Wednesday, April 13, 2011

KATIBU MPYA WA CCM BAADA YA KUVUA GAMBA LA KALE

Mrithi wa Makamba aingia na moto  Send to a friend
Tuesday, 12 April 2011 22:20
0diggsdigg
Katibu Mkuu mpya wa CCM Wilson Mukama
Waandishi Wetu, Dar na Dodoma
UPEPO wa kisiasa ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), unazidi kuvuma kwa kasi baada ya Katibu Mkuu mpya wa chama hicho, Wilson Mukama, kutangaza kiama kwa mafisadi akitaka wajiuzulu mapema, huku Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa Chama hicho, Makongoro Nyerere akitajwa kuchochea maamuzi magumu dhidi ya genge hilo.Kauli hizo nzito za vigogo hao dhidi ya genge la mafisadi ambalo lina nguvu za fedha ndani na nje ya chama hicho tawala, ni sehemu ya mpango mkakati wa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, wa kukivua magamba.Mukama ambaye ndiye Mtendaji Mkuu wa chama hicho aliyetangazwa mjini Dodoma usiku wa kuamkia jana, alisema ili chama hicho kiweze kurudisha heshima yake kinatakiwa kuwa na watu safi wasiotiliwa mashaka kabisa katika jamii. Akizungumza na Mwananchi ofisini kwake muda mfupi baada ya kumaliza kikao na watendaji wa mikoa wa chama hicho, Katibu huyo alisema hana jipya atakalopeleka CCM isipokuwa yeye atasimamia weledi na misingi iliyokuwapo tangu kuanzishwa kwa CCM.
“CCM inatakiwa kujengwa upya kabisa na ili hayo yaweze kufanikiwa, kuna kila sababu za kuwa na watu safi, hivyo mimi nawataka ndugu zangu wasimame katika misingi ya zamani tuliyokuwa nayo katika chama chetu,” alisema Mukama na kuongeza:
“Nawataka wote wenye tuhuma za rushwa na ufisadi ndani ya chama waanze kujiuzulu mapema ili kulinda heshima yao, kwani tunaingia kujenga chama sio kukibomoa.”
Katibu Mkuu huyo ambaye ana kibarua kigumu cha kusafisha chama na kukirejesha katika misingi ya waasisi wake  tangu enzi TANU na CCM ya mwaka 1977, alisema mwelekeo wa CCM pamoja na sera zake bado unakubalika kwa wananchi na kuongeza: "Kinachotakiwa sasa ni kuwa na usimamizi na maamuzi magumu kwa kila mtu atakayekabidhiwa dhamana hiyo".
Akizungumzia juu ya chama kujengwa upya alisema: "Ili tuweze kufanikiwa katika hilo mimi nitasimamia maamuzi ya Kamati Kuu ya CCM ya kukirudisha chama kwa wanachama ngazi ya chini ili wao ndio wakafanye maamuzi.”
Mukama ambaye alikuwa akizungumza kwa kujiamini alisema atasimamia kikamilifu itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea, kwa kuwa ndio sera kubwa ya CCM tangu kuanzishwa kwake.
Jambo lingine alilosisitiza kiongozi huyo ni pamoja na kukiongoza chama katika kupata ushindi ambao hautakuwa ukitiliwa mashaka na watu wengine.“Jambo kubwa na la msingi hapa ni kukiongoza chama katika kufikia malengo makubwa ya kupata ushindi usiokuwa na manung’uniko, kwani mbinu za kivita hupatikana katika medani sio uwanja wa vita,” alitamba Mukama. Hata hivyo, alisifia hatua ambayo imechukuliwa na chama ambayo imesaidia kukijenga hadi sasa.
Aliyataja mafanikio ya hatua hiyo kuwa ni pamoja na kuwa viti vingi bungeni, kwani zaidi ya asilimia 78 ya wabunge wanatoka CCM.

Abeza nguvu ya upinzani
Akizungumzia nguvu za upinzani, Mukama alibeza na kusema hilo haliwezi kumsumbua yeye wala kumfanya asilale usingizi, kwani anatambua ni wapi panatakiwa kusimamiwa na ni wapi panatakiwa kutolewa maelekezo yake.
“Kwenye siasa hata siku moja ni kubwa sana huwezi kuidharau. Leo tutazungumzia miaka minne ili tuingie katika Uchaguzi Mkuu mwingine, hivyo bado kuna muda mzuri na wa kutosha kufanya maandalizi, ndio maana siwezi kutaja moja kwa moja chama kinachonipa tabu bali kitajulikana mbele ya safari,” alitamba Mukama

Ofisini siku ya kwanza
Kutwa nzima jana, Mukama akiwa na wasaidizi wake John Chiligati (Bara), Vuai Alli Vuai (Zanzibar) pamoja na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, walifanya vikao na makatibu wa mikoa na watumishi wa CCM Makao Makuu.Awali, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Kikwete, alizungumza na watumishi makao makuu na baadhi ya makada wa chama kwa lengo la kuitambulisha Sekretarieti mpya na kuweka mikakati.

Makamba ataka aachwe
Kwa upande wake Katibu Mkuu aliyeachia ngazi, Yusuph Makamba, alisema huu ni wakati wake wa kupumzika kwani amechoka.Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana kuhusu uamuzi mgumu wa kujiuzulu aliouchukua mjini Dodoma hivi karibuni alisema, "Naomba mniache nipumzike... Nimechoka."
Alifafanua kwamba ametumikia nchi kwa zaidi ya miaka 50, hivyo huu ni wakati wake kupumzika na watu wengine kufanya kazi na yeye aachwe apumzike.
"Nimetumikia nchi hii kwa miaka mingi, nimekuwa mkuu wa wilaya, mkoa na baadaye chama, sasa ni wakati wangu wa kupumzika kwani kazi niliyofanya ni kubwa," alisisitiza.
Katibu Mkuu huyo mstaafu aliyetuhumiwa kukigawa chama, alisema kama ni chama kimepata uongozi mpya ambao anaamini utaweza kusimamia ajenda zake kwa ufanisi.
Makongoro Nyerere amchochea JK
Mtoto wa Baba wa Taifa ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Makongoro Nyerere, amemshauri Mwenyekiti wake Rais Kikwete, kuwabwaga wote wanaotuhumiwa kwa ufisadi hata kama ni maswahiba wake kisiasa.
Habari kutoka ndani ya kikao cha Nec, zilidokeza gazeti hili kwamba Makongoro alimweleza Rais Kikwete wakati wa kikao kuwa hana budi kuchukua uamuzi utakaowaumiza marafiki zake, ili kukinusuru chama.
“Vitabu vitakatifu vinatueleza kuwa awali Mungu alikuwa akishirikiana kwa karibu na shetani, lakini shetani alipoanza ushetani wake, Mungu akamtimua na kumtupa uwanjani. Mungu hakai na shetani,” mpasha habari wetu alimnukuu Makongoro.
Makongoro anadaiwa kumweleza Rais Kikwete kwamba, watu wa Dar es Salaam walipokwenda kuhiji katika kaburi la baba yake, walipata jibu la kuwa Kikwete ndiye anayefaa, hivyo asivurugwe na watu wachache.
Makongoro alimtahadharisha rais kuwa kama atachukua uamuzi wa kuilipa Kampuni ya Dowans Sh94 bilioni, hakuna Mtanzania atakayemwelewa.
Katika hatua nyingine, uamuzi wa kuvunjwa kwa Sekretarieti na Kamati Kuu ya CCM, kumechochea wanachama kudai mabadiliko yafanyike haraka katika ngazi ya mikoa.
Mbunge wa Kinondoni (CCM), Iddi Azzan, alisema mabadiliko yaliyofanywa ndani ya chama hicho ni mazuri.
Hata hivyo, Azzan alisema mabadiliko hayo yanatakiwa kufanyika katika ngazi za mikoa na wilaya ambako alidai kuwa kumeoza.
Aliitaka Sekretarieti ya Mkoa wa Dar es Salaam kujiuzulu kama walivyofanya wa Sekretarieti ya Taifa.
Sekretarieti ya CCM, Mkoa wa Dar es Salaam inaundwa na Katibu wa CCM Mkoa, Kilumbe Ng'enda, Katibu Mwenezi, Juma Simba, Katibu wa Uchumi, Abbas Tarimba, Katibu wa Wazazi, Mustafa Yakub, Katibu wa UWT, Tatu Mariaga na Katibu wa UVCCM, Omar Mwanag’alu.

January  ajiuzuluKamati ya Bunge
Katika tukio lingine, Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa CCM, Januari Makamba, anatakiwa kujiuzulu nafasi yake ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Chiligati, alisema Makamba anatakiwa kupima uzito wa kazi aliyopewa na ile ya Bunge. Anatakiwa kubaki na ubunge kwa sababu sio kazi ya kuwajibika kila siku.
Katika mkutano wake Nec iliamua kuwa watumishi wa chama wanatakiwa kuwapo kila siku kwa ajili ya utendaji na kwamba wanatakiwa kutenganisha viongozi wa Serikali na chama.
Habari hii imeandikwa na Habel Chidawali na Midraj Ibrahim, Dodoma, Ramadhan Semtawa, Dar