Tuesday, November 22, 2011

HOTUBA YA RAISI KIKWETE KWA WAZEE WA CCM-DAR ES SALAAM


HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE,
KWA WANANCHI KUHUSU HALI YA UCHUMI NCHINI NA MCHAKATO WA KATIBA MPYA, TAREHE 17 NOVEMBA, 2011

Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa,
Mstahiki Meya,
Viongozi wa Serikali,
Wazee wangu,
Ndugu Wananchi,

Nakushukuru Mkuu wa Mkoa na viongozi wenzako wa Jiji la Dar es Salaam kwa kuniandalia fursa hii ya kukutana na Wazee wa Dar es Salaam.  Nawashukuru sana wazee wangu kwa kuitikia wito wangu huu wa kukutana nanyi.  Nimefarijika sana kwa mahudhurio yenu makubwa pamoja na taarifa kuwa ya muda mfupi.
Nimewaiteni wazee wangu nizungumze nanyi na kupitia kwenu nizungumze na wananchi wote wa Tanzania.  Mwisho wa mwezi uliopita sikuweza kufanya hivyo kupitia utaratibu wetu wa kawaida kwa sababu nilikuwa kwenye Mkutano wa Jumuiya ya Madola nchini Australia.  Mwisho wa Mwezi  huu nitakuwa Bujumbura kuhudhuria  Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, hivyo sitaweza kuongea na wananchi wakati huo. Lakini, yapo masuala kadhaa ambayo ni muhimu watu kupata ufafanuzi kutoka kwangu.  Kwa ajili hiyo nimeona nitumie fursa hii kuzungumza nanyi siku ya leo.   Leo nataka kuzungumzia hali ya uchumi na mchakato wa kupata Katiba Mpya.
Hali ya Uchumi
Ndugu Wananchi;
Katika kuelezea hali uchumi nchini, naomba nianze kwa kuelezea hali ya uchumi duniani kwani yanayotokea nchini yana uhusiano mkubwa na yanayotokea duniani.  Hali ya uchumi duniani siyo shwari.  Ukweli ni kwamba hali katika uchumi wa mataifa ya Marekani, Ulaya Magharibi na Japan haijatengemaa kufuatia machafuko ya masoko ya fedha na mdororo wa uchumi wa miaka miwili iliyopita.  Hivi sasa uchumi wa mataifa tajiri ya Ulaya , wanachama wa Umoja wa Ulaya na hasa wanachama wa Umoja wa Sarafu ya Euro unapita katika kipindi kigumu na mashaka.  Thamani ya sarafu hiyo inashuka na hata kuaminika kwake ni kwa mashaka. Mfumuko wa bei umepanda, ukosefu wa ajira umeongezeka na ipo hofu kubwa ya uchumi wa nchi hizo kudorora tena.  Lakini nchi hizi ndiyo masoko makubwa ya bidhaa zetu, watalii na bidhaa za viwandani.  Hivyo, athari zao zinatugusa na sisi.  Kuongezeka kwa mfumuko wa bei kunaongeza bei ya bidhaa tunazonunua kutoka kwao.  Aidha, kutetereka kwa uchumi wao nako kumepunguza masoko ya bidhaa zetu.
  Lakini kulegalega kwa sarafu ya Euro kumesaidia kuimarika kwa sarafu ya dola ambayo kabla ya hapo ilikuwa imepungua nguvu.  Kwa sababu hiyo thamani ya sarafu ya dola imepanda duniani ikilinganishwa karibu na sarafu nyingine zote pamoja na yetu.  Wakati huo huo bei ya mafuta imeendelea kupanda duniani kutoka dola 76.1 kwa pipa Septemba,, 2010 hadi dola 100.5 Septemba, 2011.  Jumla ya yote haya ni kuongezeka kwa mfumuko wa bei kutoka asilimia 4.2 Oktoba, 2010 hadi asilimia 17.9 Oktoba, 2011.
Ndugu Wananchi;
Serikali na vyombo husika vimekuwa vinachukua hatua mbalimbali kukabiliana na matatizo ya kushuka kwa thamani ya shilingi, bei ya mafuta, bei ya sukari na matatizo ya umeme.  Kuhusu kushuka kwa thamani ya shilingi Benki Kuu imeendelea kuchukua hatua zilizopo ndani ya mamlaka yake hususan kubana ulanguzi wa fedha za kigeni, kudhibiti matumizi ya fedha kigeni kufanyia malipo hapa nchini na kuongeza fedha za kigeni katika masoko ya fedha.  Kwa kweli uwezo wao una ukomo.  Jawabu la uhakika lipo kwenye uchumi wa mataifa makubwa kuchukua hatua thabiti kuimarisha uchumi wao ili thamani ya dola irejee mahali pake stahiki na bidhaa zetu zipate masoko ya uhakika na bei nzuri ili mapato yetu ya fedha za kigeni yaongezeke.
Kwa upande wa mfumuko wa bei, ni vyema tukatambua kuwa Asilimia 75 ya ongezeko hili imetokana na kupanda kwa bei ya chakula na mafuta.   Asilimia 25 iliyobaki imechangiwa na sera za fedha.  Kwa upande wa mafuta, tunaamini utaratibu wa kuagiza mafuta kwa pamoja utasaidia kudhibiti bei za ndani za bidhaa hiyo.  Aidha, itsaidia kupunguza makali ya athari ya bei za dunia zinazopanda.  Kwa upande wa bei za vyakula, tatizo kubwa ni uhaba wa chakula katika nchi jirani unaosababisha wote kututegema sisi na hivyo kupandisha bei nchini.  Tunaendelea kudhibiti magendo ya chakula na wakati huo kutengeneza taratibu rasmi za kuziuzia chakula nchi jirani.
Kwa upande wa sukari tumeamua kuruhusu tani 120,000 ziagizwe ili kupunguza uhaba wa bidhaa hiyo na kushusha bei yake.


Hatuko Peke Yetu

Ndugu Wananchi;
Ni vizuri tukafahamu kuwa, matatizo ya mfumuko wa bei na kushuka kwa thamani ya fedha yetu siyo yetu peke yetu.  Nchi zote za Afrika Mashariki zinakabiliana na matatizo haya.  Kwa mfano, mfumuko  wa bei  kwetu ni asilimia 17.9, Kenya wako asilimia 18.9 na Uganda asilimia 30.5.  Wakati mwaka wa jana sote tulikuwa kwa watani karibu asilimia 5.  Kwa upande wa kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola sote tumeathirika.  Shilingi ya Tanzania imeshuka kwa asilimia 9.4, Kenya kwa asilimia 6.8 na Uganda kwa asilimia 17.4.  Randi ya Afrika Kusini kwa asilimia 18.7, Rupia ya India kwa asilimia 9.8, Pauni ya Uingereza kwa asilimia 6.6. na Euro kwa asilimia 9.7.
Ndugu Wananchi;
Katika kukabiliana na tatizo la umeme, Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa dharura wa kuongeza uzalishaji wa umeme.  Serikali imewawezesha TANESCO kukodi mitambo ya kuzalisha umeme kutoka kwenye makampuni ya Symbion (112 MW) na Aggreko (100 MW) na kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL (100 MW).  
Napenda niwahakikishie wananchi kuwa, ifikapo Desemba, 2011 hali ya upatikanaji wa umeme itakuwa nzuri na mgao utapungua sana baada ya kufunga mitambo mingine mipya ya kuzalisha umeme ya TANESCO (160 MW) na Symbion (60 MW).  Mikakati tuliyonayo ya muda mrefu ni kuongeza mitambo zaidi na kuongeza upatikanaji wa gesi ya kuendeshea mitambo kwa kujenga bomba kubwa la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.
Mchakato wa Katiba
  Ndugu Wananchi;
Kama mtakavyokumbuka tarehe 31 Desemba 2010 katika hotuba yangu ya kuuaga mwaka 2010 na kuukaribisha mwaka 2011 nilizungumzia maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika ambayo sasa ni Tanzania Bara tarehe 9 Desemba, 2011.  Miongoni mwa mambo ambayo niliyataja kuwa tutayafanya katika kusherehekea siku hiyo adhimu ilikuwa ni kuanzisha mchakato wa kuitazama upya Katiba ya nchi yetu kwa nia ya kuihuisha ili hatimaye tuwe na Katiba mpya.
Nilifafanua siku ile kwamba tunataka kufanya hivyo si kwa sababu Katiba yetu ya sasa ni mbaya, la hasha!  Nilieleza kwamba Katiba yetu ya sasa ni nzuri na imelilea vyema taifa letu.  Tuna nchi yenye amani, utulivu na umoja pamoja na watu wake kuwa wa rangi, makabila, dini na itikadi mbalimbali za kisiasa.  Tunayo nchi ambayo imepiga hatua kubwa sana ya maendeleo ukilinganisha na ilivyokuwa miaka 50 iliyopita.  Pamoja na hayo tunataka kuihuisha Katiba yetu ili tuwe na Katiba inayoendana na Tanzania ya miaka 50 baada ya Uhuru wa Tanzania Bara, Tanzania ya miaka 47 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na Tanzania ya miaka 47 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Kwa ajili hiyo nilielezea dhamira  yangu ya kuunda Tume Maalum ya Katiba yaani Constitutional Review Commission itakayojumuisha Watanzania wa makundi mbalimbali katika jamii yetu na kutoka pande zetu mbili za Muungano.  Aidha, nilifafanua kuwa jukumu la msingi la Tume hiyo litakuwa ni kuongoza na kuratibu mchakato wa kupata maoni ya Watanzania kuhusu nini wanachokitaka kiwemo katika Katiba yao.
Tume itasikiliza maoni hayo na baadaye kutengeneza rasimu ya Katiba mpya ambayo baada ya kukubaliwa na Bunge itafikishwa kwa wananchi kutoa ridhaa yao kwa kupiga kura.  Nilisisitiza kuwa mchakato huo utawahusisha Watanzania wote wa ngazi zote na popote walipo mijini na vijijini.  Hapatakuwa na aina yoyote ya  kuwabagua watu kwa itikadi zao za siasa, shughuli wazifanyazo, dini zao, rangi zao au jinsia zao.
Ndugu Wananchi;
Nilifarijika sana na kauli za pongezi kwangu na kwa Serikali kwa uamuzi wa kuanzisha mchakato wa kupata Katiba mpya.  Miongoni mwa waliotoa pongezi alikuwa Ndugu Freeman Mbowe, Mbunge wa Hai na Mwenyekiti wa CHADEMA  ambaye wakati akichangia hotuba yangu ya kufungua Bunge Jipya, tarehe 11 Februari, 2011; nanukuu Hansad ya Bunge aliposema “Mheshimiwa Spika, ninapenda kwenye hili, nimpongeze Rais kwa kuwa msikivu, na Rais anapofanya jema tutampongeza, Serikali yake inapofanya jema tutaipongeza na Chama chochote kitakapofanya jambo jema kwa Taifa letu, tutakipongeza.  Napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu moja ya msingi sana, kuridhia mabadiliko au kuitafuta upya Katiba ya nchi yetu.”  mwisho wa kunukuu.    Lakini siku chache baadaye Chama chake kikaja na msimamo tofauti, wakawa wanalalamikia kunyang’anywa hoja yao na kukataa Rais asiunde Tume ya Katiba na wala asihusike kabisa na mchakato huu.  Tangu wakati huo wameendesha kampeni kubwa ya kutaka Rais asihusishwe kwenye mchakato wa kubadili Katiba
 Kwa kweli watu wengi wanaoitakia mema nchi yetu walishangazwa na madai hayo na vitendo vya ndugu zetu hao.  Hii si mara ya kwanza kwa nchi yetu kufanya zoezi la marekebisho ya Katiba au hata kuandika upya Katiba tangu Uhuru na Muungano.  Mara zote hizo iliundwa Tume ya kukusanya maoni ya wananchi ambayo iliundwa na Rais.  Ndivyo ilivyokuwa wakati wa Rais wa Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere,  Rais wa Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi na Rais wa tatu Mzee Benjamin Mkapa.  Mwalimu Julius Nyerere alifanya hivyo mara tatu.  Mara ya kwanza mwaka 1963 wakati wa kubadilisha mfumo wa vyama vingi kwenda Chama kimoja, Rais aliunda Tume ya Mheshimiwa Rashid Kawawa, Amon Nsekela.  Mara ya pili wakati wa kutengeneza  Katiba ya Kudumu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 aliunda Tume ya Mzee Sheikh Thabit Kombo.  
Mwaka 1984 Mabadiliko ya Katiba ya 1977 yaliyoweka ukomo wa Urais na kuingiza katika Katiba Haki za Binadamu, yaliyotokana na mchakato uliokuwa ni wa Kichama, ambapo CCM ilikusanya maoni kupitia mtandao wa kichama kuanzia Matawi hadi kufikia Makao Makuu.  Wakati wa Rais Ali Hassan Mwinyi wa Awamu ya Pili, kulikuwa na Tume ya Jaji Mkuu Francis Nyalali iliyotuletea mabadiliko  ya nane ya Katiba yaliyoruhusu vyama vingi vya siasa.  Wakati wa Rais wa Awamu ya Tatu, mzee Benjamin Mkapa kuliundwa Tume ya Jaji Kisanga iliyoleta mabadiliko ya 13 na 14 ya Katiba ya nchi.
Hivyo la ajabu lipi kwa Rais wa sasa kuunda Tume ya Katiba?  Amepungukiwa nini Kikatiba na Kisheria ambacho Marais wenzake walikuwa nacho katika madaraka yao?  Hakipo hata kimoja!  Madaraka waliyokuwa nayo Marais waliomtangulia ndiyo aliyonayo Rais wa sasa.  Hajapungukiwa chochote kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi.  Kwa kweli hakuna hoja yoyote ya msingi ya kumuengua Rais katika mchakato wa kutengeneza Katiba ya nchi.  Haipo hoja ya Kikatiba wala ya Kisheria.  Hivi Rais asipounda Tume, nani aiunde Tume hiyo?  Na huyo atakayeunda atapatikanaje?
Juzi Bungeni msemaji wa kambi ya upinzani, katika mjadala wa Muswada wa Kuunda Tume ya Kukusanya Maoni alisema Rais ni dikteta.  Ama kweli “akutukanae hakuchagulii tusi” kama ulivyo msemo wa Kiswahili.  Hivi mimi kweli ni dikteta?  Kwa jambo lipi?  Hivi ndugu zangu Rais dikteta anatoa uhuru mkubwa kama uliopo sasa wa vyombo vya habari na wa watu kutoa maoni yao?  Kama mimi ningekuwa dikteta kweli nina hakika hata yeye asingethubutu kusema hivyo na kama angethubutu basi mpaka sasa asingekuwa anatembea kwa uhuru.  Mimi ninachofahamu ni kuwa nasemwa kwa kuwapa watu, vyama vya siasa na vyombo vya habari uhuru mkubwa mno ambao watu wanaona unatumika vibaya kusema maneno yasiyokuwa na staha au hata matusi, fitina na kupandikiza chuki katika jamii.  Labda, nijaribu kuwa dikteta kidogo watu waone tofauti yake.  Naamini kungekuwa na malalamiko makubwa zaidi ya haya.
Ndugu Wananchi;
Mimi na wenzangu Serikalini tumefanya yote ambayo Katiba ya nchi na Sheria vinaruhusu.  Ndivyo Marais walionitangulia na Serikali zao walivyofanya tena sisi tumefanya zaidi ya wao.  Wote waliunda Tume za kukusanya maoni ya Katiba na wakati wa Mwalimu Julius Nyerere liliundwa Bunge Maalum la Katiba lililojumuisha Wabunge na wananchi wengine kama tulivyoamua kufanya sisi.  Ilifanyika hivyo wakati wa kutengeneza Katiba ya Tanganyika kuwa Jamhuri na Katiba ya Kudumu ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977.  Sisi tulichofanya cha ziada ni kulihusisha Bunge kutunga Sheria ya Kuunda Tume ya kusimamia mchakato wa Katiba mpya na vile vile kuwapa wananchi wote ridhaa ya kuamua kwa kuipigia kura Katiba inayopendekezwa.  Ni kutokana na nyongeza hii ndipo tukaona busara ya kuwepo kwa Sheria maalum ya kuongoza mchakato wa kupata Katiba mpya.  Tumepanua demokrasia na kuwahusisha wananchi wenyewe siyo tu katika kutoa maoni bali pia kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu Katiba ya nchi yao, badala ya kuwaachia Wabunge na viongozi wengine Serikalini peke yao.  Kwa kweli tunastahili pongezi badala ya shutuma na lawama zisizokuwa na msingi.
Pia inasikitisha kuona au kuwasikia watu wanaojua wakijifanya ukweli huu hawaoni au  hawajui.  Baya zaidi ni pale wanapojihusisha na kupotosha ukweli na kuipaka sura isiyokuwa ya kweli kuhusu kinachofanywa na Serikali.  Mimi hujiuliza kwa nini wanafanya hivi.  Kwa nini wanafanya hiyana ya upotoshaji wote huu?  Kwa kweli sipati majibu ya uhakika.  Labda ndiyo ile dhamira ya kutaka nchi isitawalike.  Au ndiyo pengine ni ile nia ya kutaka kwenda Ikulu kwa njia ya mkato.  Ati kwa kutumia nguvu ya umma.  Basi hata hiyo nguvu unaitumia bila ya kuwa na hoja za kweli?
Ndugu Wananchi;
Nayasema haya kwa sababu kumekuwepo na upotoshaji mkubwa wa jambo hili tangu baada ya hotuba yangu ya tarehe 31 Desemba, 2010 mpaka wakati wa kuwasilishwa kwa Muswada wa Sheria wa Kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba uliomalizika leo Bungeni.  Upotoshaji wa kwanza ulikuwa ni ule wa kujenga dhana kana kwamba Serikali imewasilisha Muswada wenyewe wa Katiba mpya.  Wapo watu wamefanywa waamini hivyo wakati si kweli hata kidogo.  Huu ni Muswada ambao ukipitishwa, itaundwa Tume ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu nini wanachokitaka kijumuishwe katika Katiba yao mpya.  Kwa maneno mengine, maoni yenu mtakayoyatoa wananchi kwa Tume ndiyo yatakayotumika kutengeneza Katiba mpya.

Ndugu Wananchi;
Katika Muswada huu kuna mambo tuliyotaja kuwa ni ya msingi ambayo yamewekewa wigo wa kuhakikisha yanalindwa.  Mambo hayo ni yale ambayo yanalitambulisha taifa letu na tunu zake kuu.  Mambo yenyewe ni haya yafuatayo:  Kuwepo kwa nchi yetu na mipaka yake; kuwepo kwa Serikali, Bunge na Mahakama; kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; kuwepo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; umoja wetu, mshikamano wetu na usalama wetu; Mfumo wa uchaguzi kwa kura unaotoa fursa kwa wote; Hifadhi ya haki za Binadamu; Haki za watu; Usawa mbele ya sheria na haki; Uhuru wa kuabudu na kuvumiliana kwa imani zetu.
Kumekuwepo na upotoshaji ati huko ni kuwaziba watu midomo.  Siyo hivyo hata kidogo.  Mambo hayo yanajadiliwa, lakini siyo kwa nia ya kuyaondoa bali kuboresha.  Kwa mfano, kuhusu Muungano,  tunachosema ni kwamba hatujadili kuwepo au kutokuwepo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bali namna bora ya kuendesha shughuli za Muungano wetu.  Lakini, tulichokifanya siyo kitu kigeni, hata Rais wa kwanza alifanya hivyo mwaka 1963 alipounda Tume ya Mfumo wa Chama Kimoja cha Siasa iliyoongozwa na Mheshimiwa Rashid Kawawa.  Alitoa mwongozo na aliyataja mambo ya kulinda.  Sisi tulichokifanya ni kuyataja kwenye sheria badala ya kuwa Mwongozo wa Rais.
Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu;
Kwani Katiba ya Nchi ni kitu gani.  Katiba hutaja nchi na mipaka yake.  Kwetu sisi nchi yenyewe ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotokana na kuungana kwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika.  Pili, Katiba inaelezea jinsi nchi hiyo itakavyoendeshwa kwa maana ya mihimili mikuu mitatu ya dola ya Utawala/Serikali, Bunge na Mahakama.  Katiba inafafanua jinsi Serikali inavyopatikana, muundo wake na inavyofanya kazi.
Aidha, inaeleza jinsi Bunge linavyopatikana, jinsi linavyofanya kazi ya kutunga sheria na mahusiano yake na mihimili mingine.  Vile vile, Katiba inaeleza jinsi Mahakama inavyofanya kazi ya kutoa haki, muundo wake na jinsi Majaji na Mahakimu wanavyofanya kazi.  Kwa kweli mchakato wote huu unahusu hayo.  Tunatakiwa kutoa maoni juu ya namna gani bora zaidi na ikiwezekana namna mpya ya kuendesha shughuli za Muungano wetu na jinsi mihimili yetu inavyopatikana na kufanya shughuli zake.
Ndugu Wananchi;
Jambo lingine lililopotoshwa ni dhana ya muswada kusomwa mara ya kwanza.  Kwa mujibu wa utaratibu wa kutunga sheria, Miswada, husomwa mara tatu Bungeni.  Muswada kusomwa mara ya kwanza ni pale unapogawiwa kwa Wabunge baada ya kuchapishwa katika gazeti la Serikali siku 21 kabla ya kuwasilishwa Bungeni.  Baada ya kuchapishwa, hugawiwa kwa Wabunge.  Muswada husomwa mara ya kwanza Bungeni ili kutoa fursa kwa Mheshimiwa Spika kuwasilisha Muswada huo kwenye Kamati iuchunguze na kuutolea maoni.  Mheshimiwa Spika anaweza pia kuielekeza Kamati kutafuta maoni ya wananchi.
Baada ya Kamati kukamilisha kazi yake, Muswada husomwa mara ya pilli ambapo Muwasilishaji atatoa hoja kwamba Bunge liujadili Muswada pamoja na kutoa maelezo ya Muswada.  Mjadala huanza kwa Kamati ya   Bunge kutoa maoni yake ikifuatiwa na maoni ya Kambi ya Upinzani.  Wakati Kamati ya Bunge inapojadili Muswada, Waziri mhusika huwepo na mara nyingi maoni ya Kamati ya Wabunge na wadau hujumuishwa wakati Waziri anapowasilisha hoja Bungeni ya Muswada unaposomwa mara ya pili.  Baada ya mjadala, Bunge hukaa kama Kamati ya Bunge zima ambapo hupitia Muswada kifungu kwa kifungu.
Katika hatua hii Wabunge huweza kupendekeza mabadiliko mahsusi kwenye kila kifungu.  Aidha, Waziri nae anaweza kutetea marekebisho ya Muswada.  Baadaye Bunge hurejea, taarifa ya Kamati ya Bunge zima hutolewa kwamba Muswada umepitiwa kifungu kwa kifungu na kukubaliwa.  Kisha Muswada husomwa mara ya tatu kuashiria kwamba Muswada umepitishwa.  Mara nyingi Muswada hutokana na majadiliano katika hatua hizi zote, mabadiliko hufanywa na wakati mwingine mabadiliko  huwa makubwa kiasi kwamba kufanya  Muswada uliochapishwa na kusomwa mara ya kwanza na ule uliokubaliwa mwishoni uwe tofauti kabisa.
Ndugu Wananchi;
Muswada huu ulisomwa mara ya kwanza mwezi Aprili na kupelekwa kwenye Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala mwezi Aprili, 2011.  Tangu wakati huo Kamati imekuwa ikiufanyia uchunguzi Muswada huo na kukusanya maoni ya wadau.  Walisikiliza wadau Dodoma, Dar es Salaam na Zanzibar pamoja na kufuatilia maoni ya makongamano, magazetini na kwenye mitandao.  Kisha Kamati ikayajadili na kutoa mapendekezo yake ambayo Serikali iliyasikiliza na kuyajumuisha wakati uliposomwa mara ya pili.  Muswada huu haukuwahi kuondolewa Bungeni.  Kwa sababu hiyo, hakuna sababu ya kurudia kusomwa mara ya kwanza kwa mujibu wa taratibu za kuendesha Bunge.  
Tukumbuke kwamba baadhi yao waliahidi kwamba wangetoa Katiba Mpya katika siku mia moja tu.  Serikali imechukua miezi kumi na mmoja na wanalaumu kwamba eti inawahisha mchakato!!  Hiyo Katiba ya siku mia moja sijui wangeipataje bila kuwashirikisha wananchi?
Ndugu Wananchi;
  Ni kutokana na hoja hizo Spika akaamua Muswada uendelee kujadiliwa na Bunge na leo Bunge limeupitisha Muswada huo.  Baadae Muswada utaletwa kwangu kwa ajili ya kutiwa saini uwe Sheria.  Baada ya hapo itabakia kazi yangu na Rais wa Zanzibar kuunda hiyo Tume ili mapema mwakani kazi ya kukusanya maoni ya wananchi ianze.  Lengo letu ni kuwa ifikapo mwaka 2014 zoezi zima liwe limekamilika ili mwaka 2015 tufanye uchaguzi tukiwa na Katiba mpya.  Itapendeza tukisherehekea miaka 50 ya Muungano na Katiba mpya.  Ni matumaini yangu kwamba wananchi wote watashiriki kwa ukamilifu kutoa maoni yao kwa Tume hiyo.

Ndugu Wananchi;
Nimechukua muda wenu mwingi kuyafafanua masuala haya kwa umuhimu wake.  Nia ni kutaka watu waelewe maoni ya upande wa Serikali.  Matatizo ya kiuchumi yanayotukabili tunaendelea kuyashughulikia.  Yale yaliyo kwenye uwezo wetu tutayamaliza na yale yaliyo nje ya uwezo wetu tutaendelea kuchukua hatua za kupunguza makali.  Aidha, tutaendelea kutoa wito kwa mataifa husika kuchukua hatua thabiti kutatua matatizo yao kwani tunaoumia ni wengi.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa mchakato wa kupata Katiba mpya nawasihi Watanzania tujiandae kwa maoni ya kutoa kwenye Tume ya Katiba mara itakapoanza kazi.  Kwa wale ambao hawatapata walichokitaka nawaomba warudi kundini, sote tuungane kwa hatua inayofuata.  Najua wanayo maoni mengi mazuri wayatayarishe na kuyawasilisha kwa Tume itakayoundwa.  Njia ya maandamano na vurugu si ya busara kufuata.  Haijengi bali inabomoa, haina faida bali hasara nyingi, haina faraja bali machungu kwa pande zote.  Busara ituongoze sote kuchagua njia inayojenga, yenye faida, furaha na faraja kwa wote.  Tutofautiane bila kupigana.  Serikali itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa nchi ya amani na utulivu.  
Mwisho
Ndugu Wananchi,
Naomba nimalizie kwa kuwashukuru wananchi kwa kuwa na subira kwa kipindi chote hiki toka tutangaze nia yetu ya kuanza mchakato wa kupata Katiba mpya.  Kwa mara nyingine tena nawaomba mjiandae kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kupata Katiba mpya mara utakapoanza ili tuendelee kuijenga na kuiendeleza nchi yetu na vile vile tuendelee kuithamini na kuitunza amani ya nchi yetu.

Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni sana kwa kunisikiliza!

No comments:

Post a Comment