CCM kwachafuka | Send to a friend |
Monday, 21 November 2011 18:54 |
UVCCM WAPANGA KUASI, NI HOFU YA KUFUTWA KWA UMOJA WAO Neville Meena, Dodoma HALI imezidi kuwa tete ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kundi kubwa la Umoja wa Vijana wa Chama hicho (UVCCM), linadaiwa kupanga mkakati wa kuasi, endapo mkakati unaodaiwa kuandaliwa wa kuuvunjwa umoja huo utafanikiwa.Hatua ya viongozi wa UVCCM kutoka karibu mikoa yote nchini kukusanyika mjini Dodoma kufanya kile walichokiita kuwa ni “kupigania umoja wao na chama chao,” imezidi kuchafua hali ya hewa. Taharuki ndani ya chama hicho tawala imekuja kipindi ambacho vikao vikuu vya chama hicho ambavyo ni Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), vinakutana chini ya mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete. Kamati Kuu ilianza jana saa 8:00 mchana pasipo Rais Kikwete kutoa maelezo yoyote ya ufunguzi. Kilitanguliwa na kikao cha Kamati ya Maadili kilichoanza juzi na kumalizika jana asubuhi, pia kikiongozwa na Kikwete. Juzi usiku, wenyeviti wa UVCCM kutoka mikoa 18 nchini walikutana katika ukumbi wa baa moja maarufu iliyopo eneo la Area D mjini hapa kupanga mikakati jinsi ya kuuokoa umoja wao usivunjwe na hatua za kuchukua iwapo azma hiyo itatekelezwa. Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na baadhi ya washiriki wa kikao hicho zinasema, moja ya maazimio ni kwamba ikiwa UVCCM utavunjwa, basi watahamia vyama vya upinzani, huku wakikitaja Chadema kuwa ni mahali panapowafaa kwa ajili ya kuendeleza harakati za ukombozi wa nchi. Kikao hicho kilichohudhuriwa na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya UVCCM na wale wa Baraza Kuu, kiliweka msimamo wa kutetea kuendelea kuwepo kwake kwa gharama yoyote, hata ikiwa ni kuwafungia ndani wajumbe NEC ya CCM iwapo wataridhia kufanya hivyo. Kauli za viongozi Hata hivyo, mmoja wa wajumbe wa Sekretarieti ya CCM ambaye hakupenda kuandikwa jina gazetini alisema hakuna mpango wa kufuta UVCCM na kuziita taarifa hizo kuwa ni za kupika. Kauli yake iliungwa mkono na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye ambaye alisema: “Hakuna kitu kama hicho, mimi ni mshiriki wa vikao vyote vya Sekretarieti hakuna ajenda hiyo kwenye vikao vyetu hivi.” “Ndiyo maana kwenye mkutano na waandishi wa habari nimesema kwamba watu waache kupandikiza vitu ambavyo kimsingi havipo, vikao hivi ni vya kawaida na ajenda zimewekwa wazi, sasa kama kuna watu wanaleta hizi hoja, basi wana malengo yao tu.” Mapema Nape akizumgunza na waandishi wa habari alisema kumekuwapo na taarifa nyingi zinazowafanya Watanzania kutaharuki kana kwamba kuna vita inayotarajiwa kutokea mjini hapa. “Naomba wanahabari wenzangu, nisaidieni maana haya yote yanatokana na taarifa zinazoandikwa kwenye magazeti na vyombo vingine vya habari, lakini ajenda zetu kama nilivyosema jana (juzi) zinafahamika, kubwa ni kupitia utekelezaji wa mabadiliko ndani ya chama chetu,” alisema Nape. Naye Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela alisema hana taarifa zozote kuhusu kuwepo kwa mpango wa kufutwa kwa umoja huo ambao yeye ni mtendaji wake mkuu na kwamba hata katika kikao cha sekretarieti ambacho yeye ni mjumbe hakukuwa na ajenda ya aina hiyo. Hata hivyo, Shigela hakuwa tayari kuweka bayana iwapo alifahamu mkusanyiko wa viongozi wa UVCCM kutoka mikoani waliopo Dodoma, zaidi ya kusisitiza kwamba kipindi hiki ni cha kutulia kwa wana CCM kutokana na kuwepo kwa taarifa nyingine ambazo wakati mwingine vyanzo vyake si bayana. Chimbuko la hisia Chimbuko la hisia za kufutwa kwa UVCCM ni taarifa zisizo rasmi kutoka ndani ya vikao vya Kamati ya Maadili ambayo katika siku yake ya kwanza iliwahoji baadhi ya viongozi wake akiwamo Kaimu Mwenyekiti, Benno Malisa. Wengi walihojiwa kuhusu utendaji wa kamati ya kutathmini upya uendeshaji wa UVCCM, ambayo tayari imefanya kazi yake katika mikoa 19 ya Tanzania Bara. Kamati hiyo inayoongozwa na Mjumbe wa Baraza Kuu ya UVCCM, Hussein Bashe, inatuhumiwa kuendesha mikutano iliyotumika kuwakashifu viongozi wa juu wa CCM wakiwamo Mwenyekiti Kikwete na Katibu Mkuu, Wilson Mukama. “Kuna taarifa za uhakika kwamba ajenda hii haikupitia kwenye sekretarieti, inatoka kwenye kamati ya maadili kwa tuhuma kwamba eti sehemu kubwa ya UVCCM tuko nyuma ya kundi moja ndani ya chama,” alisema mmoja wa wenyeviti wa umoja huo na kuongeza: “Sasa mpango wao ni kufuta viongozi wote wa kuchaguliwa na baada ya hapo waandae uchaguzi mwingine ili kuwaweka viongozi wanaowataka, sasa hili sisi tunasema hapana kama ni tatizo litatuliwe lakini wasituulie umoja.” Mmoja wa maofisa wa CCM makao makuu alisema jana kuwa taarifa kwamba UVCCM inafutwa zimezagaa katika ofisi hizo lakini bado zilikuwa hazijathibitishwa kutokana uamuzi wa vikao vya Kamati ya Maadili kufanywa kwa siri kubwa. Mkakati wa Kupinga Taarifa za mpango huo ndizo zilizowatia wazimu UVCCM kiasi cha kuitana Dodoma kwa lengo la kukabiliana na NEC ikiwa ‘itathubutu’ kuubariki. Habari kutoka ndani ya kikao cha juzi usiku zinasema wenyeviti hao walikubaliana kwa kauli moja kuwaita wenyeviti wa wilaya wa umoja huo wa vijana ili kuongeza nguvu za kuwakabili wakuu wa CCM. Mmoja wa wenyeviti kutoka mikoa ya Kanda ya Mashariki alisema juzi usiku kwamba: “Katika hili tumejipanga, tunao vijana zaidi ya 300 wapo kambini, tutawaleta hapa, tutaungana nao kupinga uamuzi huu.” Harakati za UVCCM zinakwenda sambamba na kupinga utekelezaji wa mpango wa kujivua gamba ambao wanasema unatekelezwa kwa upendeleo ukiwalenga baadhi tu ya watu. Mmoja wa viongozi hao alinukuliwa na chanzo chetu akisema wanaopaswa kufukuzwa au kuchukuliwa kwa hatua na CCM ni makada ambako Rais Kikwete alipata kura chache wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka jana. Kwa mantiki hiyo, vijana hao walisema mpango wa kujivua gamba hauna tija kwa sasa kwani unakigawa chama na kwamba CCM kina matatizo makubwa zaidi kinayopaswa kushughulikia badala na siyo kuchochea chuki miongoni mwa wanachama wake. Maazimio ya NEC NEC inakutana miezi minne tangu kilipokutana mara ya mwisho na kutoa maazimio ambayo yalisababisha mmoja wa makada wake, Rostam Aziz kujiuzulu ubunge katika Jimbo la Igunga pamoja na ujumbe wa NEC. Rostam katika kujiuzulu huko aliitupia lawama sekretarieti ya chama hicho kwa kile alichokiita kuwa ni kuendesha siasa chafu dhidi yake na kuwataja kwa majina Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Tanzania Bara, John Chiligati na Nape kuwa wahusika. Kujiuzulu kwa Rostam ni miongoni mwa mambo ambayo yanatarajiwa kuchukua nafasi katika mjadala wa CC na NEC. Katika mazingira hayo, kuna kila uwezekano wa kutathmini jinsi falsafa ya kujivua gamba ilivyotekelezwa. Kuna madai kwamba Sekretarieti inayoongozwa na Mukama nayo imegawanyika katika suala la utekelezaji wa uamuzi wa NEC, hali inayoongeza sintofahamu ndani ya chama hicho. |
No comments:
Post a Comment