Tuesday, May 17, 2011

MAFISADI NI KAA LA MOTO?

RAIS Jakaya Kikwete ameonyesha kutokuwa na uwezo wa kufukuza wenzake ambao wametuhumiwa ufisadi kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), MwanaHALISI limeelezwa.
Uchambuzi wa hotuba yake wakati wa kufunga vikao vya chama – Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) mjini Dodoma wiki tatu zilizopita, ndio umedhihirisha udhaifu huo.
Badala ya kuwa wazi, thabiti na elekezi, mwenyekiti Kikwete aliongea kwa njia ya kubembeleza huku akijaribu kumtwisha mzigo kila mmoja ukumbini.
Katika hotuba yake ya kufunga, ambayo MwanaHALISI ina nakala yake, Kikwete anang’angania maneno mawili yanayoonyesha, ama woga au kutokuwa tayari kuchukua hatua.
Rais Kikwete alirudia neno “Kukubaliana” mara 18 na neno “Tufanye” mara saba, katika hotuba fupi ya karibu dakika 30. Maneno hayo yametumika pale ambako alitegemewa kutoa kauli inayouma.
“…tuliyokubaliana mnayajua…nikiyarudia nitakuwa nawasumbua kwa sababu tumekubaliana,” alisema bila kutaja kilichokubaliwa.
Tumekubaliana. Hakuna wa kumtumia meseji (sms) mwenyekiti, kwamba hawa jamaa wamekutukana na wewe jibu…Haya tumekubaliana wote. Tukafanye kama tulivyokubaliana” alisema Kikwete akionyesha kutwisha kila mmoja jukumu ambalo yeye angetekeleza mara moja – kufukuza mafisadi. 
Kikwete aliwaambia wajumbe wa NEC Dodoma, “Lakini ni matumaini yangu kwamba tuondoke hapa bila unyonge. Tukafanye kama tulivyokubaliana.
“Nafurahi tumefanya uchambuzi kwa kina na kwa kituo. Kila pendekezo moja baada ya jingine tumelijadili vizuri. Ni kwa sababu, tumejipa muda wa kutosha,” alisema.
Kikwete alisisitiza, “Hakuna atakayetoka hapa na kusema, nilitaka kusema, lakini mwenyekiti ameninyima nafasi. Yupo?” aliuliza Kikwete na sauti zikasikika zikisema, ‘Hakunaa…!’
“Kila aliyetaka kusema nimempa nafasi kwa sababu ya uzito wa jambo lenyewe (hataji jambo). Sisi ni chama cha siasa, kazi yetu ni kushinda uchaguzi; na tunapofanya tathmini ya uchaguzi uliopita, ndipo tunapojijengea nguvu ya kushinda uchaguzi mwingine.”
Kwa kauli hii, wachambuzi wanasema Kikwete alikuwa anawapiga kijembe akina Edward Lowassa, Andrew Chenge na Rostam Aziz ambao walituhumiwa lakini hawakuamsha mkono kujitetea; kwa maana kwamba sasa wanakubaliana na yaliyoamuliwa.
Tumefanya tathimini ya uchaguzi uliopita, ili tupate kujenga misingi ya kushinda uchaguzi mwingine. Tumezungumza kwa kina yote yenye udhaifu kwa upande wetu na tuliokubaliana tunayajua. Twende tukafanye yale tuliotaka tuyafanye sasa; yale ya muda wa kati na yale ya muda mrefu. Na tunapozungumzia muda mrefu hapa, tunakusudia kabla ya mwaka 2014.
Tufanye mageuzi. Tujenge upya chama chetu. Mkimaliza uchaguzi mnafanya tathimini na kwa muono wangu, chama chetu kinatakiwa kufanya mageuzi.
“Tumekuwa na mapendekezo mengi. Tumeletewa tabu (kitabu kikubwa) kubwa lenye kurasa 58. Tumechambua pendekezo moja baada ya jingine kwa utulivu, kwa kituo na kwa kina na tuliyokubaliana tunayajua sote.
“Na kwa kuwa mjadala ulikuwa mkali, safari hii watu walikuwa hawatoki nje, tofauti na vikao vingine. Tumekubaliana ya kuyafanya, twende tukayafanye.
Tumekubaliana mambo ya msingi ya tawi na shina; tumekubaliana kwenye muundao wa chama chetu; tuitishe mkutano mkuu wa taifa ili kurekebisha katiba ili sasa wajumbe wa NEC wapatikane kupitia wilaya ili kupanua uwakilishi.”
Kinachoonyesha kuwa Kikwete, ama anakwepa kusema hoja yenyewe anayojadili au hana dhamira ya kutenda, ni pale anapotaja waziwazi mabadiliko ya Katiba ili kupata wajumbe kutoka wilayani; lakini linalohusu kufukuza au kutenga watuhumiwa wa ufisadi, analizunguka kwa maneno “kukubaliana” na “kufanya” au “kutenda.”
Alisema, “Tumekubaliana kuchambua mazingira ya nchi yetu… Tumezungumza kwa ukali, kwa kina na kwa undani, suala la maadili kwa viongozi wetu. Tuliokubaliana mnayaelewa, lakini la msingi ni kwamba utovu wa maadili, miongoni mwa wanachama na viongozi ni mambo ambayo yamepunguza haiba ya chama chetu mbele ya wananchi.
Tumekubaliana, tusionekane kuwa lichama ambalo vitendo vya rushwa, hatuchukizwi navyo. Wanaofanya vitendo vya rushwa hatuwachukii. Tumekubaliana vizuri. Tumeanza kuchukua hatua na hizo hatua tulizoanza ni sehemu ya yale tuliokubaliana. Kwamba wenzetu tunaowatambua, tusiwaonee haya.
Tumekubaliana hatua mbili: Kwanza, kuwabana ili waamue wenyewe kuwajibika, lakini pili, wanapokataa, tusichelee kuwawajibisha. Maana kuendelea hivi, chama kinasemwa, lakini sisi tunakaa kimya kama vile hakuna kinachofanyika, kunakitokomeza chama chetu,” alieleza Kikwete.  
Ilipofikia CCM hivi sasa, hakuna uwezekano wa kusalimika. Kwa kufukuza watuhumiwa wa ufisadi au kwa kuwaacha katika chama, CCM haiwezi kurejesha hadhi yake.
“Imebakia njia moja tu: Chama chetu kijiandae kukaa pembeni na kujipanga upya; hatimaye kijitahidi kurejea madarakani,” ameeleza kiongozi mstaafu wa ngazi ya juu katika CCM.
Hata hivyo, katika kile kinachoonekana “kurejesha majeshi nyuma,” katibu mkuu mpya wa chama hicho, Wilson Mukama aliwaambia waandishi wa habari wiki iliyopita, “…hakuna mahali popote katika maazimio ya NEC panapotaja siku 90” za kufukuza mafisadi.
Mukama alisema, “Kama ni muda basi ni pale mwenyekiti wetu aliposema NEC ijayo. NEC hukutana kila baada ya miezi minne na kwa hiyo, kama ni siku, basi ni 120 na siyo 90.” Alikuwa akijibu swali la mmoja wa waandishi waliotaka kufahamu lini chama hicho kitaandika barua na kukabidhi watuhumiwa.
Katika mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari, Mukama alisema, “NEC ilitoka na maazimio 26. Azimio mojawapo linasema chama kiendelee na mapambano yake dhidi ya ufisadi na kwamba watuhumiwa wajitafakari, wajipime na kuchukua hatua.”
Taarifa zinanukuu mjumbe mmoja wa NEC ambaye hakupenda kutajwa gazetini akisema Kikwete alipitisha azimio la kuwafukuza Lowassa, Rostam na Chenge kwenye chama kwa staili ya kuviziana ili kuzuia kile alichoita, “hofu ya kujipanga na kurejesha mapigo.”

No comments:

Post a Comment