Hakielimu watangaza utafiti kuhusu elimu | Send to a friend |
Wednesday, 06 April 2011 21:54 |
0diggsdigg Fidelis Butahe na Hussein IssaTAASISI ya Hakielimu, imetoa ripoti ya utafiti kuhusu uhusiano wa ubora wa mitaala na utoaji wa elimu bora, unaonyesha kuwa mtaala wa elimu wa Tanzania, hauna uwezo wa kutoa wahitimu mahiri, katika nyanja mbalimbali. Utafiti huo unasema asilimia 79.9 ya walimu walipendekeza kutumika kwa kitabu cha aina moja cha kiada katika kufundishia wanafunzi wa shule zote nchini.Ripoti hiyo inasema ni asilimia 20 tu walimu, ndio waliopendekeza kuendelea kwa sera ya sasa ya kutumika kwa vitabu vya kiada vya aina mbalimbali. Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya utafiti, vitabu vingi vya kiada, haviendani na muhtasari rasmi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, jambo linalochangia katika kuwapotosha wanafunzi. Utafiti huo ulifanyika Agosti mwaka jana katika wilaya sita nchini na kuhusisha maofisa elimu wa wilaya, walimu, wanafunzi na wazazi.Unaonyesha kuwa baadhi ya vitabu vina makosa makubwa ya kimaudhui na lugha na hivyo kuwafanya wanafunzi, washinwe kuunganisha kinachofundishwa na kile wanachotarajia kupata. Akizungumza wakati wa kuwasilisha ripoti hiyo, Mchambuzi wa Sera wa taasisi hiyo, Mtemi Zombwe, alisema ni asilimia 35 tu ya walimu na asilimia 26 ya wanafunzi, ndio walioripoti kuwa mitaala unafaa katika kuandaa wahitimu mahiri wenye kujiamini Alizitaja wilaya ambazo utafiti huo umefanyika na mikoa ya wilaya hiyo katika mabano kuwa ni Monduli (Arusha), Mafinga (Iringa), Pangani (Tanga), Misungwi (Mwanza), Uyui (Tabora) na Bukombe (Shinyanga). "Katika utafiti huu walimu, wazazi na wanafunzi, walibainisha kuwa elimu iliyokuwa ikitolewa kati ya miaka ya 1980-1990 ilikuwa ikimwezesha mhitimu kuwa na mawazo ya kujitegemea katika ngazi yoyote ya elimu aliyofikia," alisema Zombwe."Wengi wa watu waliohojiwa walisema kwamba elimu ya sasa inamfanya mhitimu ategemee zaidi kuajiriwa na kufanya kazi za ofisi," alisisitiza mchambuzi huyo. Alisema katika utafiti huo. walimu waliikosoa serikali kwa kuanzisha mtaala ambao hauendani na mahitaji ya watu. "Pia wameilalamikia serikali kwa kufanya mabadiliko ya mtaala bila kuwahusisha walimu na wanafunzi, jambo ambalo walidai linawafanya wawe nyuma katika utekelezaji wa mitaala," alisema Zombwe.Alisema wazazi wengi waliohojiwa, walionyesha kutokuwa na uelewa mkubwa kuhusu mitaala na sera ya elimu nchini, jambo ambalo limewafanya wawe nyuma katika kufundisha na kujifunza. Mapendekezo Kufuatia utafiti huo wadau wa elimu walitoa mapendekezo kwamba matumizi ya vitabu vya aina tofauti, hayana tija kwa sababu yanawafanya wanafunzi wajifunze dhana zinazotofautiana wakati wanatarajiwa kufanya mtihani wa aina moja. Alisema pia walitaka kuwe na udhibiti wa ubora wa vitabu, kuwapo kwa nyenzo na vifaa vya kufundishia na walimu kufahamishwa kuhusu sera za elimu |