Kikwete alia na mawaziri mizigo | Send to a friend |
Monday, 09 May 2011 21:54 |
0diggsdigg Habel Chidawali, DodomaRAIS Jakaya Kikwete amewataka mawaziri na makatibu wakuu kujiamini katika utendaji wao wa kazi badala ya kutegemea maelekezo ya mamlaka zilizo juu yao.Alisema hayo jana alipokuwa akifungua semina elekezi kwa viongozi na watendaji wakuu wa Serikali iliyofanyika katika Ukumbi wa St Gasper nje kidogo ya Manispaa ya Dodoma.“Hadi leo sijui kwa nini hasa watu (mawaziri) wanashindwa kuzungumza mambo yaliyofanywa na Serikali na kuwapa uwanja mpana wenzetu wa upande wa pili (wapinzani) ambao wanajua kweli kuvitumia vyombo vya habari. Sisi tunaendelea kulalamika kila siku kwamba hatuandikwi, nani atakuandika wakati hutoi taarifa,” alisema Kikwete. “Kuna wakati waziri mmoja aliwahi kunipigia simu na kusema 'Mheshimiwa Rais habari hii tuikanushe?' Nilichokifanya nilimwambia pima wewe baada ya hapo nikakata simu,” alisema Rais Kikwete alisema kitendo cha mawaziri kukataa kutoa habari na kuwafanya maofisa habari wa wizara kuwa kama waandishi wa habari ni hatari kwa serikali. Katika hotuba yake, Rais Kikwete aliwataka watendaji hao kufanya kazi kwa kufuata misingi ya Katiba, sheria, kanuni na taratibu ili kukwepa hasara inayoweza kutokana na uamuzi usiofuata kanuni na kuiaibisha Serikali. "Ni muhimu kwenu kama viongozi mkajielimisha juu ya Katiba, sheria, kanuni na taratibu mbalimbali zinazoongoza utendaji kazi katika sehemu zenu za kazi. Uhalali wa maamuzi mtakaoyafanya hupimwa na sheria," alisema Kikwete na kuongeza: "Ukifanya uamuzi unaokinzana na sheria utahojiwa wewe binafsi lakini pia utaibebesha Serikali mzigo wa hasara na fedheha itakayotokana na uamuzi huo. Uamuzi usiofuata sheria unaweza kuwa na madhara kwa wananchi. "Heshimuni Katiba na fuateni sheria, kanuni na taratibu zilizopo katika utekelezaji wa majukumu yenu. Katika semina hii masuala hayo yatafafanuliwa na kuzungumzwa. Kadhalika, uhusiano wa Serikali na mihimili mingine ya dola yaani, Bunge na Mahakama utafafanuliwa." Rais Kikwete pia aliwataka watendaji hao kuepuka kauli na vitendo vinavyoweza kuwafarakanisha na kuleta mgawanyiko katika Serikali ili kulinda dhana ya uwajibikaji wa pamoja. "Viongozi na watendaji wakuu wa wizara hamna budi kujenga uhusiano mzuri na uwajibikaji wa pamoja. Haifurahishi kuona waziri na katibu mkuu au waziri na naibu waziri; naibu waziri na katibu mkuu au katibu mkuu na naibu katibu mkuu hawaelewani." "Wanasemana na hata wanapingana hadharani, yaani mbele ya wafanyakazi. Baya zaidi ni pale wanapopingana katika vyombo vya habari kuhusu uamuzi au utendaji wa wizara au serikali kwa jumla. Hayo si maadili mema katika taasisi yoyote. "Kama unaona vigumu kuuafiki ni bora kutoka. Hairuhusiwi kupinga taasisi ambayo wewe umo ndani kama mmoja wa viongozi wake. Ni vyema hili likaeleweka. Msitupe tabu ya kuulizana maswali na kuwasemea." Rais Kikwete pia aliwataka watendaji hao kuwa mstari wa mbele kuzungumzia mafanikio ya Serikali ili kuziba midomo ya wapinzani wanaopita kila kona nchini na kuwaeleza wananchi kuwa haijafanya chochote. "Sijui kwa nini hatuwi wepesi kuyasemea mafanikio mengi tuliyoyapata tukaacha wasiotutakia heri wanaosema hatukufanya kitu wasikike mpaka waonekane wanasema kweli," alisema. Alisema hajui na hana majibu mazuri ya kwa nini Serikali imekuwa ikishindwa kuzungumza mambo mazuri yaliyofanywa katika kipindi cha miaka mitano na hata wakati mwingine kushindwa kuzungumza jambo hadi wampigie simu, kitu ambacho ni aibu. Alisema kuna udhaifu katika kujipanga kwa wasemaji kutokana na kuchelewa kutoa taarifa au kukanusha habari ambazo zimekuwa zikitolewa na upinzani, jambo linalowafanya wananchi waamini kuwa ni kweli, kwani uongo ukizungumzwa mara nyingi hugeuka na kuwa ukweli. “Unajua mimi sijui hadi leo ni kwa nini hasa watu wanashindwa kuzungumza mambo yaliyofanywa na serikali na kuwapa uwanja mpana wenzetu wa upande wa pili ambao wanajua kweli kuvitumia vyombo vya habari huku sisi tunaendelea kulalamika kila siku kwamba hatuandikwi, nani atakuandika wakati hutoi taarifa,” aliuliza Kikwete. Alikanusha madai kuwa baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikiandika habari za upinzani na kuacha habari nzuri za serikali na badala yake akasema woga na urasimu uliowajaa wasemaji katika serikali, ndilo tatizo hasa kwa kuwa hawajui kuwa vyombo vya habari vinatafuta habari na kama wao hawatoi habari ni lazima waandike zile zinazotolewa na upande wa pili. Katika hatua nyingine, Kikwete alisema kuwa anategemea kuona Serikali yake ikifanya kazi kwa umoja na ushirikiano mkubwa katika kipindi hiki cha miaka mitano na kwamba kushirikishana na kupeana habari iwe ndiyo dira ya maendeleo yao. Sikuteua mawaziri wa kusoma mafaili ofisini Aliwataka viongozi hao kuacha umangimeza, badala yake watoke ofisini kujionea matatizo ya wananchi. "Mawaziri na makatibu wakuu lazima mtoke. Hiyo ndiyo njia bora zaidi ya kujua mambo yahusuyo wizara zenu na ndiyo njia bora ya kuongoza: kuona wenyewe na kutenda," alisema Rais Kikwete na kuongeza: "Hii itawafanya mjiamini kuelekeza na pia mnaposimama mbele za watu na kusema. Msiwe mamangimeza. Tokeni, tembeeni kuona shughuli zenu. Tembeleeni wananchi muwafahamu, wawafahamu, mjue shida zao muwatatulie." Alikemea tabia ya viongozi hao kushinda kwenye mitandao kila siku na kusoma ujumbe badala ya kwenda kuwatumikia wananchi vijijini.Alisema tabia hiyo haipaswi kuvumiliwa hata kidogo na akaonya viongozi wa namna hiyo wataishia kuwa wababaishaji na hatakwenda nao katika kipindi chake cha uongozi. “Mimi sikuteua mawaziri wa kusoma mafaili ofisini, bali niliteua watu wanaoweza kukimbizana kwa kasi zaidi, ari zaidi pamoja na nguvu zaidi, kwani nataka kuwasikia mkichakarika huko kwenye miradi mlikopeleka fedha, siyo kupokea taarifa ofisini bila ya kujua fedha za walipa kodi zinatumikaje huko.” Dawa ya mawaziri hawa ipo jikoni Rais Kikwete pia aliwatahadharisha mawaziri ambao wamekuwa wakipinga kauli na miswada ya mawaziri wenzao, huku wengine wakiwa wanatoa siri za Serikali.Alisema kuwa watu wa namna hiyo dawa yao iko jikoni kwa kuwa kitendo wanachokifanya si kizuri ndani ya Serikali. Alisema anayo mamlaka ya kuchagua na ya kumwondoa waziri wakati wowote akiamua, hasa kama haoni umuhimu wa kuendelea na mtu wa aina hiyo. “Katika hili nawaambia mapema kabisa kuwa waziri anayeishi kwa kupinga miswaada ya Serikali ajue kuwa anaipinga Serikali na hivyo sitakuwa tayari kufanya kazi na mtu wa aina hiyo. Sehemu kubwa ya kazi zenu mawaziri nataka ziwe za Serikali na zile za jimbo mtajua namna mtakavyojipanga bila ya kuharibu kazi za Serikali,” alisema. Pato la Mtanzania litakua miaka mitatu ijayo Rais Kikwete alisema kasi ya kukua kwa pato la Mtanzania ni ndogo na kwamba kunahitajika juhudi za makusudi katika kuongeza pato hilo. Hata hivyo, alitamba kuwa pato la Mtanzania litaongezeka katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia sasa kutokana na baadhi ya nchi wahisani kuahidi kuongeza misaada kwa Tanzania. Alisema katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake, umaskini umepungua kwa asilimia mbili tu hivyo, akaahidi kuwa katika kipindi cha miaka mitano ya awamu ya pili ya uongozi wake, umaskini utapungua kwa kiasi kikubwa. Alisema mkakati uliopo hivi sasa serikalini ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2025, Tanzania inakuwa nchi yenye uchumi wa kati pato la Mtanzania wa kawaida likitarajiwa kufikia Dola za Marekani 2,500 hadi 3,000. Sasa ni Dola 600. Kuhusu kipindi cha miaka mitatu, alisema kuwa, ipo mipango mizuri kutoka kwa wahisani, ikiwamo Benki ya Dunia ambayo imekubali kuisaidia Tanzania kiasi cha Dola 2.8 milioni ambazo zinaweza kusaidia katika kutengeneza ajira na kupambana na umaskini. Semina hiyo ilihudhuriwa na watendaji wote wa Serikali wakiwamo Waziri Mkuu, Jaji Mkuu, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, mawaziri na manaibu waziri, makatibu na naibu makatibu wakuu, Mwanasheria Mkuu na naibu wake, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na viongozi wastaafu, akiwamo Spika wa zamani na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa na Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa Msuya. |
No comments:
Post a Comment