Wednesday, December 19, 2012

NGUO ZA NDANI ZINAZOBANA SANA ZABAINIKA KUVUNJA UNYUMBA KWA KUADIMIKA KWA WATOTO NA HUDUMA ISIYORIDHISHA KITANDANI


“Kwa kawaida mwanamume anayeishi maeneo ya joto anapaswa kuwa makini sana, ili kuhifadhi vizuri manii yake anatakiwa kutumia mavazi yenye kupitisha hewa,” alisema Dk Massawe"

TAFITI za kisayansi zimebaini kuwa nguo za ndani hasa zinazobana kwa wanaume na zile za aina ya nailoni (nylon) zinaathiri uwezo wa mbegu za kiume, hivyo kushindwa kutunga mimba.

Utafiti huo uliofanyika katika nchi za Ufaransa na Uingereza na kuchapishwa katika Gazeti la Daily Mail la Uingereza unabainisha kuwa, wanaume wanaovaa nguo za ndani zinazobana na zile zilizotengezwa kwa malighafi ya nailoni, mbegu zao za kiume (manii) huwa nyepesi na kupoteza uwezo wa kutunga mimba.

Vazi la ndani la wanaume linalojulikana kama boksa na nguo nyingine za ndani za kubana zenye asili ya nailoni, zinakuwa na athari kubwa zaidi hasa zinapovaliwa katika sehemu zenye joto, kama Dar es Salaam.

Kutokana na matokeo hayo, wanasayansi wameonya kuwa wanaume wanapaswa kuchukua tahadhari, hasa kutokana na tafiti nyingi za karibuni kuthibitisha kuongezeka kwa matatizo ya mbegu za kukosa uwezo wa kutunga ujauzito katika nyumba ya uzazi ya mwanamke.
Akizungumzia utafiti huo jana, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi katika Hosipitali ya Taifa Muhimbili, Dk Cyril Massawe, alisema una ukweli kutokana na mbegu za kiume kuwa nje ya mwili wa mwanamume tofauti na mwanamke ambaye kizazi chake kipo ndani.

“Kwa kawaida mwanamume anayeishi maeneo ya joto anapaswa kuwa makini sana, ili kuhifadhi vizuri manii yake anatakiwa kutumia mavazi yenye kupitisha hewa,” alisema Dk Massawe.

Ufaransa na Uingereza
Utafiti uliofanywa Ufaransa umebaini kuwa, upungufu wa nguvu za kiume kwa wanaume wengi ulianza kutokea tangu mwanzoni mwa 1990.

Awali, ilikuwa ikiaminika kuwa kupungua kwa uwezo wa mbegu za kiume kulitokana na sababu kama vile mtindo wa maisha, ulaji na matumizi ya dawa kupindukia na matumizi ya vyakula vyenye kemikali nyingi, lakini safari hii utafiti umebaini kuwa matumizi ya nguo za ndani yamekuwa yakiwaathiri wanaume wengi.

Mtafiti wa Uingereza, Profesa Richard Sharpe anasema tatizo hilo linaweza kuepukwa ikiwa mhusika atajitahidi kuvaa nguo zinazokubalika na mahala alipo. Hata hivyo, anapendekeza uchunguzi zaidi ufanywe ili kulinda kizazi cha sasa na kijacho.

Mtafiti huyo kutoka Chuo Kikuu cha Edinburgh anasema: “Uingereza suala hili halijawahi kuonekana wala kutiliwa mkazo na kuwa kipaumbele katika afya, labda kwa sababu ya wasiwasi kwamba sehemu za mwanamume zinatakiwa kubanwa. Hivi sasa hakuna shaka kwamba suala hilo ambalo liliongelewa hapo awali lina ukweli ndani yake, hivyo ni wakati kwa watu wote kuchukua hatua.”

“Kutokuchukua hatua kutasababisha familia nyingi kukosa watoto na hivyo idadi ya watu itapungua, lakini katika hali ya kawaida, ni vyema watu wakaelimishwa namna ya uvaaji. Sehemu za joto mtu anatakiwa kuvaa pamba na si nailoni ili kulinda mbegu zake.”

Profesa Sharpe anasema bado wanasayansi wana kazi kubwa kwani mpaka sasa karibu kila eneo ambalo wanasayanasi wamelichunguza limebainisha kuchangia tatizo hilo, lakini mpaka sasa wanafikiri kuwa vyakula vyenye mafuta na vile vyenye kemikali nyingi vina mchango mkubwa zaidi katika tatizo hilo.

Watafiti ambao walitumia takwimu kutoka katika vituo vya afya 126, waligundua kuwa tangu mwaka 1989 mpaka 2005, kulikuwa upungufu wa uwezo wa manii kwa mwanamume kufanya kazi kwa asilimia 32.2, kiwango ambacho ni karibu asilimia mbili kwa mwaka.

Watafiti walisema: “Kwa ufahamu wetu, ni utafiti wa kwanza kufanyika na umehusisha mbegu za kiume hai na uwezo wa manii katika nchi nzima kwa kipindi kirefu.”
“Huu ni utafiti mkubwa na unatoa onyo kali kiafya kwa jamii. Lakini huwezi kumlazimisha mtu kuhusu matumizi ya nguo za ndani,” wanasema.

LULU BADO MAJI YA SHINGO, ANAENDELEA KUSOTA JERA NA UJAUZITO WAKE

"Hata hivyo, jana upande wa mashtaka ulieleza mahakamani kuwa kwa sasa imebadilisha mashtaka kutoka kuua kwa kukusudia na kuwa kuua bila kukusudia, kinyume cha kifungu cha 195 cha CP"

MSANII Elizabeth Michael, maarufu kama Lulu, ameepuka adhabu ya kunyongwa hadi kufa kwa tuhuma za kumuua msanii mwenzake, Steven Kanumba baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kumbadilishia mashtaka, ambapo sasa anatuhumiwa kuua bila kukusudia.
Kutokana na mabadiliko hayo, Lulu ameepuka adhabu hiyo kwani hata kama atapatikana na hatia, adhabu yake ni kifungo cha maisha au kuachiwa huru.
Hii inatokana na kifungu cha 196 cha kanuni za adhabu ya kosa la kuua bila kukusudia, ambapo anayepatikana na hatia anaweza kuhukumiwa kifungo cha maisha, miaka kadhaa au kuachiwa huru.
Hata hivyo, baadhi ya wanasheria waliliambia gazeti hili kwamba uzoefu wa adhabu nyingi za kuua pasipo kukusudia zilizowahi kutolewa nchini, ni kati ya miaka 15 na wengine waliachiwa huru.
Lulu alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Aprili 11, mwaka huu akikabiliwa na tuhuma za kumuua Kanumba Aprili 7, 2012.
Alikuwa akidaiwa kutenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 196 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), shtaka ambalo mshtakiwa anayepatikana na hatia adhabu yake ni kunyongwa hadi kufa.
Hata hivyo, jana upande wa mashtaka ulieleza mahakamani kuwa kwa sasa imebadilisha mashtaka kutoka kuua kwa kukusudia na kuwa kuua bila kukusudia, kinyume cha kifungu cha 195 cha CP.
Mshtakiwa huyo alitarajiwa kusomewa mashtaka hayo mapya jana pamoja na maelezo yote ya kesi, ambapo angesomewa ushahidi wa mashahidi wote pamoja na vielelezo muhimu katika kesi hiyo.
Hata hivyo, hatua hiyo ilikwama kutokana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka anayeiendesha kesi hiyo kutokuwapo mahakamani na badala yake aliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Ofmedy Mtenga.
“Upelelezi wa shauri lako umeshakamilika na tungeweza kukusomea comital (maelezo ya kesi) leo, lakini kwa kuwa waendesha mashtaka hawapo basi tunaliahirisha mpaka tarehe nyingine.”, alisema Hakimu Mkazi Agustina Mmbando, anayesikiliza kesi hiyo katika hatua hiyo ya awali.
Taarifa hizo za kukamilika kwa ushahidi wa kesi hiyo zilipokewa kwa furaha na shangwe na msanii huyo, kiasi kwamba alishindwa kujizuia kuonyesha furaha yake.
Wakili wake Peter Kibatala aliiomba mahakama itoe ahirisho fupi hadi Ijumaa kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa mashtaka haya mapya pamoja na maelezo ya awali.
Hakimu Mmbando alikubaliana na ombi hilo la Wakili Kibatala na akaahirisha kesi hiyo hadi Ijumaa.

CHAMA CHA NCCR-MAGEUZI CHAMEGUKA MKOANI MANYARA

 
"Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Godbess Lema akipeana mkono na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama cha NCCR-Mageuzi (Bara) Lawrence Surumbu Tara na Diwani wa kata ya Bashnet Wilayani Babati Mkoani Manyara  ambaye jana  alitangaza kujivua udiwani na vyeo vyote alivyokuwa navyo NCCR-Mageuzi na kujiunga na Chadema mjini Babati jana" 

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Lawrence Tara, amejivua uanachama wa chama hicho na kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Tara ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Bashnet, wilayani Babati,  Mkoa wa Manyara tangu mwaka 2000, alitangaza uamuzi huo mbele ya waandishi wa habari jana, baada ya kupokewa Chadema na Mjumbe wa Kamati Kuu wa chama hicho, Godbless Lema.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na kiongozi mwingine wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini, Ally Bananga.
Tara alitoa sababu mbili zilizomfanya aihame NCCR-Mageuzi na kujiunga na Chadema; upendeleo na dhuluma kwa watumishi wa chama hicho.
Alidai kwamba baadhi ya viongozi wa NCCR-Mageuzi wanaonyesha upendeleo wa wazi kwa kigezo cha urafiki kama kifanyavyo chama tawala, CCM.
Alisema yeye ni mmoja wa waathirika wa mfumo huo mbovu ndani ya NCCR- Mageuzi, baada ya chama hicho kumtelekeza katika kudai haki yake ya ubunge aliyodai kwamba iliporwa na CCM.
“Tunahitaji chama cha siasa kilicho makini na ambacho Watanzania tunapaswa kuunganisha nguvu zetu kwa pamoja bila kutengana na kwa maoni yangu NCCR-Mageuzi siyo chama cha aina hiyo,” alisema Tara.
Akifafanua madai ya kudhulumiwa na CCM, Tara alidai kwamba alishinda ubunge wa Jimbo la Babati Vijijini, lakini akadhulumiwa.
Alisema katika mazingira hayo amebakiwa na chaguo mojawapo kati ya kubaki ndani ya chama kisichokerwa na hali hiyo na ambacho baadhi ya viongozi wake wanaendeleza upendeleo wa urafiki na undugu.
“Nikaona bora kujitenga na kuachana na chama chenye viongozi wa aina hiyo na kutafuta chama imara ambacho hakina simile na mambo kama hayo. Pia chenye kupigania haki, ukweli na ambacho kimepania utawala bora na ustawi wa Watanzania,” alisema.
“Ninaamini Chadema ni chama makini kilichopania kutokomeza dhuluma, uovu na ufisadi wa kidola na kuleta ustawi wa Tanzania,” alisema na kuwaomba wakazi wa Bashnet, Manyara na
Watanzania kumuunga mkono.
Akizungumza katika mkutano huo, Lema alimpongeza Tara na kusema chama hicho sasa kimeongezewa nguvu.
“Huyu ni sawa na Leonel Messi (mchezaji soka mahiri wa klabu ya Barcelona na Argentina). Sasa huwezi kumleta achezee AFC ya Arusha na Babati Stars halafu mpate mafanikio kutokana na mfumo uliopo, huyu anatakiwa awe Manchester United au timu nyingine kubwa,” alisema Lema.
Alisema viongozi wa chama chake badala ya kumpa ushirikiano ili aweze kushinda ubunge, Mwenyekiti wake alikubali kupewa ubunge wa kuteuliwa na Rais na hivyo Tara kuachwa mwenyewe.
“Uso umeumbwa na haya kuna vitu ukishakula huwezi kupinga. Hivyo jambo bora ni kuondoka huko na kwa hili nampongeza Tara kwa kuacha vyeo vyote ikiwemo posho za vikao vya udiwani na posho ya kila mwezi,” alisema Lema.
Alisema Tara anatarajiwa kupewa kadi ya chama hicho na Mwenyekiti wa Chadema,  Freeman Mbowe au Katibu Mkuu wake, Dk Wilbroad Slaa kwa kuwa yeye hawezi kufanya hivyo kutokana na nafasi kubwa aliyokuwa nayo mwanachama huyo mpya.

KAMATI KUU YA CHADEMA IMEADHIMIA MAKUBWA, YASOME HAPA

 
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe
“Kama CCM wakitumia polisi sisi tutapambana kwa njia nyingine ambayo sio vurugu wala kugombana na vyombo vya dola” alisema Mbowe".
0
Share
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema mwaka 2013 utakuwa mwaka wa chama hicho kutumia nguvu ya umma, itakayolenga kuishinikiza Serikali kuyafanyia kazi mambo ya msingi ambayo yamekuwa yakipigiwa kelele tangu mwaka 2010.
Amesema kutokana na hali hiyo kuanzia Januari mwakani hakuna kulala wala mtu kupumua, kwamba chama hicho kitafanya harakati za kisiasa za aina yake ikiwa ni pamoja na kuifanyia maboresho Operesheni yake ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C).
Akisoma maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho iliyokutaka kwa siku mbili Dar es Salaam jana, Mbowe alisema tangu 2010 wamekuwa wakiitaka Serikali kutekeleza masuala mbambali lakini imekuwa haifanyi hivyo.



“Kama CCM wakitumia polisi sisi tutapambana kwa njia nyingine ambayo sio vurugu wala kugombana na vyombo vya dola” alisema Mbowe.

Alifafanua, “Septemba 9, mwaka huu tulifanya kikao cha Kamati Kuu baada ya mauaji ya aliyekuwa Mwandishi wa Habari wa Televisheni ya Channel Ten, Daudi Mwangosi na kumwandikia barua Rais Jakaya Kikwete tukimtaka aunde tume huru ya kimahakama ya uchunguzi wa jambo hili, ila mpaka leo kimya.”

Mbowe ambaye alikuwa ameambatana na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willbroad Slaa alisema, “Pia nimewahi kukutana na Rais Kikwete na kumsisitiza suala hili, lakini mpaka leo hii umepita zaidi ya mwezi mmoja hakuna jibu lolote.”
Alisema kwa muda wa miezi mitatu chama hicho kilisitisha mikutano yake ya M4C iliyokuwa ikifanyika mikoa mbalimbali nchini, ili kusubiri hatua zitakazochukuliwa na Rais Kikwete baada ya kumwandikia barua hiyo, ambayo pamoja na mambo mengine ilitaka kuchukuliwa hatua kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, maofisa wa juu wa Jeshi la polisi pamoja na Makamanda wa polisi wa Mkoa wa Morogoro na Iringa.

Alisema katika kikao hicho mambo yaliyojadiliwa na ambayo watakayowasilisha bungeni ni pamoja na kutofanyika kwa chaguzi za marudio katika kata 13 nchini, licha ya kuwa umeshapita zaidi ya mwaka mmoja.

“Katika hili inaonekana wazi kuwa CCM ina hofu ya kushindwa, zipo kata 13 nchini ambazo zipo wazi kwa zaidi ya mwaka sasa na uchaguzi haujafanyika, hii ni kinyume na sheria za uchaguzi zinazoeleza kuwa uchaguzi unatakiwa kufanyika ndani ya siku 90 baada jimbo au kata kutokuwa na mwakilishi” alisema Mbowe.

Alisema jambo jingine lililojadiliwa ni kuboreshwa kwa daftari la kudumu la wapiga kura ili kila mwananchi mwenye sifa za kupiga kura awe na haki ya kufanya hivyo.

“Jambo jingine ni Katiba, kamati kuu imetoa mapendekezo yake kwamba wakati mchakato wa kupata Katiba Mpya ukiendelea, tunataka ufanywe utaratibu wa kubadili sheria mbalimbali ikiwemo ya uchaguzi ya mwaka 1985,” alisema Mbowe.

Alifafanua zaidi, “Sheria hii ikibadilishwa italifanya taifa kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi isiyofungamana na upande wowote pamoja na kuboresha daftari la kudumu la wapigakura.”

 source facebook

Haya ndiyo tuliyoadhimia kama kamati kuu ya chama, kikao kilichodumu kwa siku mbili mfululizo hapa jijini Dar es salaam,

1.KIKAO cha kamati kuu kilikuwa cha
kawaida ,hakuna jambo la dharula

2.Mchakato wa katiba mpya usiathiri
mabadiliko ya sheria nyingine kama
mabadiliko ya sheria ya uchaguzi

3.Mwaka 2013,ni mwaka wa nguvu ya
umma,hakuna kubembelazana na
serikali rais kikwete hajajibu madai ya
yetu kwa hiyo tutamshinikiza.

4.sehemu ambazo CCM wanaogopa kuitisha
uchaguzi,tutawalazimishwa kuitisha
uchaguzi kata za arusha
mjini,sengerema,nk.ziko 15

5.Uongozi wa KARATU wa CHADEMA
Tumeusimamishwa kwa muda mpaka chama
kitakapokamilisha uchunguzi wake
huko wanasheria Marando na Prof Safari
watachunguza kashfa za mtu mmojammoja
huko karatu, kumekuwa na kashfa kwenye
miradi ya maji na ardhi.

6.Hatua za kisheria kufuatia matukio ya
uchaguzi wa ilemela mwanza,baada ya
madiwani 2 kufukuzwa uanachama
zitaendelee kuchukuliwa,pia hatua za kisiasa
zianzishwe kudai uwajibikaji wa
halmashauri ya jiji la mwanza ili haki
itendeke.

7.kamati kuu imetambua kutapatapa kwa
CCM juu ya sera zake za katiba mpya,elimu
bure na bei ndogo za vifaa vya ujenzi CCM
haiaminiki,kwa hiyo CHADEMA tutaendelee
kuunganisha umma ili CCM iondolewe 2014
na 2015

8 M4C itaendelee kwa kasi mapema mwaka
2013,sekretariati itatangaza ratiba januari.

9.juu ya hoja binafsi za wabunge wetu zito na mdee(kuhusu uporaji wa
ardhi na mabilioni ya Uswis),pamoja na
hoja ya Tundu Lisu juu ya uteuzi holela wa
rais wa majaji,kamati kuu imependekeza
maazimio ya bunge yafuatwe na baadaye
kidogo kama hairidhiki kamati kuu
itaelekeza nini kifanyike kwa hatua za ziada

10.Kamati kuu imesikitika kuwa rais
amepuuza barua ya yetu juu ya
kuunda tume ya kimahakama kuhusu
mauwaji mbalimbali nchini.hivyo M4C
itatumika mwaka 2013 kumshinikiza rais
kujibu barua hiyo na kutekeleza yale barua
inaelekeza yafanyike
Kamati kuu imesisitiza kuwa mwaka 2013
ni mwaka wa nguvu ya umma,na hakuna
tena kubembelezana na serikali.

Sisi kama chama tunatambua mchango wenu sana, kwa pamoja tutapata mabadiliko tuyatakayo

Kiongozi wenu
Freeman Aikaeli Mbowe (Mb)