CCM yakiri kuwahoji na Rostam, Lowassa na Chenge | Send to a friend |
Saturday, 04 June 2011 10:17 |
Mwandishi Wetu CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimethibitisha kwamba kimewahoji Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge ikiwa ni moja ya hatua ya kutekeleza maazimio ya Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho uliofanyika Aprili 10 hadi 11 mjini Dodoma. Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa CCM, Willison Mukama ilisema kuwa hiyo ni moja hatua za awali zilizochukuliwa na kuongeza kuwa nyingine zitafuata baadaye. Alisema hatua hiyo ya awali, Makamu Mwenyekiti CCM (Bara), Pius Msekwa alikutana na wanaotajwa katika tuhuma hizo katika sura mbili, kwanza ya nafasi yake ndani ya chama na pia kama mzee wa CCM. Mukama alisema Mei 26, mwaka huu Msekwa alikutana na Rostam ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na siku Iliyofuata alikutana na Lowassa ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa. Alisema siku hiyo hiyo ya Mei 27, mwaka huu alikutana na Mjumbe mwingine wa Halmashauri Kuu, Chenge."Kwa vile Msekwa alikutana kwa faragha na viongozi hao mmoja mmoja, hakuna anayejua kilichozungumzwa. Ni Mzee Msekwa na wao peke yao," alisema katika taarifa hiyo. Alisema hatua itakayofuata baada ya hapo ni kufikisha kwenye vikao vya chama taarifa ya mambo yaliyojiri wakati wa mazungumzo baina ya Msekwa na viongozi hao."Endapo vikao husika vitaamua lolote kuhusiana na taarifa hiyo, umma utajulishwa," alisema. Katika mkutano huo wa Halmashauri pamoja na mambo mengine, uliwataka viongozi wa CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi kutafakari, kujipima na kuchukua hatua wenyewe kwa maslahi ya chama na kwamba wasipofanya hivyo chama kitawawajibisha |
No comments:
Post a Comment