Tuesday, May 10, 2011

MAPUMZIKO NI MUHIMU KWA WANAFUNZI

Je, wanafunzi huhitaji kupumzika?  Send to a friend
Monday, 09 May 2011 21:30
0diggsdigg
Na Minael Msuya
NIMEWAHI kusikia baadhi ya wanafunzi wakilumbana kuhusu suala la mapumziko pindi wanapomaliza masomo na kurudi majumbani mwao.Malumbano yao yalinifanya nitafakari kwa kina kuhusu elimu husika na mapumziko hayo ndipo nilipojaribu kuwauliza wadau wa elimu.

Wadau hao walinifafanulia kuwa hakuna kazi isiyokuwa na mapimziko, hivyo masomo yanahitaji mapumziko ili mwanafunzi aweze kurejesha akili mpya na kufanya kazi kwa umakini zaidi.

Wanafunzi hao waliokuwa wakilumbana kuhusu mapumziko, baadhi walisema baada ya kutoka shuleni mwanafunzi anapaswa kupata muda mfupi wa kupumzika ili aweze kupata nguvu na akili yake iweze kutulia.

Walisisitiza kuwa mtu anaposoma wakati wote anachoka akili na mwili wake unashindwa kumudu kufanya hata kazi za kawaida mbali na masomo hivyo kila kitu kina faida zake katika kuimarisha mwili na akili ya mtu.
Lakini, wengine walisema baada ya kutoka shule mwanafunzi anapaswa kufanya kazi za nyumbani ili asipoteze muda wake wa kujisomea suala ambalo kimsingi halikuwa na nguvu kwa kuwa tayari wadau wa mambo hayo walisema kila kazi inahitaji mapumziko.

Katika  udadisi  wangu niligundua kuwa wapo wanafunzi wanaojitengea muda mzuri wa kusoma na kufanya kazi pindi wanapotoka shuleni lakini wanasahau kuwa wanapaswa kupata muda wa kupumzisha akili zao japo kwa robo saa.
Hata hivyo fikra zangu zilifika mbali na kujikuta nikiwamulika wazazi kuhusu kuwapangia watoto wao muda wa kazi na kusoma, hapo nilitambua kuwa wazazi wanaweza kuwa chanzo cha kuwafanyisha watoto kazi pindi wanapotoka shuleni kuliko kuwapa muda wa kupumzika na kujisomea.

Katika hili wadau wa elimu wanasema mwanafunzi anapojisomea bila mpangilio wowote ukiwemo muda wa kupumzika anaweza asifikie malengo yake kwa kuwa atakuwa anajichosha kwa kudhani kuwa atafanikiwa kumbe anapotea.

Ni vyema kila mwanafunzi akatambua wajibu wake kimasomo, kupumzika na kusaidia kazi za nyumbani ili aweze kuimarisha afya na kutengeneza msingi mzuri utakaomfanya afaulu vizuri kwa kuzingatia mambo hayo matatu.

Wazazi nao wanatakiwa kuwapangia watoto wao muda wa kupumzika, kujisomea  na kufanya kazi za nyumbani na si kuwapangia watoto kazi  wanapotoka shuleni bila kuwapa muda wa kupumzika.

Wapo baadhi ya wazazi wanawapangia watoto wao kazi nyingi pale wanapotoka shuleni bila kufahamu kuwa watoto wamechoka kwa kiwango gani walipokuwa shuleni.

Kufanya hivyo kutamsaidia mwanafunzi yeyote yule kuweza kumudu masomo yake vizuri kwa kuwa atakuwa na uwezo wa kusoma na kufanya kazi kwa wakati na hata kuweza kupumzisha akili yake pale inapokuwa imechoka.
 

No comments:

Post a Comment