Thursday, November 15, 2012

POLISI WASIINGILIWE NA CHAMA DOLA KATIKA UTENDAJI KAZI ZAO


RAIS Jakaya Kikwete juzi aliwaonya wanachama wa CCM akiwataka waache kubweteka kwa kuwategemea askari polisi katika masuala ya kisiasa, kwani kufanya hivyo watakuwa wanajidanganya.

Kikwete alitoa kauli hiyo wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Nane wa CCM uliofanyika kwa siku tatu mfululizo katika Ukumbi wa Kizota mjini Dodoma.

Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, alisema kitendo cha wanaCCM kuishi katika siasa kwa kutegemea Jeshi la Polisi hakipaswi kukubaliwa kwani kimepitwa na wakati.

“Mnaishia kulalamika tu kila siku, eti wanatukana halafu mnaishia kusema ndiyo kawaida yao…au utasikia mtu anasema eti Serikali haipo! Kazi ya Serikali siyo hiyo, hiyo ni kazi ya kisiasa maana hao ndio wenzenu,”alisema Kikwete na kuongeza:

“Sasa mnataka wakisema Serikali ya CCM haijafanya kitu polisi wawafuate, au wakisema Kikwete nchi imemshinda, polisi wakawakamate? Kama wakisema hatujafanya kitu ni kazi yenu kusema kwamba tumefanya kitu, waonyesheni barabara, shule na mambo mengine.”

Licha ya kwamba hakuwataja moja kwa moja, kauli za Rais Kikwete zilikuwa zikielekezwa kwa uogozi wa Chadema ambao kimsingi kinaonekana kuwaumiza vichwa CCM.

Huku akirudia mara kadhaa maneno hayo alisema, “Nataka mfahamu ndugu zangu kuwa tukiishi kwa kutegemea Jeshi la Polisi kufanikisha mambo yetu, tutakwisha na tutakwisha kweli.”

Kikwete aliwatuhumu viongozi wa upinzani kwamba ni waongo na kwamba wakati mwingine wamekuwa wakizusha mambo ambayo hayapo, huku wakijifanya kuwa na ushahidi wa kimaandishi.

Alimtaja Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kwamba kuna wakati aliwahi kuzusha kwamba yeye (Kikwete), na makada kadhaa wa chama hicho wakiwamo Rostam Aziz walikuwa jijini Mwanza usiku, wakati si kweli kwani siku waliyodai alikuwa Nachingwea mkoani Lindi kwenye mikutano ya kampeni za urais.

Katika mazingira hayo, aliwataka wanaCCM kila mahali kujibu hoja za wapinzani kwa kauli na vitendo na wasikubali kuburutwa kwani uongo ukiachwa kwa muda mrefu unageuka kuwa ni ukweli.

Aliwaeleza kuwa ukimya wao katika kujibu hoja za wapinzani ni sumu kwao na kwamba wenzao wameanza kuaminika zaidi yao licha ya kuwa CCM ndio wenye majibu yote.

“Mkijibu kwa hoja wanatulia, sio Polisi. Nakumbuka Mwigulu aliwajibu pale bungeni kuhusu bajeti yao mbadala. Walipoitoa kijana wetu akasimama na kupiga msumari kweli wakachanganyikiwa sasa hizo ndio kazi zinazotakiwa jamani,” alisisitiza Kikwete.

Mbali na hilo aliwaonya kuacha malumbano ya mara kwa mara akieleza kuwa hali hiyo inakibomoa chama.

Alisema baadhi ya wanaCCM wamekuwa wakitumia muda mwingi kukosoana wao kwa wao, huku wakitoa nafasi kwa adui zao.

Mwenyekiti huyo alisema hakuna mtu kutoka nje ya chama anayeweza kukidhoofisha CCM kwa hoja isipokuwa chama hicho kinaumizwa na wanachama wake ambao wamekuwa wakilumbana bila sababu.

Akizungumzia suala la wagombea urais aliwataka wanachama wenye nia kufuata taratibu zote za chama pamoja na kuvumiliana ili ifikapo Mei 2015, mkutano utafanya uamuzi wa nani anasimama kupeperusha bendera ya chama hicho.

“Kwa wale mnaotaka kugombea, andikeni hiyo tarehe tutakuja hapa kuteua, lakini msituvuruge lazima mfuate utaratibu. Utaratibu huo utatangazwa, maana mkianza kupita huko na huko ndiko tunakopata matatizo,” alisema Kikwete.

Kikwete juzi alichaguliwa kwa mara nyingine kuwa Mwenyekiti wa CCM baada ya kupata asilimia 99.92 ya kura zilizopigwa, huku kura mbili zikimkataa. Kadhalika mkutano huo uliwachagua Dk Ali Mohamed Shein kuwa Makamu Mwenyekiti (Tanzania – Zanzibar) na Phillip Mangula kuwa Makamu Mwenyekiti (Tanzania Bara).

VURUGU ZA KIKUNDI CHA UAMSHO Z'BAR, KARUME ATUSHWA ZIGO


RAIS Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Aman Karume juzi usiku alizomewa na baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku wakimwita kwamba ni mmoja wa wanakundi la Uamsho.

Uamsho ni kundi ambalo katika siku za hivi karibuni limekuwa likihusishwa na vurugu ambazo zimekuwa zikitokea Tanzania Visiwani, ambazo zimesababisha watu kadhaa kukamatwa na kufikishwa mahakamani.

Rais Karume alikutana na zahama hiyo wakati akitoa hotuba ya kuwaaga wanaCCM baada ya kumaliza ngwe yake ya utumishi ndani ya chama hicho akiwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar.

Dalili za Rais Karume kuzomewa zilianza baada ya baadhi ya wajumbe kutoka Mkoa wa Mjini Magharibi kuanza kutaja neno ‘Uamsho’ kila alipokuwa akizungumzia matatizo yaliyopo Zanzibar.

Hali ilikuwa mbaya zaidi pale alipokuwa akizungumzia vurugu za kidini ambazo ziliikumba Zanzibar hivi karibuni zikiongozwa na kikundi cha Uamsho.

Karume alisema kuwa kikundi cha Uamsho kina haki ya kutoa maoni yake kuhusu muungano, lakini hakipaswi kufanya vurugu kama ambavyo kimekuwa kikifanya.

Wakati akiendelea kuzungumzia suala hilo, kelele nyingi zilienea katoka kwa wajumbe wa mikoa ya Zanzibar ambao walikuwa wakipaza sauti, “ Uamsho huyo….Uamsho huyo… Uamsho huyo….”

Hali hiyo ilimfanya wakati mwingine kukatiza hotuba yake na kulazimisha kuwatuliza watu hao kwa kusema “CCM oyeee….CCM…..oyeee…Mapinduziii….”
Hata hivyo, baada ya kelele hizo kuendelea Karume alionekana kuhamaki na kuwaambia wajumbe hao kwamba amechoka kusikia akiitwa jina hilo la Uamsho.

“Nimechoka kusikia naitwa jina hilo ati,” alisema Karume na kuongeza:
“Hivi wengine wana vichwa vya samaki kwa nini mnapiga kelele wakati mimi ninapozungumza, si mniache nizungumze mambo ambayo ni muhimu zaidi kwa masilahi ya chama chetu.”

Hata hivyo, licha ya kutafuta namna ya kuwatuliza wanachama hao kwa maneno mengi na historia ya maisha yake tangu alipojiunga na Chama cha ASP mwaka 1970, bado hakukuwa na utulivu na safari hii kelele zilianza kwa pande zote za wajumbe.

Kwa upande wa wajumbe wa Bara, baadhi yao walikuwa wakipiga kelele za kumtaka kumaliza hotuba yake ambayo walisema ilishachukua muda mrefu huku wakisema hakuna cha ajabu alichokuwa akizungumza.

Mara baada ya kumaliza hotuba yake, Karume alihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Redio Deutche Welle ya Ujerumani, na alisisitiza kuwa Uamsho wana haki ya kutoa maoni yao kuhusu muungano, lakini hawaruhusiwi kuvunja sheria.

Aliwataka wanachama wa kikundi hicho kujenga hoja, kwani alisema wengine wana hoja za msingi, lakini wasitumie vitisho.

Karume alistaafu uongozi wa CCM katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti (Tanzania Visiwani) na nafasi yake ilichukuliwa na Rais wa sasa wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein.

Tofauti na utamaduni ambao CCM kimeujenga kwa viongozi wake wakuu, Karume aliendelea kuwa makamu mwenyekiti hata baada ya kustaafu urais wa Zanzibar, hivyo kumlazimisha Dk Shein kusubiri hadi juzi kuchukua nafasi hiyo.

Kwa kawaida, viongozi wa ngazi ya Rais wa Muungano na Zanzibar, baada ya kuondoka katika nafasi zao za uongozi wa nchi, pia huachia madaraka ndani ya chama na kumwachia Rais mpya.