Mbowe huru, polisi watumia ndege ya JWTZ | Send to a friend |
Monday, 06 June 2011 21:17 |
0diggsdigg Waandishi Wetu.MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe jana aliachiwa kwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, baada ya kusomewa mashtaka ya kutotii amri halali ya kuhudhuria mahakamani katika kesi inayomkabili ya kufanya mkusanyiko wa watu bila ya kibali na vitendo vya uchochezi.Aidha, mahakama hiyo imemkataa mdhamini wake wa awali, Julius Margwe baada ya kuwa na shaka na mwenendo wake. Diwani wa Kata ya Elerai (Chadema), John Bayo alijitokeza na kuwa mdhamini mpya wa Mbowe. Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Charles Magesa alisema mdhamini huyo amekataliwa kutokana na kukiuka masharti ya kuhudhuria mahakamani hapo pamoja na kukabiliwa na kesi katika Mahakama ya Mwanzo Maromboso hivyo, kuamua kutoa nafasi kwa mdhamini mwingine. Juzi, Mbowe alisafirishwa chini ya ulinzi hadi Arusha akitokea Dar es Salaam baada ya kukamatwa na polisi. Akizungumzia safari hiyo, Mbowe alidai kuwa alipelekwa kwa ndege ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) usiku wa manane huku akisindikizwa kwa magari manne ya askari wa kutuliza ghasia, kuanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) hadi mahakamani hapo huku akilalamikia hali hiyo na kusema ni matumizi makubwa ya fedha na rasilimali za umma. "Wamenisafirisha kuja Arusha kwa ndege ya JWTZ kama mtuhumiwa wa ujambazi. Haya ni matumizi makubwa ya fedha na rasilimali za umma. Ile ndege ina uwezo wa kubeba zaidi ya watu 100, wametuleta watu watatu, mimi kama mtuhumiwa, Kamishna mmoja wa polisi Wilaya ya Ilala na Kamishna wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU)," alidai Mbowe. Hata hivyo, JWTZ limekanusha likisema halikuwajibika na tukio hilo la kumsafirisha huku polisi nayo ikimtaka Mbowe asijitafutie umaarufu wa kisiasa kwa mgongo wa suala hilo. Mbowe alifikishwa mahakamani mjini Arusha jana saa moja asubuhi akiwa chini ya ulinzi mkali. Alikuwa katika gari la polisi aina ya Toyota Land Cruiser VX, lililokuwa likisindikizwa na magari mengine manne ya FFU. Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuachiwa kwa dhamana, Mbowe alisema hajutii kuwekwa mahabusu na kusafirishwa hadi Arusha.Pia alisema kukamatwa kwake na kuwekwa mahabusu kamwe hakutasitisha harakati za Chadema kudai haki na demokrasia ya kweli ndani na nje ya Bunge.Alisema alipokuwa katika mahabusu katika Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam, hakuteswa na polisi wala kupigwa lakini alikuwa chini ya ulinzi hadi alipofikishwa Arusha jana alfajiri. Kukamatwa kwake mwishoni mwa wiki kulichafua hali ya hewa ya kisiasa baada ya juzi, mamia ya mashabiki wa Chadema kupiga kambi Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, wakishinikiza mwenyekiti wao aachiwe huru kabla ya kupelekwa mahakamani Arusha. Baadaye, juzi saa 7:00 usiku vyanzo huru vilidokeza kwamba Mbowe alisafirishwa kwa ndege hiyo ya JWTZ akiwa na maofisa waandamizi wa polisi kutoka Dar es Salaam na wanajeshi watatu. Kauli ya JWTZ Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe alisema hadi jana mchana hakuwa na taarifa zozote kuhusu jeshi kuwajibika katika suala hilo. Alisema hilo lilikuwa suala la polisi na mahakama huku akisisitiza kuwa hajaona nafasi ya JWTZ katika mchakato huo. "Ndiyo kwanza unaniambia wewe (mwandishi) kuhusu JWTZ kutumia ndege yake kumsafifirisha huyo mtu. Ninachoweza kukwambia hakuna kitu kama hicho na jeshi halikuwajibika kwa lolote," alisisitiza Mgawe na kuongeza: "Tukio hilo linawahusu polisi na mahakama wao ndiyo wanaojua na ndiyo waliopaswa kuwajibika siyo jeshi. Kwa hiyo kama una vyanzo vyako vingine sijui sisi tunasema hakuna kitu kama hicho.'' Mahakamani Arusha Baada ya kufikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka na kisha kuchiwa kwa dhamana, wafuasi wake waliokuwa wamefurika mahakamani hapo, walishangilia na kumbeba juu kwa furaha. Kabla ya kuachiwa kwa dhamana Hakimu Magesa alisema mdhamini wa awali wa Mbunge huyo wa Hai, Margwe amekataliwa kwa sababu mbali na kuieleza uongo mahakama kuwa alikuwa akifika mahakamani hapo, haina sababu ya kuendelea naye kwani tayari ana kesi ya jinai ambayo hatima yake haifahamiki.Kuhusu Mbowe hakimu huyo alikiri kwamba mahakama iliruhusu washtakiwa wabunge kuhudhuria kikao cha Bunge la Bajeti , lakini kutokana na kukosekana kwa mdhamini wake, ndiyo sababu walitoa amri kwamba akamatwe. “Ila sasa mkaendelee na vikao vyenu vya Bunge kama tulivyosema awali, lakini wadhamini wenu lazima waje mahakamani kila kesi itakapotajwa na tunaondoa amri ya kukamatwa na sasa utaendelea na dhamana yako ya awali,” alisema Magesa. Kabla ya hakimu huyo kutoa uamuzi huo, alimpa nafasi Margwe ya kueleza sababu za kutofika mahakamani. Margwe alisema Mei 27, mwaka huu hakufika kwa sababu alikuwa na kesi Mahakama ya Mwanzo Maromboso na Mei 30 alifika mahakamani lakini kwa sababu hakupewa nafasi ya kusema lolote, hakujitokeza. Wakili upande wa utetezi, Method Kimomogoro aliiomba mahakama hiyo, kuondoa amri ya kukamatwa kwa mteja wake na kutaka apewe dhamana yake ya awali ili aweze kuhudhuria vikao vya Bunge la Bajeti ambalo yeye ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani. Alimtetea mdhamini huyo kwa kutofika mahakamani na kusema kuwa hiyo ipo kwa kila mtu hata kwa mawakili akisema huwa wanasahau tarehe za mahakama na ndiyo sababu huziandika, hivyo kwa mwananchi wa kawaida ni lazima atasahahu tarehe hizo. Wakili wa Serikali, Juma Ramadhani aliiomba mahakama hiyo itoe onyo kali kwa mshtakiwa kwa kutofika mahakamani hapo mara anapohitajika na pia kumtaka yeye na wenzake wawe na mawasiliano ya karibu na wadhamini wao ili wasikose kufika mahakamani hapo. “Mnajua hii ni kesi ya jinai, lazima muwepo mahakamani na mkikosa lazima wadhamini wawepo ili kuondoa utata, ila hofu tuliyo nayo ni pale tutakaposubiri kikao cha Bunge kiishe ndipo washtakiwa waje mahakamani ni muda mrefu sana, hivyo naomba wakili wa utetezi awasiliane na washtakiwa kupata siku ya nafasi ili kuanza kutoa maelezo ya awali,” alisema Juma.Alisema hana shaka juu ya dhamana ya Mbowe isipokuwa mdhamini wake akisema hajui anachokifanya na kusema hafai kuwa mdhamini. Aliiomba mahakama kutoa uamuzi juu ya mdhamini huyo. Hata hivyo, Wakili Kimomogoro alipinga hoja ya kutaka mahakama impe onyo Mbowe kwa sababu kosa lililojitokeza halikuwa ka kwake na kwamba Mahakama ilimpa udhuru Aprili 29, mwaka huu kesi hiyo ilipotajwa na kutoa sababu kwamba watakuwa katika vikao vya Bunge la Bajeti hivyo kuiomba mahakama imrejeshee dhamana yake ya awali. Baadaye Hakimu Magesa alitoa uamuzi wa kumwachia Mbowe kwa dhamana ili aendelee na vikao vya Bunge la Bajeti hadi hapo Juni 24 mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa tena. Hata hivyo, Mbowe na wabunge wenzake wanaohusika na kesi hiyo, hawatakuwapo mahakamani katika tarehe hiyo. Akizungumza na waandishi wa habari na wafuasi waliofurika mahakamani hapo mara baada ya kuachiwa, Mbowe alisema hakuwa na kosa la kukamatwa na ndiyo sababu mahakama haikumhoji hata swali moja. “Ila mimi naheshimu mahakama, lakini sitakosa kusema pale wanapokosea kama vile baadhi ya watumishi wa mahakama wanakubali kupewa amri na viongozi wa serikalini ili mradi tu kutimiza matakwa yao,” alisema Mbowe. Alisema hakukuwa na sababu za msingi za kutumia rasilimali za Serikali ambayo ni mali za umma na kumsindikiza kama mhalifu ilihali hakuwa hata na silaha moja.Alisema anashukuru kwamba polisi hawakumfanyia vitendo vyovyote vibaya isipokuwa walimnyima haki yake ya msingi ya kuwa na uhuru wa kuwasiliana na watu. Wafuasi Chadema wasitisha shughuli za mahakama Mamia ya wafuasi wa Chadema waliokuwa wamefurika katika Viwanja vya Mahakama hiyo walisababisha kusitishwa kwa muda kesi nyingine kutokana na eneo hilo kutawaliwa na kelele. Kesi nyingine ziliendelea kusikilizwa saa 5:00. Wafuasi hao wa Chadema bila kujali eneo hilo la mahakama, walikuwa wakipiga kelele za 'peoples power' na baada ya Mbowe kuachiwa walianza kuimba: “Wamebana wameachia, wamebana wameachia,” huku wakimbeba kiongozi huyo juu juu. Mamia ya watu walizuiwa kuingia ndani ya Mahakama hiyo huku polisi wakiwa wametanda kudhibiti uvunjifu wa amani.Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema mara kadhaa alikuwa akitoka nje ya Ukumbi wa Mahakama kuwaeleza wafuasi wa chama hicho kilichokuwa kikiendelea ndani huku akiwahimiza kutokatishwa tamaa katika kudai haki yao. Lema alisema kukamatwa kwa Mbowe ni ishara ya ushindi wa chama hicho kuchukua dola miaka ijayo. "Msihofu hata kina Mandela waliteseka hivi hivi, lakini baadaye walikamata dola na chama. Tutaongoza nchi hii miaka michache ijayo, hawa polisi watakuwa wakitulinda sisi badala ya kutukamata kamata," alisema Lema. Maoni ya wananchi Baadhi ya wakazi wa Arusha wameelezea kushangazwa kwao na matumizi makubwa ya fedha za umma katika kumkamata Mbowe na kumfikisha Arusha kisha kuachiwa kwa dhamana. Mmoja wa wakazi hao, George Kavishe alisema kitendo cha kujisalimisha Dar es Salaam na kisha kusafirishwa kwa ndege ya jeshi na kusindikizwa kwa magari ya Serikali ni matumizi mabaya ya fedha za umma. "Sasa kama walijua akifika hapa atapewa dhamana tu kwa nini wasingemalizia Dar es Salaam suala hili? Ni jambo la ajabu," alisema Kavishe ambaye ni mfanyabiashara. Mkazi mwingine Lucas Kaaya, alisema hatua ya polisi kumfikisha Mbowe mahakamani akiwa chini ya ulinzi imedhihirisha kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria. "Ingekuwa sisi watu wa chini, leo hapa dhamana isingetoka tena tungepewa siku 14 za kukaa magereza sasa hili ni funzo tuheshimu vyombo vya sheria kwani hakuna amani bila haki," alisema Kaaya. Polisi wadhibiti maandamano kwa amani Polisi jana, walifanikiwa kuzima maandamano ya wafuasi wa Chadema ambao walikuwa wamejiandaa kufanya hivyo wakiwa wamebeba majani wakiashiria amani. Viongozi wa jeshi hilo walifanya mazungumzo na Mbowe na viongozi wa Chadema mkoani Arusha na kuwasihi waondoke mahakamani kwa magari yao, ili kuzuia maandamano yasiyo na kibali. Baada ya kukubaliana, Lema aliamua kuondoka mahakamani hapo kwa pikipiki aina ya Toyo na wafuasi wachache, hasa vijana walianza kumfuata nyuma lakini walipofika makutano ya Barabara ya Nyerere walitawanywa na polisi. Polisi:Mbowe hakuonewa Akizungumzia kitendo cha Jeshi hilo kumkamata Mbowe, Kamishna wa Operesheni wa Polisi, Paul Chagonja alisema kuwa kiongozi huyo alikamatwa kama ilivyo kwa watu wengine na hakuonewa inavyodhaniwa na baadhi ya watu. Aliwataka Watanzania kutokubali kutumiwa na wanasiasa wanaotaka umaarufu kwa nguvu kwa kulazimisha kufanya maandamano kinyume na sheria. Chagonja aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuwa, kiongozi anayetaka kuingia madarakani kwa mtindo wa kushawishi wananchi kufanya maandamano si mzuri. “Wapo viongozi wa kisiasa wanaotumia wananchi kujipatia umaarufu. Nawaonya wananchi wakumbuke kwamba yatakayowapata ni hasara kwa familia zao, kwa nini ukubali kushinikizwa na mtu mwenye lengo la umaarufu na wewe unakubali?” “Alikamatwa baada ya kushindwa kutii amri ya mahakama ni utovu wake wa nidhamu na sheria iko wazi kwamba kama mtu hajafika mahakamani bila sababu za msingi hati ya kukamatwa inatolewa. Kama kuna ugomvi, Chadema ingeilalamikia mahakama si Jeshi la Polisi.” “Nchi hii ni ya amani, mtu yeyote atakayeleta uchokozi hatutamuonea aibu, hatuwezi kukubali kumnyamazia mtu wa namna hii, kama anachimba shimo basi atumbukie mwenyewe,” alisema Changonja na kuongeza:“Mbunge akitoka nje ya Ukumbi wa Bunge atapigwa pingu tu, maneno yanayosemwa kuwa mbunge ana kinga ni ya kutapatapa tu.” Kaimu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Peter Kivuyo alisema katika mafunzo ya jeshi hilo kuna aina moja tu ya kumkamata raia: “Ili kumkamata Rais wa nchi kuna taratibu zake, lakini watu wengine wanakamatwa kwa mujibu wa sheria zilizopo.” Katika hatua nyingine, Jeshi hilo Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, linawashikilia watu watatu wakiwamo wanafunzi wawili wa vyuo kwa tuhuma za kufanya fujo na maandamao, huku wakiwa na mabango yenye ujumbe unaochochea nchi kuingia katika machafuko ya umwagaji wa damu. Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema waliokamatwa ni pamoja na mwanafunzi mmoja wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) ambaye ni mkazi wa Kijitonyama na mwanafunzi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) anayeishi katika Hosteli za Mabibo pamoja na mkazi mwingine wa Tegeta. Kova alisema kukamatwa kwa watu hao kunatokana na vurugu zilizojitokeza baada ya Mbowe kukamatwa na jeshi hilo kwa kukaidi agizo la mahakama. Kova alisema kumejitokeza tabia ya baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa kuwachochea vijana kuingia mitaani kufanya fujo kwa madai ya kuwa wanadai haki yao kikatiba. “Jeshi la polisi haliko tayari kuvumilia tabia hii na tutatoa adhabu kali kwa yeyote atakayehusika kuwahamasisha au kuwachochea vijana kuleta machafuko. Kama fujo za jana (juzi) zilizochochewa na viongozi wa ngazi za juu wa vyama vya siasa kuhamasisha vijana kuingia mitani wakiwa wamevaa fulana pamoja na kubeba mabango yenye ujumbe unaochochea nchini kuingia katika machafuko ya umwagaji damu,” alisema. Habari hii imeandaliwa na Mussa Juma na Moses Mashalla, (Arusha); Ramadhan Semtawa, Fidelis Butahe, Hadija Jumanne na Aziza Masoud (Dar) |
No comments:
Post a Comment