BURIANI DR. REMMY
yangu, kwa hakika mimi ni mzima na naendelea vizuri kuwapasha mengi yanayohusu muziki wetu wa zamani.
Leo nianze na kushukuru wa wasomaji wengi kunitumia ujumbe ukiwa na hili au lile, ilimradi wenye dira ya kuberesha safu yetu hii. Kwa walioshiriki kunitumia ujumbe na hata kunipigia simu nawashukuru kwa dhati kabisa kutoka moyoni.
Lakini kati yetu leo nimalize kiu ya msomaji wetu Ibrahim Vuai, aliyejitambulisha kwamba anaishi Vuoni kisiwani Zanzibar. Yeye alituma ujumbe akilaani tabia ya wanamuziki kuhamahapa kutoka bendi moja kwenda nyingine, akisema kwamba hiyo ni moja ya vigezo vilivyodumaza muziki wa Tanzania.
Kwa kweli akawataja wengi tangu miaka ile ya 1960 mpaka akaja hivi karibuni akalikumbushia tukio la bendi mbili za African Stars ‘Twanga Pepeta’ na Extra Bongo Next Level kuchukuliana wanamuziki.
Huko sikutaka kuingia sana, ila kubwa jingine ni pale alipowataka wanamuziki waige mfano wa
aliyekuwa kiongozi wa bendi ya Super Matimila Dk Remmy Ongala ambaye alimtaja kuwa ni mwanamuzikji aliyetulia, kwani alipotoka Makassy na kujiunga Orchestra Matimila basi hakutoka hadi umauti ulivyompata mwishoni mwa mwaka jana.
Hapa kidogo ndipo kwenye masahihisho yaliyonifanya niandike makala hii, kwa vile zipo kumbukumbu za kimuziki zinazoonesha kwamba licha ya uvumilivu wa muda mrefu Dk Remmy akiwa na bendi ya Super Matimila lakini aliwahi kuhama.
Ikumbukwe mwaka 1985 mwimbaji huyo alitangazwa kuikimbia bendi ya Matimila, na alipohojiwa na vyombovya habari alikiri kuiacha bendi hiyo na kurejea bendi ya Orchestra
Makassy.
Ndicho kipindi hicho alichotunga wimbo Narudi Nyumbani, lakini ndani yake kulikuwa na maneno siyo yale yaliyorekodiwa baadaye Wimbo huo ulikuwa ukisema "Narudi kwa mjomba" ikiwa na maana anarejea kwenye bendi ya mjomba wake Mzee Makassy ambaye ilielezwa miaka hiyo kuwa wana undugu fulani.
Hata katika msiba wa mwanamuziki huyo mtu aliyeitwa Kiteguru Makassy ndiye huo aliyekuwa mmiliki wa bendi ya Makassy na ndiye aliyekuwa msmemaji wa familia. Kilitokea nini wakati huo?
Labda watu wengi na hasa wale wasiojua historia hii watakuwa wakijiuliza kilichojitokeza kwenye bendi ya Matimila ambayo yeye alikwa akiiongoza tangu alipoachiwa kijiti na aliyekuwa mpiga solo hatari wa bendi hiyo Mosese Fanfan ambaye naye alitokea Orchestra Makassy.
Baada ya kuwa kiongozi wa muda refu na pia kuweza kutunga nyimbo nyingi ndani ya kundi hilo ilitokea wakati umuliki wa bendi hiyo ulihitaji kuiweka bendi kwenye utawala kwa idara maalum.
Kama vile idara ya fedha na masuala mengine yawe nje ya kiongozi mkuu Dk Remmy ili kumpa nafasi yeye afanye vizuri kazi yake ya muziki.
Labda tukio hilo na mengine ambayo hayakufahamika kirahisi yalimfanya mwimbaji huyo kutangaza kuikimbia bendi hiyo na kweli alipokewa kwa shangwe kwenye bendi yake ya zamani aliyopata kutamba nayo na nyimbo kama Siku ya Kufa, Harusi ya Mwanza, Namolema, Athumani Valuvalu, Sisca na Mosese.
Hatimaye mzee mwenyewe Makassy akasimma jukwaani na kuimba pamoja na Dk Remmy na pia walifanikiwa kurekodi wimbo mmoja uitwao Shida za Dunia.
Baadhi ya mashairi ya wimbo wa Dk Remmy alioimba na Mzee Makassy baada ya kurejea bendi ni haya:- Kweli nasikitika mtoto anapozaliwa anakuta shida nyingi za duniani, njaa kali, magonjwa mengi,shurua kuhara homa kali"
Hata hivyo katika bendi ya Matimila ilikohesabiwa na wapenzi wa muziki kwamba kutakuwa na pengo, nako kulichangamka kiasi chake. wanza kitu kilichowashangaza wapenzi wengi ni kuwepo kwa sauti ya Dk Remmy licha ya yeye mwenyewe kutokuwepo kwenye bendi hiyo.
Sauti hiyo ilikuwa na mwimbaji anayeitwa Bink Wabinsalunjivu, ambaye pia uvaaji wake wa kofia alishabihiana na Dk Remmy licha ya kumudu sauti yake. Vilevile alikuwepo mwimbaji
mwingine Nkhulu Wabangoie aliyejiunga na bendi hiyo akitokea Orchestra Marquiz Du Zaire.
Kipindi hicho Binki aliibuka na kibao kiitwacho Roda Binti Rashid, na Talakaka Changamka, ambapo Wabangoie alikuja na wimbo wa Sifa za Mage.
Kwa kuwepo na 'vichwa' hivyo na vilevile kuimarika kwa ukumbi wa Wami Bar iliwawezesha wapenzi wa Matimila kuendelea kuingia kwenye kumbi wanazofanya maonesho kwa vile kulikuwa na mabadiliko fulani ya muziki.
Kwani licha ya waimbaji hao kubuni mbinu mpya lakini pia aliyekuwa mpiga solo wa bendi
hiyo Batii Osenga Lipopolipo aliweza kuchangamsha mkono na hivyo kujikuta wakipiga mtindo
mpya wa Talakaka Changamka.
Hata hivyo Dk Remmy alikuwa yari amejawa na mapenzi ya bendi ya Orchestra Matimila kwani hata kabla ya miezi mitatu akatangaza kurejea Matimila na safari hii akiubadilisha wimbo uliokuwa ukiimbwa Narudi kwa Mjomba sasa ukawa Narudi Nyumbani Matimila.
Aliporejea mwimbaji Binki aliacha bendi hiyo na kwenda kuanzisha bendi ya Salna Brothers
akiwa na mwimbaji mwingine Kapelembe Kokoo ambao waliisuka bendi hiyo hadi kunyakuwa ubingwa wa pili wimbo wa taifa kufuatia kibao chao kiitwacho Ufitina, wakati washindi wa kwanza walikuwa ni Mk Group kufuatia wimbo wao Utakuja Kuanguka Kwenye Matope.
Dk Remmy naye aliifanyia ukarabati mkubwa bendi ya Matimila kwa kuwakaribisha wanamuziki wengine kama vile wapiga solo wengine Christopher Kasongo aliyepiga wimbo wa Mariam Wangu na Cobra Wabilumbu.
Hapo ndipo alipoibuka na vibao kama Mariam wangu, Mwanza Mji Mzuri na nyimbo nyingine kadhaa, Kwa hiyo zipo kumbukumbu kuwa Dk Remmy alitoka Matimila wakati fulani na kurejea Makassy lakini baadaye akarejea kwenye bendi hiyo hadi alipofariki.
No comments:
Post a Comment