Magufuli apeleka Sh1bn Loliondo | Send to a friend |
Thursday, 31 March 2011 21:56 |
0diggsdigg Neville Meena na Mussa Juma, SamungeWAZIRI wa Ujenzi, Dk John Magufuli, jana aliingia katika Kijijini Samunge kwa mchungaji Ambilikile Masapila na kupata kikombe cha dawa, kisha kutangaza neema ya kujengwa kwa barabara kuu inayoingia kijijini hapo. Magufuli aliuambia umati wa watu uliokuwa ukisubiri zamu yao kunywa dawa kuwa, Serikali itatumia Sh1.05 bilioni kwa ajili kutengenenza barabara hiyo ili iweze kupitika wakati wote kwa lengo la kuwarahisishia usafiri wanaokwenda kunywa dawa kwa Babu Masapila. Barabara inayoingia katika kijiji hicho ambacho kimeshuhudia maelfu ya magari yakiingia kila siku tofauti na ilivyokuwa awali, ipo katika hali mbaya kiasi cha baadhi ya maneo kutoruhusu magari kupishana. Kwa mujibu wa Magufuli, Serikali ilikwishatoa Sh500/-milioni kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kuanzia Mto wa Mbu eneo la Kigongoni, Ngaresero, Samunge hadi kuungana na barabara ya kutoka mkoani Mara. Dk Magufuli alisema jana ndio aliuagiza uongozi wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) Makao Makuu kutuma Sh500 milioni ili kuharakisha ujenzi huo. "Tayari fedha hizo zimeshatumwa Tanroads mkoani Arusha na Meneja wa Mkoa, Kakoko (Deodatus), niko naye hapa hivyo kazi itakwenda haraka ili watu wanaokuja kwa mchungaji kunywa dawa wasiendelee kuteseka," alisema Dk Magufuli huku akishangiliwa na mamia ya watu waliokuwa wakimsikiliza. Waziri pia huyo alisema kwa mamlaka aliyonayo, atawasiliana na uongozi wa Mfuko wa Barabara ili utume fedha za dharura kiasi cha Sh50 milioni kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorogoro kwa ajili ya kufanya matenegenezo mengine ya barabara, wilayani humo. Alisema fedha zilizotengwa kwa ajilii ya barabara za nchi nzima kupitia mfuko huo zinafikia Sh286 bilioni katika bajeti ya mwaka 2010/11, na kwamba upo uwezekano mkubwa wa fedha za dharura kupatikana kwa ajili ya matenegenezo ya barabara ya Samunge. Matengenezo Kwa mujibu wa Magufuli, matengenezo ya barabara hiyo ni muhimu sana kwani awali barabara hiyo kuanzia Mto wa Mbu ilikuwa ikipitisha magari kati ya 20 na 25 kwa siku lakini, sasa yameongezeka hadi 3,500 kwa siku. "Nasema barabara hii ni muhimu sana hivyo nakuagiza Meneja wa Tanroads mkoa wa Arusha kuhakikisha mkandarasi aliyepewa kazi ya kutengeneza barabara hii anafanya kazi usiku na mchana ili ikamilike, akizembea fukuza," alisema Magufuli na kuongeza: "Sheria namba 17 ya mwaka 1997 na vifungu vyake inatoa mamlaka ya kuondolewa kwa mkadarasi anayezembea. Pia sheria inaelekeza kufikishwa mahakamani kwa wakandarasi wa aina hiyo, na akitiwa hatiani na anaweza kufungwa miaka mitano. Hivyo basi sheria ipo na pale tutakapolazimika tutaitumia". Magufuli aliuagiza uongozi wa Halmashauri ya Ngorogoro kuwasilisha maombi ya dharura ya fedha za matengenezo ya barabara katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ili kuwezesha matengenezo ya barabara nyingine kufanyika. "Tukiacha barabara ya kuja huku, nimetembelea barabara zenu katika wilaya ya Ngorongoro, kwa kweli ni mbaya sana hivyo zinahitaji matengenezo,"alisisitiza. Juzi Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Eliasi Ngorisa, aliliambia Mwananchi kwamba halmashauri yake ilikuwa imeomba kiasi cha Sh400 milioni kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya kuifanyia matengenezo ya dharura barabara zinazoingia kijijini Samunge. Dk Magufuli pia alimwelekeza Meneja wa Tanroads mkoani Arusha kuandaa mpango wa matengenezo ya barabara za Ngorongoro na kuwasilisha mapendelezo yake serikalini kwa ajili ya utekelezaji wake. "Kaandike mpango huo sasa na ulete ili tuone jinsi ya kufanya, kama hujui kuandika tafuta watu wakusaidie," alisema Magufuli na kusababisha umati wa watu kuagua kicheko. Waomba msaada Tofauti na viongozi wengine waliowahi kufika kwa mchungaji Mwasapila, Waziri Magufuli aliruhusu maswali kutoka kwa wananchi waliokuwa wakimsikiliza. Wengi wao walilalamikia hali mbaya ya mazingira. "...pamoja na kwamba wewe si Waziri wa Afya, lakini tunajua unatoka Serikalini, tunaomba utusadie maana afya zetu zipo hatarini. Huwezi kuamini kwani huko barabarani unakuta mtu anajisaidia haja kubwa hapo,na mtu mwingine anakula chakula, kwa kweli hali ni mbaya tunaomba msaada,"alisema Nicholas Mwangoka. Akijibu hoja hiyo, Waziri Magufuli alisema atawasilisha taarifa yake kwa Waziri Mkuu ambaye yupo mkoani Arusha na kwamba anaamini kupitia njia hiyo waziri wa sekta ya afya atafikishiwa ujumbe ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa. Mapema mchungaji Mwasapila kupitia kwa msaidizi wake, aliomba Serikali ijenge daraja katika mto wa Samunge ambao umekuwa kikwazo cha magari kuingia kijijini hapo kwani hufurika kila mvua zinaponyesha. Pia mchungaji huyo alimshukuru Waziri huyo kwa ahadi aliyoitoa akisema kuwa hatua hiyo inamtia moyo kuendelea kutoa tiba kwa wagonjwa wanaofika nyumbani kwake. "Nakushukuru sana kwa ujio wako na yale uliyoyasema, unatupa matumaini,unatupa moyo, asante tunashukuru sana," alisema Masapila. Foleni yapungua Samunge Katika hatua nyingine, foleni ya magari ambayo ilikuwa zaidi ya kilometa 30 kutoka eneo analotolea tiba mchungaji Masapila sasa imepungua. Kupungua kwa foleni hiyo kumetokana na utaratibu mpya wa kuingiza magari katika kijiji cha Samunge ambao unatarajiwa kuanza leo, pia kutokana na kasi ya mchungaji huyo katika kugawa dawa. Tacaids yawaasa wagonjwa Ellen Manyangu anaripoti kutoka Dar es Salaam kuwa, Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids), imewataka wagonjwa waliokunywa dawa ya Mchungaji Masapila kutoacha kuendelea na dozi walizopewa hospitalini kwa kuwa dawa hiyo haijathibitika kutibu Ukimwi. Mratibu wa tume hiyo Dk Bwijo Bwijo alisema jana kuwa utafiti bado unaendelea kujua endapo kikombe hicho cha babu, kinaweza kutibu magoonjwa yanayoelezwa. Alisema hayo jana alipokuwa akizungumza katika mjadala ulioandaliwa na Kituo cha Radio Clouds FM na kufanyika katika hoteli ya Kempisky jijini Dar es Salaam jana asubuhi. Akizungumza katika mjadala huo, Dk Bwijo alisema dawa ya Mchungaji Masapila bado inafanyiwa utafiti ili kuthibitisha kama inatibu, hivyo wananchi hawapaswi kuacha kutumia dawa za kitabibu ghafla. Kwa mujibu wa Bwijo, jitihada za kuthibitisha ubora wa dawa hiyo bado zinaendelea kwa ufadhili wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Kudhibiti Ukimwi (UNAIDS). “Wagojwa wote walioko kwenye matibabu ya dawa za kitaalamu na wamekunywa kikombe cha dawa ya babu wasiache kutumia dawa zao mpaka itakapothibitishwa kuwa dawa hiyo ni halali na inatibu,” alisema Dk Bwijo. Mwenyekiti Mstaafu wa Mtandao wa Wanaoishi na Ukimwi Afrika (TANEPHA), Alex Margery, alisema suala la Loliondo limejaa sura ya Ukimwi na kutahadharisha kuwa watu wasiache kutumia dawa za kitaalamu kwa kuwa dawa ya babu bado haijathibitishwa. Alisema walishajitokeza watu mbalimbali katika nchi za Kenya na Afrika Kusini na kutoa dawa zilizoaminika kuwa zinatibu maradhi sugu ikiwemo ukimwi, lakini baadaye zilisababisha watu wengi kufa kutokana na kuacha kutumia dawa za kitaalamu kwa imani kuwa wamepona. “Hili ni jambo la hatari sana hasa kwa jamii yetu kwani wagonjwa wanaacha kutumia dawa za kisayansi zilizothibitishwa kutibu, au kupunguza makali ya maradhi waliyonayo kwa imani kikombe cha dawa wanachopewa Loliondo kinawaponyesha…, "alitahadharisha Margery. Aliongeza dawa za kupunguza makali ya virusi vya ukimwi ARV zilikuwa katika dozi kubwa ya vidonge 14 kwa siku moja, lakini kadri siku zinavyoongezeka dozi hiyo inapungua na hivi sasa ni kidonge kimoja kwa siku. Mtaalam wa Afya ya Jamii na Ukimwi, Dk Bennect Fimbo, alisema awali ugonjwa wa Ukimwi ulikuwa tishio kwa jamii kwa vile hawakuwa na uhakika wa mtu kuishi nao muda mrefu lakini, hivi sasa mtu anaweza kuishi nao kwa muda wa miaka 20. Aliongeza kuwa mti wa Mugariga unaotumiwa na babu kama dawa umefanyiwa utafiti kwa muda mrefu, hivyo inapaswa uchunguzi wa ziada ufanyike ili kubaini mti huo unatibu magonjwa yapi na dozi yake. Kandoro aweka udhibiti Kutoka Mwanza Frederick Katulanda na Sheila Sezy wanaripoti kuwa, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Abbas Kandoro, amewaagiza wasafirishaji wa watu wanaokwenda kutibiwa kwa Mchungaji Masapila kuwaorodhesha watu wote ili kuweka kumbukumbu. Akizungumza jana katika kikao chake na wamiliki a mabasi, Kandoro alisema Serikali imepanga utaratibu maalum ikiwa ni pamoja na kuweka vizuizi kwa lengo la kupunguza msongamano na kuwezesha wagonjwa kumfikia babu haraka zaidi. Alisema Serikali imetambua kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la watu wanaoenda Loliondo kwa ajili ya matibabu hayo hivyo utaratibu huo mpya utasaidia kupunguza msongamano. Alifahamisha kuwa kuanzia sasa magari yote yanayotoka Mwanza na Kagera na wageni kutoka nchi za Rwanda, Uganda na Burundi kwenda Loliondo, wanapaswa kujiandikisha jijini Mwanza na kuacha majini yao katika kizuizi cha Magu. Magari yatakayoruhusiwa kuondoka na kupita katika vizuizi ni yale yenye nguvu maalumu (four wheel drive) na mbasi. Malori ya aina yote hayaruhusiwi kwenda huko, alisema. Akizungumzia suala la nauli kuwa juu, Kandro alisema serikali haitaingilia utozaji wa nauli bali kuhakikisha inaboresha mazingira ya Loliondo na kwamba nauli zitashuka zenyewe. |
No comments:
Post a Comment