Wednesday, December 14, 2011

NDANI YA CUF KWAFUKUTA, USHIKIANO WAO NA CCM BUNGENI NDIO CHANZO

Vita ya Seif, Hamad Rashid yavuta kasi  Send to a friend
Tuesday, 13 December 2011 20:39
0digg
Maalim Seif Shariff Hamad
KAMATI YA MAADILI YAINGILIA KATI, KUWASHUGHULIKIA WANAOKIUKA TARATIBU
Geofrey Nyang’oro
CHAMA Cha Wananchi (CUF), kimetoa tamko kuhusu vurugu zilizofanywa na wafuasi wake katika mikutano ya mbunge Wawi, Hamad Rashid Mohamed, huku kikipanga kumuita mbunge huyo mbele ya Kamati ya Maadili ili ajibu tuhuma za kukiuka taratibu za chama.Desemba 11 na 12 mwaka huu, wanachama wa CUF wamekuwa wakipambana kwa kutumia silaha za jadi yakiwamo mapanga katika mikutano iliyoitishwa na Hamad Rashid kwenye matawi ya chama hicho, Kata ya Manzese, huku tukio la juzi katika tawi la Chechinya, likisababisha umwagaji damu.

Jana akizungumzia vurugu hizo makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam,  Naibu katibu Mkuu wa CUF Bara, Julius Mtatiro alisema kitendo kilichofanywa na mbunge huyo ni kinyume na taratibu za chama.

Mtatiro alisema  Hamad Rashid  ameungana na baadhi ya wajumbe wa Baraza Kuu la chama hicho kuendesha mikutano hiyo kinyume na taratibu.

“Ifahamike kuwa haya yanayoendelea si sahihi. Chama chetu kina namna ya kipekee ya kutafuta uongozi. Hii ya Hamad Rashid  ni zaidi ya kutafuta ukatibu mkuu, ni njia ya kuua chama. Hatuwezi kutafuta ukatibu mkuu kwa njia ya umafia,”alisema Mtatiro.

Mtatiro alisema kutokana na vitendo hivyo, CUF inatarajia kumchukulia hatua mbunge huyo kwa mujibu wa taratibu zake. Katika hatua za awali, mbunge huyo pamoja na wenzake wanaomuunga mkono wataitwa kwenye Kamati ya Maadili na Nidhamu  wakati wowote kuanzaia sasa kwa ajili ya kuhojiwa.

Alisema baada ya mbunge huyo na washirika wake  kuhojiwa, taarifa zitapelekwa kwenye Halmashauri Kuu ya chama ambayo itaamua hatua za chukua  dhidi yao.
“Siwezi kusema ni hatua gani zitachukuliwa, sababu katika hili mimi sijui na wala Seif Shariff Hamad hajui, ila chama ndio kitakachotoa maamuzi kwa mujibu wa katiba,”alisema Mtatiro.

Alisema kwa mujibu wa taratibu za CUF, mikutano inayofanywa na Hamad siyo halali . Akasisitiza, “huwezi kufanya mikutano bila  kuwajulisha makao makuu ya chama, ofisi za mikoa na wilaya unakokwenda kufanya mkutano ua ziara”.

“Mimi Mtatiro pamoja na nafasi yangu siwezi kuondoka hapa na kwenda Wawi Pemba kufanya mikutano bila ya makao makuu ya CUF kujua na pia ofisi za mikoa na wilaya katika eneo husika. Ni lazima kutoa taarifa,”alisisitiza Mtatiro huku akitolea mfano ziara inayofanywa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif

“Ni kweli anataka ukatibu, kumekuwa na vitisho, lengo nini ni kuua chama! Lakini, Hamadi fedha anapata wapi? Uchaguzi tunafanya 2014, kwanini iwe sasa?,”alihoji Mtatiro.

Hamad Rashid akana
Gazeti hili lilipomtafuta Hamad Rashid kuzungumzia hatua hiyo ya chama chake, alisema "Mtatiro aeleze kwa nini alituma vijana kwenda kuvuruga mkutano wangu juzi badala ya kuleta bla bla."

Alisema awali mkutano wake ulitawaliwa na amani na alipokewa na viongozi wa chama katika tawi hilo na kupelekwa sehemu ya mkutano bila tatizo.

“Aulizwa kama ni haki kwa walinzi kuvamia mkutano wa wananchi, wakiwa na mapanga na sime kwa ajili ya kufanya vurugu ,“alisema.

Mbunge huyo alisisitiza kwamba  hajafanya kosa kwa kuamua kufanya ziara na mikutano ya hadhara bila kutoa taarifa kwa uongozi wa chama na kuongeza,   "Kama viongozi hao wa makao makuu wanaona taratibu zimevunjwa, walistahili kuniandikia barua ya kuniita na kunihoji. Sio kutuma vijana wa Blue guard  kwenda kuzuia mkutano."
Vurugu za juzi
Mtatiro alimtuhumu Mbunge huyo kuwa aliandaa vurugu kwa kukodi vijana zaidi ya 100, kutoka katika eneo la Nakos ambao ni wafuasi na wapenzi wa CCM.

Alisema vijana hao walipewa kazi ya kushambulia hata kwa kuua endapo wangewaona walinzi wa chama hicho maarufu blue guard.
Kuhusu walinzi kufika katika eneo hilo, Mtatiro alisema walikuwa wakitekeleza majukumu yao ya kila siku ya kufuatilia na kujua kila kinachoendelea katika chama hicho na pia moja ya kazi yao ni kuhoji jambo lolote linalofanywa kinyume na taratibu za chama.

“Hawa walinzi wa CUF walifika katika eneo hilo baada ya kusikia kuna mkutano unaofanyika kinyume na utaratibu wa chama. Hawa kazi yao ni kuhoji wahusika na kukusanya taarifa za kwanini watu wamekiuka taratibu kisha  kuziwasilisha kwenye ofisi za chama kwa ajili ya hatua zaidi,”alisema Mtatiro.

Alisema walipofika na kuanza kazi, ghafla walivamiwa na kundi la vijana zaidi ya 100 wakiwa na silaha za mapanga na marungu na kuanza kuwashambulia na kusababisha walinzi wanne na baadhi ya wanachama kujeruhiwa.
Ushuda wa majeruhi
Katika hatua nyingine, walinzi wawili walionusurika kifo katika mapambano hayo ya juzi;  Abdallah Kassim na Hamis Idd wakiwa na majeraha ya mapanga mmoja kichwani na mwingine  shingoni, walifika kwenye mkutano huo wa Mtatiro na waandishi wa habari na kueleza kilichotokea juzi.

Akizungumzia tukio hilo, Kassim ambaye alikuwa ameshikilia RB yenye namba MAG/RB/22150/2011 aliyoifungua katika kituo cha polisi Magomeni,  alisema ni Mungu tu ndiye aliyemuokoa.

“Sisi tulisikia kuna mkutano unafanyika kinyume na utaratibu wa chama eneo la Chechnya , tulikuwa walinzi 8, tulichukua gari na kwenda eneo la tukio. Tulipofika wenzetu waliingia ndani kwa lengo la kutaka kujua kinachoendelea ndipo tulipovamiwa,”alisema Kassim.

Alifafanua kwamba, kundi la vijana wakiwa na mapanga, Sime na marungu walianza kwa kutaka kutoa upepo gari walilokwenda nalo.

Kassim aliyekatwa panga shingoni, alisema wakati akifanyiwa unyama huo nyuma yake kulikuwa na kijana aliyetaka kumkata na panga kichwani lakiin mlinzi mwenzake akadaka mkono wa kijana huyo na kumuokoa.
“Panga hilo lingenikata sijui kama ningekuwa hai mimi, yaani ni Mungu tu alininusuru na kifo, ” alisimulia  Kassim kuhu akiwa na jereha  shingoni na kueleza kuwa anakabilia pia na maamivu mbavuni.
Naye Hamiss Idd aliliambia Mwananchi kuwa, tukio hilo na la hatari ambalo kamwe hakulitegemea na tayari ameshonwa nyuzi nne.

Alisema vijana hao waliowakata mapanga pia waliwapora  vitu vyote, walivyokuwa navyo pamoja na simu nane na kwamba yeye binafsi aliporwa  fedha tasilimi Sh 35,000.

No comments:

Post a Comment