Marando, Nape ni jino kwa jino | Send to a friend |
Thursday, 12 May 2011 22:06 |
Ramadhan Semtawa na Elias Msuya CCM na Chadema, vimeendeleza siasa za jino kwa jino kufuatia viongozi wake kuzidi kurushiana makombora yaliyobeba tuhuma ndani yake.Jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alimtaka Dk Willibrod Slaa ambaye ni Katibu Mkuu wa Chadema aliombe radhi Bunge, huku Chadema nayo ikimtaja Nape kwamba ni mtuhumiwa wa ufisadi wa EPA uliofanyika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambapo Sh133 bilioni zilikwapuliwa. Tuhuma hizo kutoka kila upande, ambazo sawa na siasa za jino kwa jino, zimekuja baada ya Nape kutaja alichokiita unafiki wa Dk Slaa kwa kushinikiza kulipwa mshahara wa Sh7.5 milioni na Chadema, wakati alikataa mshahara wa Sh7 milioni alipokuwa mbunge akidai ni mkubwa na uliwanyonya Watanzania.Vyama hivyo jana kwa nyakati tofauti, kila kimoja kiliongeza mashambulizi dhidi ya kingine, ambapo Nape alikwenda mbali zaidi akimtaka Dk Slaa aliombe radhi Bunge na wabunge kwa alichoeleza kuwa Dk Slaa alipokuwa Mbunge wa Karatu, alichochea chuki kwa wananchi dhidi ya taasisi hiyo. "Najua Chadema watakuwa wanajibu, lakini nasema msimamo wangu uko mbele zaidi kwamba Dk Slaa aliombe radhi Bunge na wabunge, kwani alichochea chuki kwa wananchi dhidi ya Bunge, halafu yeye anakuja kuchukua mshahara zaidi ya ule aliojidai kuukataa. Huu ni unafiki," alisisitiza Nape.Nape alisema Dk Slaa ni Padre hivyo pia alipaswa kuungama kwa Mungu kwa kutokuwa mkweli ndani ya dhamira yake."Bahati nzuri Dk Slaa ni Padre, namshauri pia amuombe radhi Mungu, kwani amekuwa akipita mitaani kupandikiza chuki miongoni mwa Watanzania kumbe naye hana maadili yoyote," aliongeza Nape. Alifafanua kwamba mshahara anaolipwa Dk Slaa ni kodi ya wananchi inayotokana na ruzuku, hivyo ni matumizi mabaya kumpa mshahara mkubwa kama huo wakati aliukataa akiwa mbunge.Kama alivyofanya katika mkutano wa kwanza aliofanya Kata ya Ulugu jimboni Iramba, Nape alisema ataendeleza mashambulizi dhidi ya Dk Slaa katika mikutano yake yote itakayofanyika mkoani Singida ili kuweka wazi maovu ya kiongozi huyo kwa kile alichokiita uchonganishi. "Hapa naelekea Iramba Mashariki, lakini ninachosema ni kwamba, nitaendelea kuwaeleza Watanzania unafiki wa Dk Slaa. Hatutaki viongozi wanaoeneza chuki wakati wao wenyewe hawana maadili yoyote,"aliongeza. Alisema ndani ya Chadema wapo baadhi ya watu wanalipwa kiasi cha fedha ambacho ni kidogo na wanaishi kwa shida kubwa hivyo, kama Dk Slaa ni mwadilifu awaangalie hao. Chadema waja juu Lakini mkutano na waandishi wa habari jana, licha ya kufafanua kuhusu mshahara wa Katibu Mkuu wake, Dk Slaa na ununuzi wa magari, Chadema jana ilimuita Nape kuwa ni 'Vuvuzela' na kwamba hana sifa ya kuinyooshea kidole Chadema. “Tuna ushahidi wa kutosha kuwa mmoja wa watu walionufaika na fedha za EPA kupitia kwa Jeetu Patel ambaye ameeleza vizuri jambo hili katika maelezo yake mbele ya kamati ya Rais,” alisema Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Chadema, Anthony Komu. Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Mabere Marando alidai kuwa Nape aliwahi kuomba kugombea ubunge kupitia Chadema baada ya kushindwa kupata nafasi hiyo kupitia CCM, lakini wakamtosa kwa kuwa hakuwa na sifa. “Nilikuwapo kwenye kikao cha kumjadili Nape, tukaona kuwa hana sifa kumzidi John Mnyika ambaye sasa ni mbunge” alisema Marando. Lakini akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, Nape aliwataka Chadema kutoa ushahidi unaoonyesha kuwa alihusika na ufisadi wa EPA. “Atoe ushahidi hadharani, unajua hawa watu ni waongo, hata Watanzania watawashangaa,” alisema Nape. Kuhusu suala la kuhamia katika chama hicho, Nape alisema: “Tena uandike kabisa, mimi ndiyo ninao ushahidi wa wao kunitaka nikagombee kupitia chama chao nikakataa, kwa sababu siwezi kuhamia kwenye chama cha Wachagga, kile ni chama cha ukoo,” alisema Nape. Mishahara ya Makatibu Wakuu Akifafanua mshahara wa Dk Slaa, Komu alisema kuwa Katibu wake hawajawahi kuomba, kushinikiza wala kuchagiza kulipwa kiasi cha Sh 7.5 milioni kama inavyodaiwa bali analipwa Sh 1,725,000 milioni wakati mbunge analipwa Sh 2,305,000 kabla ya kukatwa kodi. Alifafanua kuwa Dk Slaa pia hulipwa Sh900,000 za mafuta kwa ajili ya kwenda na kurudi ofisini. Vingine ni malipo ya nyumba, mawasiliano na uwajibikaji na hivyo kuufanya mshahara wake kufikia Sh7,174,000 kwa mwezi. “Sekretarieti ya Kamati Kuu ilipeleka pendekezo hilo katika vikao vyake vya Kamati Kuu na Baraza Kuu na pendekezo hilo likapitishwa kwa njia ya uwazi na likaingizwa katika mpango kazi wa chama,” alisema Komu. Naye Mabere Marando alikituhumu CCM kuwa kinamlipa Katibu Mkuu wao Sh 11 milioni akisema: “CCM wanapigia kelele mshahara wa Dk Slaa, mbona Mukama (Wilson) analipwa Sh11 milioni?. Mbona Rais Jakaya Kikwete analipwa posho nyingi tu? Ofisi yake iko Dodoma, lakini akienda huko analipwa posho, akirudi Dar es Salaam analipwa,” alisema Marando. Alipoulizwa na Mwananchi kuhusu madai ya Marando, Mukama alikataa kutaja mshahara wake akisema kuwa ni siri yake. “Mimi leo ndiyo natimiza mwezi mmoja tangu niingine ofisini, hata mshahara wenyewe sijauona. Mshahara ni siri yangu mwenyewe, nimeingia hapa baada ya kustaafu kwa hiyo ndiyo hivyo, naomba msiniingize kwenye hizo ‘debate’ (malumbano)” alisema Mukama. Lakini akijibu hoja hiyo, Nape alisema kuwa Mukama analipwa mshahara kulingana na daraja la viongozi na hurekebishwa kama watendaji wengine serikalini. “Katibu Mkuu wetu analipwa Sh1.5 milioni na hukatwa kodi. Vilevile hulipwa posho isiyokatwa kodi ya Sh300,000. Hayo mengine ya usafiri ni mambo ya kawaida tu. Usafiri anao na hulipiwa umeme wa LUKU na nyumba. Siyo suala la kificho hilo,” alisema Nape. Mafuso ya Chadema Wakijibu hoja ya Nape kuwa Chadema kimenunua magari chakavu, walikanusha wakisema kuwa magari hayo licha ya kutokuwa chakavu, siyo magari ya kawaida bali ni mitambo maalumu ya uenezi. “Katika magari hayo kuna vipaza sauti (Public addressing system 3 sets) zenye thamani ya dola za Marekani 148,000 (Sh 222 milioni), jenereta tatu kila moja Sh15.5 milioni sawa na Sh47,000,000,” alifafanua Komu. Naye Marando alisema kuwa chama ndiyo kilimwomba Mwenyekiti Freeman Mbowe awauzie magari hayo ndipo akakubali. “Mimi mwenyewe nilihusika kumwomba Mbowe atupe magari yale, akakubali. Baada ya hapo Kamati Kuu iliunda kamati ya watu wanne chini ya makamu mwenyekiti Zanzibar Mohamed Issa kumwomba mwenyekiti akiachie chama magari hayo. Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Abdallah Safari alisema kuwa CCM inatumia ujinga wa Watanzania kama mtaji wake na kuwataka Watanzania kutoyumbishwa na propaganda za CCM. |
No comments:
Post a Comment