maiti waliotambuliwa watachukuliwa na ndugu zao kwa ajili ya mazishi ila wale ambao ndugu hawataonekana watazikwa na Serikali kwa utaratibu maalumu.



Shuhuda
Mwandishi Mkongwe wa habari Zanzibar, Salim Salim, amelieleza gazeti hili kuwa meli hiyo ilizama katikati ya Kisiwa cha Pemba na Unguja eneo ambalo ndilo lenye mkondo mkuu bahari kuliko mikondo yote ya bahari barani Afrika.

Mikondo mingine mikuu ya bahari inayoufuatia mkondo wa Bahari wa Nungwi ni Pemba Channel ulioko nchini Msumbiji na Affond ulioko Somalia

Alisema ajali hiyo ilisababisha maduka yote kisiwani Pemba kufungwa kutokana na wakazi wengi wa pemba kwenda kutambua miili ya marehemu, iliyofanyika katika Viwanja vya Maisara vilivyoko kiwani humo.

"Wananchi walianza kutambua miili ya marehemu saa 8:30 mchana wakiwamo viongozi wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar walioongozwa na Rais Shein na Makamu wake wa Kwanza, Maalim Seif Sharif Hamad.

"Maduka yote yamefungwa na misikitini kunafanyika sala maalumu. Pia vituo vyote vya radio na televisheni visiwani hapa, vimeacha kupiga muziki na pia kutakuwa na maombolezo maalumu ya ajali," alisema Salim.

Salim alisema katika viwanja hivyo vya Maisara walikusanyika madaktari kutoka maeneo mbalimbali ya Zanzibar ambao kwa pamoja wanatoa huduma ya kwanza katika mahema maalum kwa majeruhi.

"Sanda zinashonwa hapohapo uwanjani na Serikali imesema itagharimia shughuli zote za mazishi," alisema Salim.

Salim alisema maiti zote zilizokuwa zikitolewa, zilikuwa zimepewa namba na mpaka anaondoka uwanjani hapo jana mchana, maiti 160 zilikuwa zimeopolewa.

"Kazi ya uokoaji inaendelea ila mpaka mimi naondoka eneo la tukio, kulikuwa na maiti 160. Niseme tu kwamba, Serikali safari hii imeonyesha kuwajali wananchi wake, kwa kuharakisha kuanza uokoaji," alisema.


Dk Shein ashiriki kutoa
huduma ya kwanza

Katika hatua nyingine, jana Rais Shein alikuwa miongoni mwa madaktari waliokuwa wakitoa huduma ya kwanza kwa majeruhi wa ajali hiyo ya meli.

Dk Shein ambaye siku nzima alikuwa katika eneo la tukio, akishirikiana na madaktari kuwapokea wagonjwa katika mahema maalumu na kuwapa huduma ya kwanza.

Watu wengi walionusurika katika hali hiyo walionekana kupata mshituko mkubwa, ingawa hawakuwa na majeraha makubwa.
Kazi hiyo ya uokoaji ilikuwa ikiongozwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na KMKM.
Wakati Dk Shein akiwa anashiriki kutoa huduma ya kwanza kwa majeruhi, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad alionekana muda wote akiwa sambamba na vikosi vya uokoaji akisimamia kwa karibu zoezi hilo.

"Maalim Seif alionekana akisimamia upatikanaji wa vifaa na vitu vingine muhimu vya uokoaji," kilisema chanzo cha habari kutoka Pemba

Kichanga aokoka kifo

Katika hali isiyokuwa ya kawaida mtoto mchanga anayekadiriwa kuwa na umri wa miezi minne hadi mitano, aliokolewa katika ajali hiyo.

Televisheni ya Channel Ten, ilieleza kuwa mtoto huyo alikutwa akielea juu ya maji licha ya kutovalishwa kifaa chochote maalumu vya kuogolea. Kwa mujibu wa Kituo hicho cha Televisheni, mtoto huyo anaendelea vizuri.

Sumatra wazungumza

Akizungumza na Mwananchi Jumapili Meneja Mawasiliano kwa Umma wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), David Mziray.
Alisema taarifa walizonazo zinaeleza kuwa meli hiyo iliondoka Unguja kwenda Pemba saa 4:20 usiku jana.

“Mpaka sasa meli ya Mv Jitihada imeelekea eneo la tukio kwa ajili ya kuokoa watu, meli ilikuwa na abiria 500 na wafanyakazi 12,” alisema Mziray.

Aliongeza: “Meli hii imesajiliwa Zanzibar na taarifa za kuzama kwake zilifika saa 9:10 usiku wa kuamkia leo(jana),”.

Kikosi cha wanamaji Dar
Awali gazeti hili lilifika katika ofisi za kikosi cha wanamaji jijini Dar es Salaam na kuelezwa kuwa meli hiyo iliondoka jana (juzi) jioni ikiwa na abiria 229.

Akizungumza na Mwananchi Jumapili kwa njia ya simu akiwa njiani kuelekea ilipozamia meli hiyo Kamanda wa Kikosi hicho, Mboje Kanga, alisema meli hiyo ilizama ikiwa na zaidi ya watu 500.

“Mpaka sasa sijui kinachoendelea ndio niko njiani naelekea eneo la tukio, nipigie baadaye nitakuwa nimetapa kila kitu,” alisema Kanga.

Wafanyakazi Bandarini
Baadhi ya wafanyakazi wa bandarini pamoja na wabeba mizigo walilieleza gazeti hili kuwa huenda meli hiyo ilizama kutokana kubeba mizigo mingi.
Wafanyakazi hao ambao walikuwepo katika bandari hiyo wakati ikiondoka katika bandari ya Zanzibar wanasema kuwa jinsi ambavyo ilipakia abiria na mizigo huenda itakuwa ndiyo sababu ya kuzama kwake.
Mmoja wa wafanyakazi hao ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema wakati meli hiyo ikiondoka Unguja alikuwepo na kwamba ilikuwa imeelemewa upande mmoja.
“Meli iliruhusiwa kuondoka bandarini Unguja kwa nguvu kwa kuwa watu waliokuwa wakitaka kupanda licha ya kuwa kuambiwa imejaa na walikuwa wengi. Meli ilipakiwa idadi kubwa ya nondo, madirisha, magunia ya unga wa ngano na mahindi,” alisema.
Mfanyakazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Shadrack alisema meli nyingi zinazotoka Unguja kwenda Pemba huwa zinajaza mizigo na watu wengi na kusisitiza kuwa, eneo la Nungwi ni baya hasa kama meli ina mzigo mkubwa kwa kuwa eneo hilo lina mkondo mkubwa wa maji.
“Nakwambia wazi meli hii ilikuwa na watu zaidi ya 600 maana wanasema waliookolewa tu ni 500…,” alisema Shadrack.

Hekaheka Bandarini Dar
Mwananchi Jumapili lilifika asubuhi bandarini jijini Dar es Salaam na kuta idadi kubwa ya watu wakitafuta usafiri wa meli kuelekea Zanzibar kwenda kutambua ndugu zao waliokuwa katika meli hiyo.
Ally Hamisi alilieleza gazeti hili kwamba, katika meli hiyo kulikuwa na ndugu zake saba ambao hajui kama wako hai ama wamekufa.
“Walikuwa wametoka katika harusi…, kwa kweli nimechanganyikiwa kabisa, pia alikuwemo jirani yangu ambaye nilikabidhiwa ili nimpeleke Zanzibar na mpaka sasa hajaonekana,” alisema Hamis.
Alisema meli hiyo ilipofika Unguja walipanda ndugu zake wengine watatu.
“Ni jambo la kusikitisha sana, usiku nilipigiwa simu na mmoja wa ndugu zangu akanieleza kuwa tumuombee kwa kuwa meli ilikuwa ikizama, baadaye simu yake haikupatikana tena na sijui kama yupo salama au la,”.
Naye Khamisi Abdallah alisema kwa masikitiko kuwa katika meli hiyo alikuwa na ndugu 10.
“Nimekata tiketi ili niende kushuhudia mwenyewe…, mpaka sasa siamini na sijui nani kapona nani kafariki, inaniuma sana,” alisema Abdallah kwa masikitiko.
Mwantumu Suleiman ambaye ni mkazi wa Zanzibar, alisema alikuja jijini Dar es Salaam na mume wake na mdogo ambao waliondoka na meli hiyo.
“Wao walikwenda ila mimi nilibaki hapa Dar es Salaam nilikuwa naumwa tumbo, niliposikia habari hizi nimechanganyikiwa kweli, bado sijapona, lakini acha niende nikashuhudiwa kilichotokea,” alisema Mwantumu kwa masikitiko.

Hii ni mara ya pili meli kuzama katika bahari ya Malindi katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Mei 29, 2009, meli ya mizigo inayomilikiwa na Kampuni ya Seagul, MV Fatih, ilipinduka na kuzama katika Bandari ya Malindi, Zanzibar na kuua watu watatu na kujeruhi wengine 27.

Meli hiyo ilipinduka na kuzama ghafla ikiwa tayari imeshafunga gati katika Bandari ya Malindi majira ya saa 4.00 usiku na abiria waliokuwemo walikuwa wanataka kushuka.

Akisimulia mkasa wa ajali hiyo kepteni aliyekuwa akiendesha meli hiyo, Ussi Ali Ussi, alisema wakati akiingia bandarini ghafla aliona meli hiyo ikijaa maji na kulala upande wa kushoto.

Habari hii imeandaliwa na Talib Hamad, Fidelis Butahe, Claud Mshana, Elias Msuya na Geofrey Nyang’oro, Igunga