Wednesday, December 14, 2011

WABUNGE MMECHAGULIWA KUWAWAKILISHA WANANCHI NA KUTATUA KERO ZAO, JE UGUMU WA MAISHA NI KWENU TU?

Nyongeza ya posho za wabunge yaibua mjadala mzito  Send to a friend
Wednesday, 14 December 2011 10:45
0digg
Na Joyce Mmasi
NYONGEZA ya posho za wabunge imekuwa gumzo na kuzua mijadala isiyo na kikomo katika jamii ya Tanzania.
Tofauti na mijadala ya awali ya kupinga ama kuiunga mkono, sasa kinachojadiliwa ni kauli tata za viongozi waandamizi wa bunge juu ya jambo hilo.
Kauli tata ni zile za Spika wa Bunge, Anne Makinda na Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashillilah ambazo zimeonekana kutofautiana kana kwamba zimetolewa na watu wasiofanya kazi katika taasisi moja.
Utata huu unatokana na ukweli kuwa viongozi hao wanatoa majibu yanayotofautiana kuhusiana na suala moja.
Viongozi hao ambao wanafanya kazi katika ofisi moja wamezua maswali kufuatia kutoa matamko tofauti kuhusiana na suala moja ambapo wakati mmoja anapinga habari ya kuwapo kwa nyongeza hiyo ya posho kwa wabunge mwingine anaibuka na kueleza kuwa nyongeza inayozungumzwa ipo na imefanywa kwa makubaliano baina ya ofisi, serikali na wabunge wenyewe.
Mparaganyiko huo wa mawazo unatokana na taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari kuhusu kuongezeka kwa posho za wabunge kutoka Sh70,000 hadi 200,000 kutwa hivyo kufanya bajeti ya posho hizo kwa mwaka kufikia Sh28 bilioni.

Kutokana na ongezeko hilo, kila mbunge atakuwa akilipwa Sh 80,000 kama posho ya kujikimu (per diem) anapokuwa nje ya jimbo lake, posho ya vikao,  Sh200,000 na mafuta ya gari Sh50,000 kila siku, sawa na Sh330,000 kwa siku huku mshahara jumla kabla ya makato ukielezwa kuwa ni sh 2.3 milioni.

Kauli tata za viongozi
Kwa mujibu wa Dk Kashillilah, mapendekezo ya kutaka posho za wabunge zipande, yaliibuka katika mkutano wa wabunge mjini Dodoma Novemba 8 mwaka huu, lakini hadi wakati anatoa tamko anasema yalikuwa hayajaanza kutekelezwa.
Siku kadhaa baadaye, Spika wa Bunge, Anne Makinda akaibika na kauli inayoonekana kupingana na ile ya katibu wake na akakiri kuwa ni kweli posho za wabunge zilikuwa zimeongezeka kutoka Sh 70,000 hadi Sh 200,000 kwa kikao na zilikuwa zimeanza kutumika.
Mbunge huyu alikuwa anapata Sh 70000 kwa hiyo tumemwongezea Sh130,000 na hupati 'unless' (isipokuwa) umefanya kazi ya Bunge na umesaini asubuhi na jioni hujafanya hivyo hupati hizo hela, anasema Makinda katika kauli inayokinzana na ile ya Dk Kashillilah ambaye wanafanya kazi katika ofisi moja.
Utata huu wa kauli toka kwa watendaji wakuu wa taasisi hii nyeti ya Bunge ndio ulioongeza kasi ya mjadala wa nyongeza za posho za wabunge. Waliopata fursa ya kuchangia wanahoji sababu ya kukinzana kwa majibu katika suala nyeti kama hilo.
Wengine wanaenda mbali zaidi kwa kusema utata huo unaonyesha ni jinsi gani suala hilo lilivyo tata na ambalo huenda likawa halikuwa na ‘baraka’ hata na baadhi ya watendaji hao na kwamba utekelezaji wake huenda umepelekwa haraka haraka bila kupata baraka za wahusika.
Utata huo unazungumziwaje?
Mbunge wa Kigoma Kusini David Kafulila (NCCR- Mageuzi), anasema suala la kupishana kauli kwa viongozi wawili wa taasisi moja, ni udhaifu mkubwa kwa taasisi hiyo. 
Suala la posho linatakiwa litazamwe upya katika mihimili yote ya dola, panapokuwa hakuna kanuni ya kuweka uwiano miongoni mwa mihimili hii, kunasababisha manung’uniko na malalamiko kwa wananchi, inatakiwa itazamwe upya,  hili suala la posho lipatiwe ufumbuzi kabisa,” anasema Kafulila. 
Kwa upande wake, Profesa Ruth Meena ambaye ni mwanaharakati wa masuala ya kijamii na msomi aliyebobea anasema ni jambo la kusikitisha kuwa viongozi wa bunge wanapishana kauli juu ya suala hilo la posho.
Inasikitisha sana hawa wawakilishi wetu kujiongezea posho wakisema kuwa gharama za maisha zimepanda, kwenye hali kama hii ya sasa hakuna njia yeyote utakayo weza kutumia kuhalalisha ongezeka kama hili,  anasema.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia anasema mfumo mzima wa utoaji wa posho nchini ni wa kifisadi.
Mbatia anasema ipo haja ya kuutizama upya mfumo huo ambao umeacha pengo kubwa kati ya mwenye nacho na asiyekua nacho.
Jambo hili halitendi haki kwa watanzania, linaweka tofauti kubwa kati ya wenye nacho na wasiokuwa nacho hii si sawa, mfumo mzima wa utoaji posho unatakiwa kutizamwa upya, anasema.
Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba Mkoani Kagera, Dk Methodius Kilani anasema ongezeko hilo la posho limekuja ghafla na kwamba kiwango hicho ni kikubwa na hakiendani na hali halisi ya uchumi wa nchi.
Watanzania wengi wanalalamika maisha magumu sasa Wabunge wanapoongezewa posho kwa kiwango kinachofikia Sh 200,000 watambue kwamba kuna wananchi wanaohitaji msaada, hizo nyongeza za posho zingeweza kuwasaidia kwa namna moja ama nyingine ambapo ongezeko la posho hizo zingeweza kuwasaidia anasema Askofu Kilaini.
Kwa upande wake, Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaji Alhad Mussa Salum  anasema kwamba haoni tatizo posho za wabunge kuongezeka na kwamba  kutokana na majukumu yao mazito ya kuwahudumia wananchi.
Ni jambo jema lakini wabunge watambue kwamba wananchi waliowachagua wana matatizo mengi ya kiuchumi sasa wanaposikia wabunge wameongezewa posho lazima nao watahoji lakini kinachotakiwa ni kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kutatua matatizo ya wananchi wao”anasema Sheikh Alhad.
Lakini, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema)  anasema ongezeko hilo ni batili kwa sababu halina baraka za Rais Jakaya Kikwete.
Spika wa Bunge anajua kwamba posho zote hulipwa baada ya rais kuidhinisha. Anasema ongezeko la posho halikuidhinishwa kwakuwa uthibitisho wa kuidhinisha ni Masharti Mapya ya kazi kwa wabunge ambayo hayajatolewa na Ofisi ya Rais.
Anasema kitendo cha kuanza kulipa posho mpya bila masharti mapya ya kazi za wabunge ni kukiuka sheria ya utawala wa Bunge kifungu cha 19 na kwamba kutokana na hali hiyo, Tume ya Bunge inapaswa kuwajibika kwa kutumia vibaya mamlaka yake.
Anapendekeza posho mpya zifutwe na zilizolipwa zirejeshwe mara moja kwani zimelipwa kinyume na sheria. “Spika anapaswa kuheshimu sheria ambazo Bunge limepitisha na kwenda kinyume na sheria kwa makusudi ni kosa la kuvuliwa uspika, anaeleza.
Mbunge wa Jimbo la Ubungo,  John Mnyika (Chadema) anasema ongezeko hilo linatakiwa kusitishwa kwa kuwa mchakato wake umefanyika kinyume na taratibu.
Anasema kauli ya Spika Makinda kwamba nyongeza hiyo inatokana na kupanda kwa gharama za maisha mkoani Dodoma haina ukweli, wala mantiki na ina mwelekeo wa upendeleo

SERIKALI IKITAMBUA MCHANGO WA WALIMU,ITAWAJALI HATA KWA MASLAHI

CWT: Hakuna mwalimu aliyelipwa mpaka sasa  Send to a friend
Tuesday, 13 December 2011 19:45
0digg
Rais wa CWT, Gratian Mukoba
Pamela Chilongola
CHAMA Cha Walimu Tanzania (CWT), kimesema hakuna mwalimu yoyote aliyelipwa malimbikizo ya stahili mbalimbali na mishahara kama ilivyotangazwa  na baadhi ya vyombo vya habari.

Juzi Naibu waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi,Philip Mulugo alipozungumza na gazeti moja la kila siku siyo Mwananchi, alisema Novemba, mwaka huu, serikali ilikuwa imelipa Sh29 bilioni, kati ya Sh49.6 bilioni zinazodaiwa na walimu. Lakini jana Rais wa CWT, Gratian Mukoba alisema: “Hadi leo (jana) hakuna mwalimu yeyote ambaye alikuwa amelipwa malimbikizo ya stahili zao au mishahara yao.”

Alisema tangu Juni mwaka huu, CWT na Serikali wamekuwa na vikao kadhaa kuhusu madai hayo.

“Sisi tunadai mishahara yetu  tuliyodhulumiwa, tunakandamizwa sisi walimu tunashangaa badala ya kutulipa hela tunazodai, tunashangaa kusikia wabunge wameongezewa posho na vitu vingine ambavyo vimefikia Sh330,000 milioni.“Msimamo wetu wa kugoma Januari mwakani uko palepale, hivyo hakuna mtu ambaye atatulaumu,  imeshapita miezi mine, serikali haijafanya kitu chochote kuhusu sisi walimu,”alisema Mukoba.

Alisema madai hayo yanawahusu walimu zaidi ya 3,000 ambao hawajalipwa kuanzia mwaka 2008.Mukoba alisema kero nyingine ambayo itawafanya wagome ni walimu walioshushwa vyeo mwaka 2007 na kutopandishwa mpaka sasa.“Na hii imetokana na waraka kandamizi uliotolewa na serikali mwaka 2007 ambao uliwashusha vyeo baada ya kujiendeleza kielimu.

“Serikali ilikubali kuufuta waraka huo baada ya kuridhika kwamba ulikuwa unawakandamiza walimu, lakini hadi sasa unaendelea kutumika, haujafutwa,” alisema Mukoba.   
Alisema kuna walimu ambao wanapata mishahara inayolingana na kwamba haijarekebishwa. “Utakuta mwalimu anaanza kazi anakuwa sawa na yule mwalimu aliyeanza muda mrefu.“Utakuta mwalimu amepanda daraja, lakini mshahara wake haujarekebishwa huku akiendela kupokea mshahara wa zamani,”alisema Mukoba

NDANI YA CUF KWAFUKUTA, USHIKIANO WAO NA CCM BUNGENI NDIO CHANZO

Vita ya Seif, Hamad Rashid yavuta kasi  Send to a friend
Tuesday, 13 December 2011 20:39
0digg
Maalim Seif Shariff Hamad
KAMATI YA MAADILI YAINGILIA KATI, KUWASHUGHULIKIA WANAOKIUKA TARATIBU
Geofrey Nyang’oro
CHAMA Cha Wananchi (CUF), kimetoa tamko kuhusu vurugu zilizofanywa na wafuasi wake katika mikutano ya mbunge Wawi, Hamad Rashid Mohamed, huku kikipanga kumuita mbunge huyo mbele ya Kamati ya Maadili ili ajibu tuhuma za kukiuka taratibu za chama.Desemba 11 na 12 mwaka huu, wanachama wa CUF wamekuwa wakipambana kwa kutumia silaha za jadi yakiwamo mapanga katika mikutano iliyoitishwa na Hamad Rashid kwenye matawi ya chama hicho, Kata ya Manzese, huku tukio la juzi katika tawi la Chechinya, likisababisha umwagaji damu.

Jana akizungumzia vurugu hizo makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam,  Naibu katibu Mkuu wa CUF Bara, Julius Mtatiro alisema kitendo kilichofanywa na mbunge huyo ni kinyume na taratibu za chama.

Mtatiro alisema  Hamad Rashid  ameungana na baadhi ya wajumbe wa Baraza Kuu la chama hicho kuendesha mikutano hiyo kinyume na taratibu.

“Ifahamike kuwa haya yanayoendelea si sahihi. Chama chetu kina namna ya kipekee ya kutafuta uongozi. Hii ya Hamad Rashid  ni zaidi ya kutafuta ukatibu mkuu, ni njia ya kuua chama. Hatuwezi kutafuta ukatibu mkuu kwa njia ya umafia,”alisema Mtatiro.

Mtatiro alisema kutokana na vitendo hivyo, CUF inatarajia kumchukulia hatua mbunge huyo kwa mujibu wa taratibu zake. Katika hatua za awali, mbunge huyo pamoja na wenzake wanaomuunga mkono wataitwa kwenye Kamati ya Maadili na Nidhamu  wakati wowote kuanzaia sasa kwa ajili ya kuhojiwa.

Alisema baada ya mbunge huyo na washirika wake  kuhojiwa, taarifa zitapelekwa kwenye Halmashauri Kuu ya chama ambayo itaamua hatua za chukua  dhidi yao.
“Siwezi kusema ni hatua gani zitachukuliwa, sababu katika hili mimi sijui na wala Seif Shariff Hamad hajui, ila chama ndio kitakachotoa maamuzi kwa mujibu wa katiba,”alisema Mtatiro.

Alisema kwa mujibu wa taratibu za CUF, mikutano inayofanywa na Hamad siyo halali . Akasisitiza, “huwezi kufanya mikutano bila  kuwajulisha makao makuu ya chama, ofisi za mikoa na wilaya unakokwenda kufanya mkutano ua ziara”.

“Mimi Mtatiro pamoja na nafasi yangu siwezi kuondoka hapa na kwenda Wawi Pemba kufanya mikutano bila ya makao makuu ya CUF kujua na pia ofisi za mikoa na wilaya katika eneo husika. Ni lazima kutoa taarifa,”alisisitiza Mtatiro huku akitolea mfano ziara inayofanywa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif

“Ni kweli anataka ukatibu, kumekuwa na vitisho, lengo nini ni kuua chama! Lakini, Hamadi fedha anapata wapi? Uchaguzi tunafanya 2014, kwanini iwe sasa?,”alihoji Mtatiro.

Hamad Rashid akana
Gazeti hili lilipomtafuta Hamad Rashid kuzungumzia hatua hiyo ya chama chake, alisema "Mtatiro aeleze kwa nini alituma vijana kwenda kuvuruga mkutano wangu juzi badala ya kuleta bla bla."

Alisema awali mkutano wake ulitawaliwa na amani na alipokewa na viongozi wa chama katika tawi hilo na kupelekwa sehemu ya mkutano bila tatizo.

“Aulizwa kama ni haki kwa walinzi kuvamia mkutano wa wananchi, wakiwa na mapanga na sime kwa ajili ya kufanya vurugu ,“alisema.

Mbunge huyo alisisitiza kwamba  hajafanya kosa kwa kuamua kufanya ziara na mikutano ya hadhara bila kutoa taarifa kwa uongozi wa chama na kuongeza,   "Kama viongozi hao wa makao makuu wanaona taratibu zimevunjwa, walistahili kuniandikia barua ya kuniita na kunihoji. Sio kutuma vijana wa Blue guard  kwenda kuzuia mkutano."
Vurugu za juzi
Mtatiro alimtuhumu Mbunge huyo kuwa aliandaa vurugu kwa kukodi vijana zaidi ya 100, kutoka katika eneo la Nakos ambao ni wafuasi na wapenzi wa CCM.

Alisema vijana hao walipewa kazi ya kushambulia hata kwa kuua endapo wangewaona walinzi wa chama hicho maarufu blue guard.
Kuhusu walinzi kufika katika eneo hilo, Mtatiro alisema walikuwa wakitekeleza majukumu yao ya kila siku ya kufuatilia na kujua kila kinachoendelea katika chama hicho na pia moja ya kazi yao ni kuhoji jambo lolote linalofanywa kinyume na taratibu za chama.

“Hawa walinzi wa CUF walifika katika eneo hilo baada ya kusikia kuna mkutano unaofanyika kinyume na utaratibu wa chama. Hawa kazi yao ni kuhoji wahusika na kukusanya taarifa za kwanini watu wamekiuka taratibu kisha  kuziwasilisha kwenye ofisi za chama kwa ajili ya hatua zaidi,”alisema Mtatiro.

Alisema walipofika na kuanza kazi, ghafla walivamiwa na kundi la vijana zaidi ya 100 wakiwa na silaha za mapanga na marungu na kuanza kuwashambulia na kusababisha walinzi wanne na baadhi ya wanachama kujeruhiwa.
Ushuda wa majeruhi
Katika hatua nyingine, walinzi wawili walionusurika kifo katika mapambano hayo ya juzi;  Abdallah Kassim na Hamis Idd wakiwa na majeraha ya mapanga mmoja kichwani na mwingine  shingoni, walifika kwenye mkutano huo wa Mtatiro na waandishi wa habari na kueleza kilichotokea juzi.

Akizungumzia tukio hilo, Kassim ambaye alikuwa ameshikilia RB yenye namba MAG/RB/22150/2011 aliyoifungua katika kituo cha polisi Magomeni,  alisema ni Mungu tu ndiye aliyemuokoa.

“Sisi tulisikia kuna mkutano unafanyika kinyume na utaratibu wa chama eneo la Chechnya , tulikuwa walinzi 8, tulichukua gari na kwenda eneo la tukio. Tulipofika wenzetu waliingia ndani kwa lengo la kutaka kujua kinachoendelea ndipo tulipovamiwa,”alisema Kassim.

Alifafanua kwamba, kundi la vijana wakiwa na mapanga, Sime na marungu walianza kwa kutaka kutoa upepo gari walilokwenda nalo.

Kassim aliyekatwa panga shingoni, alisema wakati akifanyiwa unyama huo nyuma yake kulikuwa na kijana aliyetaka kumkata na panga kichwani lakiin mlinzi mwenzake akadaka mkono wa kijana huyo na kumuokoa.
“Panga hilo lingenikata sijui kama ningekuwa hai mimi, yaani ni Mungu tu alininusuru na kifo, ” alisimulia  Kassim kuhu akiwa na jereha  shingoni na kueleza kuwa anakabilia pia na maamivu mbavuni.
Naye Hamiss Idd aliliambia Mwananchi kuwa, tukio hilo na la hatari ambalo kamwe hakulitegemea na tayari ameshonwa nyuzi nne.

Alisema vijana hao waliowakata mapanga pia waliwapora  vitu vyote, walivyokuwa navyo pamoja na simu nane na kwamba yeye binafsi aliporwa  fedha tasilimi Sh 35,000.