ELIAS BARNABAS: THT imenifikisha hapa nilipo | Send to a friend |
Saturday, 28 May 2011 18:05 |
0diggsdigg Furaha MaugoMAFANIKIO ya wasanii wanaopikwa ndani ya nyumba Nyumba ya Vipaji Tanzania (THT), tangu kuanzishwa kwake yanathibitisha kazi nzuri inayofanywa na wasimamizi wa nyumba hiyo. Mmoja wa wasanii walitoka THT ni Elias Barnabas, maarufu kwa jina la Barnaba ambaye amefanikiwa kushinda tuzo ya Wimbo bora wa Zouk, katika tuzo za muziki za Kilimanjaro mwaka 2010/11. Alijiunga na THT, mwaka 2006 kutokana na msukumo kutoka kwa rafiki yake waliyekuwa wanaimba, kupiga vyombo na kusali naye kanisani. Tangu ameingia katika nyumba hiyo ya kuzalisha, kutengeneza na kukuza vipaji, Barnaba ametawala sana midomoni mwa wapenzi wa muziki wa kizazi kipya. Hii ni kutokana na baadhi ya nyimbo zake alizoimba na kufanya vizuri katika anga la muziki wa kizazi kipya hapa nchini. Licha ya kuimba, Barnaba ana uwezo mkubwa wa kutumia ala mbalimbali za muziki kama vile gita na ‘keyboard’. Pia ana uwezo wa kupangilia sauti yake kwa ustadi na kutawala jukwaa vyema anapokuwa kukwaani. Ni kutokana na uwezo wake huo, Barnaba amepewa jukumu la kufundisha wasanii wenzake katika kundi la THT. Mafanikio ya baadhi ya nyimbo za kizazi kipya, zinazofanya vizuri hivi sasa zimetungwa na Barnaba, nyimbo hizo ni pamoja wimbo wa Mwasiti (Kisa Pombe), wimbo wa Ray C, (Watanionaje), ‘Kizunguzungu’ ulioimbwa na Rachel, ‘Najua’ ulioimbwa na Linah na ‘Shukurani’ ulioimbwa na Nakaaya. Nyingine ni ‘Wrong number’ aliyoimbwa na Linah na ‘Milele daima’, wimbo ambao unaofanya vizuri katika chati za vituo vingi vya redio na televisheni. “Ninashukuru Mungu sasa hivi uwezo wangu ni mkubwa kwenye kuimba, kutumia vyombo na hata kuingiza sauti studio,” anasema Barnaba alipozungumza na Mwananchi Jumapili. Kuonyesha kuwa anakipaji cha hali ya juu na anafanya kazi yake kwa umakini ilimchukua takribani miaka miwili (2008-2010)kukamilisha albamu yake ya ‘Njia Panda’, ambayo alishirikiana na Amini iliyokuwa na jumla ya nyimbo 14. Baadhi ya nyimbo zinazopatikana katika albamu hiyo ni ‘Njia panda’ aliyoimba na Pipi, ‘Muongo’ , ‘ ‘Robo saa’, na ‘Mbala mwezi’ zote ameimba akishirikiana na Amini, Wrong Number aliyoimba na msanii bora wa kike mwaka 2011, Linah. Nyingine ni ‘Kodi Mangasubi’ , ‘Nivumilie’, ‘Nimelimiss’, ‘Baby I Love’, ‘mdomo’, ‘ Mwongo’, ‘Dukuduku’ na ‘Huruma’. Barnaba anasema ingawa hakusoma sana, mafunzo aliyopta THT ndiyo yaliyomfikisha hapa alipo na kufafanua: “Niliweka juhudi kubwa kwenye mafunzo nilipokuwa darasani na kuyafanyia kazi mambo yote niliyofundishwa na mwalimu wangu. “Matunda ninayopata yametokana na heshima na uvumilivu niliokuwa nao kipindi chote cha mafunzo. Hivi sasa ninaweza kukidhi mahitaji yangu binafsi na nimehama nyumbani sasa nakaa kwangu na ninapata kila ninachohitaji,” anasema Barnaba. Barnaba anasema anavutiwa sana na kazi za wanamuziki wengine wa Afrika, kama vile Fally Ipupa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Barnaba anampamgo wa kurudi shule kujiendeleza. “Kwa kuwa sikubahatika kumaliza elimu yangu vizuri nina mpango wa kurudi tena shule, nafikiria kuendelea na elimu ingwa sijajua nataka kusomea kitu gani,” anasema. Wasifu Alizaliwa Agosti 8, 1990 mkoani Morogoro, alipata Shule ya Msingi Kinondoni, Dar es Salaam mwaka1998 – 2004, alijiunga na Mikoji Sekondari na kuishia kidato cha tatu. Ni mtoto wa kwanza katika familia ya watoto watatu. Kabla ya kuingia katika muziki alikuwa akifanya biashara ya kuuza genge nyumbani kwao na alikuwa akipiga vyombo mbalimbali vya mziki kanisani kwao. Mbali na muziki Barnabas, anamiliki duka la kuuza nguo lililopo maeneo ya Kinondoni na siku za mwisho wa juma hupenda kutembelea ufukweni. |