Ikumbukwa moja ya mategemeo ya jamii ya wana Dodoma kutoka kwenye chuo cha UDOM kilipo anzishwa mwaka 2007 ilikuwa ni kujionea jamii staarabu iliyoelimika na yenye kila sifa ya kuigwa, na pia jamii ya Dodoma ilitegemea watoto wao wangejionea namna wasomi hawa wanavyoishi kwa kusadifu kwa vitendo elimu, maadili na mila za nchi yao. Zaidi waliamini mambo hayo yangekuwa chachu ya kuwachochea vijana wao kuzingatia masomo ili na wao siku moja wafikie elimu hiyo ya Chuo lakini hali imekuwa tofauti kabisa. Leo jamii hii ya wana Dodoma wanashuhudia wasomi wanaoshinda mitaani wakiranda randa na nguo za kuogelea na za kulalia kana kwamba walikotoka hakuna wazazi, wanashuhudia wasomi wanaojiuza kama njugu.
Kiukweli siwezi hata siku moja kuruhusu kulea au kuipamba tabia hizo hata kama kuna sababu za msingi ambazo zinaweza zikawa zimesababisha tatizo hili kutokea. Kinachofanywa na dada zetu hawa ni kitendo ambacho kila mungwana anapaswa kukikemea kwa nguvu, na zaidi ya yote ni wajibu wetu wote kama vijana kurudia maadili yetu kama watanzania na kulaani kwa nguvu haya. Kama tutaruhusu tabia hii ikaota mizizi tutaandaa wasomi wasio waadilifu na wasio jiamini, tutandaa wasomi wenye shahada za kwenye chupi (nisamehewe kwa hiyo lugha lakini nimekosa neon linalokidhi ninachomaanisha),tutandaa wasomi walioathirika hivyo kupoteza nguvu kazi ya taifa, tutaandaa taifa la wavivu na wasifikiri kwa ufanisi.
Tukumbuke kuruhusu tabia hii kubobea ni kuruhusu kuporomoka kwa elimu ambayo ni msingi wa taifa lolote duniani. Na sidhani kama ni busara kuangalia umauti wa taifa letu kwa kuruhusu tabia hii kuota mizizi, kwani dhambi hiyo haitaishia chuoni tu, itaingia makazini na hapatakuwa na kazi zaidi ya uzinzi tu, baada ya hapo dhambi hii itasambaaa hadi kwa watoto na wajukuu wetu na hatimaye itakuwa ndio mfumo wetu wa maisha. Lakini mbali na yote niliyoeleza hapo juu ninayo yangu kwa serikali yangu, vijana hawa wa UDOM ni watoto wenu na wengine wameingia pale wakiwa hawana hata elimu ya kimaisha au ya kujitegemea, wengine wanakutana na kila aina ya tabia pale.
Mimi nilisha kuwa kiongozi wa mikopo UDOM-HSS kwa karibu miaka yote ya masomo yangu ya shahada ya kwanza, naelewa kiasi sababu na wakati dada zetu hawa wanapojiuza. Kipindi ambacho dada zetu hawa hujiuza huwa ni pale Bodi ya mikopo inapochelewesha mikopo ya wanafunzi, hali huwa mbaya kiasi dada zetu hawa ufika mahali wanalazimika kujidhalilisha ilimradi wapate chochote cha kujikimu. Na ukizingatia majumbani kwao hawa msaada wowote wanaoupata.
Mfano mzuri wa ucheleweshaji wa mikopo kwa wanafunzi wa kozi ya Uhusiano wa Kimataifa (BA IR) hawajapewa mikopo yao mpaka leo, na wanatakiwa kula, kunywa, kuwasiliana na kununua vitini vya masomo ili hali familia walizotoka ni masikini wa kutupwa. Haya yote ni mazingira hatarishi kwa dada zetu hawa. Serikali kama mzazi nakuomba mliangalie kwa umakini sana suala hili ili tuwaepushie wale wanajihusisha na tabia hii ya kuuza miili yao kutokana na kuishiwa au kukosa fedha za kujikimu Muda mwingine unaweza kusema serikali inafanya makusudi kuwacheleweshea mikopo yao wa sababu wanaonufaika sana na tabia hiyo ya dada zetu kujiuza ni wabunge wanapokuja kwenye vikao vyao vya bunge.
Kujiuza kwa dada zetu hawa ni dhahiri ni matokeo ya mambo kadhaa ambayo serikali haina budi kuyafuatilia kwa kina na hatimaye kutatua kwa ustawi wa tafa letu la Tanzania. Hatupaswi kufurahia tabia hii hata kidogo kwan kufanya hivyo kunaweza liathiri taifa letu kwa ujumla wake siku za usoni.
……………“ukiona panafuka moshi ujue kuna moto”…………
No comments:
Post a Comment