Bajeti ijayo haiitambui mikoa mipya | Send to a friend |
Sunday, 05 June 2011 21:34 |
0diggsdigg Boniface MeenaBAJETI inayotarajiwa kusomwa bungeni Juni 8, mwaka huu inaonyesha kuwa mikoa mipya iliyoanzishwa haijatengewa fedha za kuiendesha kwa mwaka wa fedha ujao. Mikoa hiyo mipya ni Njombe, Simiyu na Geita ambayo kusudio la kuanzishwa kwake lilitangazwa bungeni mjini Dodoma mwaka jana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipokuwa akihitimisha Hotuba ya Makadirio ya Bajeti kwa ofisi yake. Kwa mujibu wa mapendekezo yaliyowasilishwa katika Kamati ya Bunge ya Katiba Sheria na Utawala, mikoa iliyotajwa katika Bajeti ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), mikoa iliyotengewa mafungu ni 21 tu. Kati ya mikoa hiyo, Dar es Salaam unaongoza kwa kuwa na bajeti kubwa ya Sh 213.8 bilioni huku Lindi ukishika mkia kwa kuwa na bajeti ndogo ya Sh 56.0 bilioni.Mbali ya Dar es Salaam mingine iliyotengewa fedha nyingi ni Mwanza (Sh175.6 bilioni), Mbeya (Sh163.4 bilioni), Shinyanga (Sh141.3 bilioni) na Kilimanjaro wenye Sh138.0 bilioni. Mikoa inayoungana na Lindi kwa kutengewa bajeti ndogo ni Rukwa Sh63.9 bilioni, Singida Sh63.8 bilioni, Mtwara Sh78.2 bilioni na Kigoma Sh72.3 bilioni. Bajeti kwa mikoa yote hiyo 21 ya Tanzania Bara ni kiasi cha Sh2.3 trilioni. Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo alipoulizwa kuhusu suala la mikoa hiyo mipya kutotengewa bajeti alisema kuwa waziri anayeweza kuzungumzia suala hilo ni George Mkuchika wa (Tamisemi): "Mwulize Mkuchinka ndiye waziri ambaye ataweza kukueleza kuhusu hilo." hata hivyo, jitihada za kumpata Mkuchika kutoa ufafanuzi zilikwama.Kamati ya Bunge ilipitisha mapendekezo ya bajeti hiyo ya Tamisemi na kuitaka kutoa kipaumbele katika miradi ya maendeleo kwenye halmashauri zote nchini. Mkuchika aliiambia kamati hiyo kuwa kati ya fedha hizo, Sh2.3 trilioni zitatumika kwa ajili ya matumizi ya kawaida na zilizobaki zitatumika kulipa mishahara watumishi wake.Alisema kutokana na hali hiyo halmashauri nchini zitasimamia miradi yake na kuongeza mapato ambayo yatatumika kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo. MIKOA MIPYA ILIYOANZISHWA (i) Mkoa wa Njombe. Huu umezaliwa baada ya kumegwa na kuunganishwa kwa Wilaya za Njombe, Ludewa na Makete kutoka Mkoa wa Iringa. Mkoa huu utakuwa na wilaya mpya ya Wanging’ombe ambayo inatokana na kugawanywa kwa Wilaya ya Njombe. (ii) Mkoa wa Geita. Huu unatokana na kumega na kuunganisha Wilaya za Geita kutoka Mkoa wa Mwanza, Bukombe kutoka Mkoa wa Shinyanga na Chato kutoka Mkoa wa Kagera. Mkoa huu utakuwa na Wilaya mpya ya Nyang’hwale ambayo inatokana na kugawanywa kwa Wilaya ya Geita. (iii) Mkoa wa Simiyu. Unatokana na kumega na kuunganisha Wilaya za Bariadi kutoka Mkoa wa Shinyanga, Maswa kutoka Mkoa wa Shinyanga, Meatu kutoka Mkoa wa Shinyanga na Wilaya mpya ya Busega kutoka Mkoa wa Mwanza. Mkoa huu utakuwa na Wilaya nyingine mpya ya Itilima ambayo inatokana na kugawanywa kwa Wilaya ya Bariadi. MADHUMUNI YA KUANZISHWA MIKOA MIPYA Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaelekeza kuwa, kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Serikali, Rais anaweza kuigawa nchi katika mikoa au Wwlaya. Hivyo, madhumuni ya kuanzishwa kwa mikoa hiyo ni kuboresha utendaji wa serikali kuu kwa kupunguza ukubwa wa maeneo ya mikoa mama ili wananchi wapate huduma za kiutawala ngazi ya mikoa kwa karibu. |
No comments:
Post a Comment