Vita ya ufisadi yageukia vyama vya siasa | Send to a friend |
Tuesday, 19 April 2011 08:13 |
0diggsdigg Ramadhan SemtawaVYAMA sita vya siasa vyenye wawakilishi bungeni, vinadaiwa kuwa vimeshindwa kuwasilisha taarifa za hesabu kuhusu matumizi ya ruzuku ya jumla ya Sh17.14bilioni kwa mujibu wa sheria.Vyama hivyo ambavyo vinapata ruzuku inayotolewa na Serikali ni pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Tanzania Labour (TLP), NCCR-Mageuzi na UDP. Tuhuma hizo zimo kwenye Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), inayoishia Juni 30, 2010. CAG ametoa ripoti hiyo baada ya sheria, kwa mara ya kwanza kumpa mamlaka ya kuvikagua vyama vya siasa ambavyo mahesabu yao, yanapaswa kuwasilishwa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania. "Taarifa za fedha kwa malipo ya ruzuku ya Sh17,146,819,904 kwa vyama vya siasa mbalimbali hazikuwasilishwa na vyama husika katika Ofisi ya Msajili," ilisema Ripoti ya CAG katika fungu la 27 kuhusu Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na matumizi ya ruzuku. Takwimu kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa zinaonyesha kuwa CCM kinapata ruzuku ya asilimia 70, CUF asilimia 20, Chadema asilimia nane na NCCR-Mageuzi, UDP na TLP vinagawana asilimia mbili. Katika mahesabu ya kawaida, kati ya fedha hizo Sh 17.14 bilioni, CCM itakuwa imepata mgawo wa Sh12bilioni, CUF Sh 3.43bilioni, Chadema Sh1.37bilioni na vyama hivyo vitatu kwa asilimia mbili yao vikipata Sh343milioni. Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa alipoulizwa na gazeti dada la The Citizen kwa simu alisema asingeweza kuzungumzia jambo hilo nyeti kwa mawasiliano ya simu kwani anahitaji kukaa na kulifanyia kazi kwa kina. Hata hivyo, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ludovic Utouh katika ripoti hiyo alisema kitendo hicho ni kinyume cha kifungu 14 (1) na (3) cha Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992. Sehemu ya kifungu hicho inasema, "Chama chochote cha siasa ambacho kina usajili wa kudumu, kinapaswa kutunza hesabu zake vizuri za ruzuku na kuwasilisha kwa Msajili." Kifungu hicho kinaendelea: "Kwa kutumia taarifa ya mwaka ya ukaguzi wa hesabu uliofanywa na mkaguzi anayetambulika kwa mujibu wa Sheria ya Ukaguzi wa Hesabu, huku ikiwa na tamko la mali zote zinazomilikiwa na chama hicho." Utouh alisema pia kwamba Sh56.9milioni zilitumika na msajili huyo wakati hazikuhusiana na shughuli za vyama vya siasa. "Jumla ya Sh56,180.44milioni zilitumika na Msajili wa Vyama vya Siasa wakati hazikuhusiana na shughuli za vyama vya siasa," alisema Utouh katika taarifa hiyo. Mbali na tuhuma hizo, Utouh alisema kwamba kiasi cha Sh272.8milioni zilitumika kulipa deni la miaka ya nyuma la Bodi ya Udhamini ya chama cha UDP bila kuonyeshwa katika taarifa za fedha na kusema: "Malipo haya yanaathiri utendaji wa ofisi kwa mwaka wa sasa wa fedha." UDP kinaongozwa na John Cheyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC). Alipoulizwa kuhusu fedha hizo, Cheyo alisema hajaisoma vyema ripoti hiyo na kuongeza kwamba atakuwa kwenye nafasi nzuri kuzungumzia hilo baada ya kuipitia kwa kina. "Kwa sasa hivi itakuwa ni vigumu kuzungumzia ripoti hiyo wakati sijaisoma vizuri. Nitakuwa siko sahihi kama nitazungumza bila kuisoma. Nipe muda nisome kisha nitaweza kuizungumza," alisema. |