RAIS Jakaya Kikwete amewasilisha taarifa ya Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Tanzania kwa umma.
Wakati akiwasilisha taarifa hiyo alisema, Tanzania ni miongoni mwa nchi 20 duniani ambazo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa.
Rais Kikwete alisema kwa hali ya uchumi, kwa maana ya viashiria vya uchumi jumla, Tanzania iko mahali pazuri licha ya nchi kukumbwa na athari za msukosuko wa uchumi duniani katika mwaka wa 2008/2009, ukuaji wa uchumi ni mzuri.
“Kwa wastani wa asilimia saba tangu mwaka 2001 hadi 2010, Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi 20 duniani ambazo uchumi wake unakua kwa kasi.
Katika kipindi hicho, pia mfumuko wa bei umekuwa wastani wa chini wa kiwango cha asilimia 10 licha ya kuyumba mwaka 2009 kutokana na matatizo ya bei za mafuta na chakula duniani kwa ujumla,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete aliwasilisha taarifa ya mpango huo wa miaka mitano wa kuanzia 2011/2012 – 2015/2016, wakati akizungumza na Taifa kutoka kwenye Ukumbi wa St Gaspar mjini hapa, akishuhudiwa na viongozi mbalimbali wa Kitaifa, wabunge, mabalozi na wananchi kupitia televisheni.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi; Waziri Mkuu Mizengo Pinda; Spika wa Bunge, Anne Makinda, wakuu wa vyombo vya Dola, wabunge, mabalozi kadhaa, ni miongoni mwa walioshiriki katika hafla hiyo iliyoandaliwa na Tume ya Mipango katika Ofisi ya Rais.
Rais Kikwete alisema makusanyo ya mapato ya ndani yameongezeka sana kwa wastani wa Sh bilioni 84.7 kwa mwezi kwa mwaka 2001/2002 hadi Sh bilioni 430 kwa mwezi katika kipindi cha Julai mwaka 2010 hadi Aprili mwaka huu.
“Makusanyo mazuri ya mapato ya ndani yametuwezesha kuongeza uwezo wa bajeti ya Serikali kutoka Sh 1.76 trilioni mwaka 2001/2002 hadi Sh trilioni 11.6 mwaka 2010/2011.
Mauzo yetu ya nje yamefikia dola za Marekani milioni 5,876.5 mwaka 2010 na akiba yetu ya fedha za kigeni ni dola za Kimarekani milioni 3.948.0 sawa na mahitaji ya kuagiza bidhaa na huduma kwa miezi sita mwaka 2010,” alieleza Rais Kikwete na kushangiliwa na waliohudhuria hafla hiyo.
Rais Kikwete alisema makusudio makuu ya Serikali katika mpango huo ni kuona kwamba, kwanza; vikwazo vya ukuaji wa uchumi vilivyopo vinatanzuliwa; pili; kujenga uwezo wa nchi wa kukuza uchumi wake na kuondoa umasikini haraka; tatu; kujizatiti katika kutumia kwa ufanisi na kimkakati fursa mbalimbali zilizoibuka nchini na katika mahusiano ya kiuchumi kikanda na kimataifa.
Pia alisema kusudio la nne, ajira ziongezeke kwa wingi zaidi ili kupunguza tatizo kubwa la ajira linalowakabili vijana na kuongeza kuwa dhana kubwa iliyobebwa na Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa ni “Kufungulia Fursa Tulizonazo za Kukuza Uchumi wa Taifa.”
Alisema Mpango huo umejengeka juu ya nguzo kuu nne za kimkakati ambazo ni kuendeleza uchumi wa jumla na kuimarisha mafanikio yaliyopatikana hadi sasa na kutumia rasilimali zetu kama fursa ya kukuza uchumi; huku kipaumbele maalumu kitawekwa katika kuleta mapinduzi ya kilimo, ufugaji na uvuvi na uendelezaji wa viwanda kwa kutumia malighafi na rasilimali zetu.
Aidha, Rais Kikwete aliyataja maeneo ya vipaumbele vya mpango kuwa ni kilimo, miundombinu, viwanda, utalii, rasilimaliwatu na kuendeleza matumizi ya Sayansi na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
Alisema Mpango huo una malengo kwa kila kipengele, ikiwamo uchumi wa Taifa unatakiwa kukua kwa asilimia 8 hadi 10 kwa mwaka; mfumuko wa bei udhibitiwe chini ya kiwango cha asilimia 5; thamani ya mauzo ya nje ikue kufikia asilimia 23 ya Pato la Taifa; ukusanyaji wa mapato ya ndani ufikie asilimia 19 ya Pato la Taifa na kipato cha mwananchi kiongezeke hadi kufikia wastani wa dola za Marekani 650.
Kuhusu gharama za utekelezaji wa mpango huo, Rais Kikwete alisema utagharimu jumla ya Sh trilioni 42.5 kwa kipindi cha miaka mitano ikiwa ni wastani wa Sh trilioni 8.5 kwa kila mwaka .
No comments:
Post a Comment