Marais, mfalme watarajiwa kutua Samunge kwa Babu | Send to a friend |
Wednesday, 11 May 2011 21:50 |
0diggsdigg Mussa Juma, SamungeMARAIS kadhaa wa nchi za Afrika akiwamo mfalme, wanatarajiwa kwenda Samunge, Loliondo kupata tiba ya magonjwa sugu inayotolewa na Mchungaji Ambilikile Mwasapila. Kutokana na ujio huo, ulinzi umeimarishwa kuanzia jana. Ofisa mmoja wa polisi wa Wilaya ya Ngorongoro, alithibitisha ujio wa wakuu hao bila ya kutaka kutoa maelezo zaidi. Hakutaja siku wala muda ambao watawasili hapa. Jana kulikuwa na idadi kubwa zaidi ya polisi kijijini hapa. Ofisa mwingine wa polisi ambaye pia hakutaka jina lake liandikwe alisema, wamepokea taarifa za ujio wa marais hao na walitegemea kwamba wangewasili Samunge kuanzia jana. "Ni kweli, kuna wageni watakuja. Nadhani ni wakubwa bado taarifa kamili hazijatufikia watatua lini," alisema. Helikopta kutoka Rwanda inayomilikiwa na Kampuni ya Akagera Aviation, imeanzisha safari za kwenda Samunge kila siku ikitokea Uwanja wa Ndege wa Arusha. Helikopta hiyo ni kubwa kuliko nyingine ambazo zimekuwa zikitua Samunge kuleta wagonjwa kupata tiba ya kikombe kwa Babu.Ujio wa helikopta hiyo, sasa unalifanya anga la Samunge kutawaliwa na helikopta nne, zinazofanya safari takriban mara tatu kwa siku kwenda na kutoka Samunge. Gharama za nauli kwa abiria mmoja kutoka Arusha hadi Samunge kwa helikopta hiyo ya Rwanda ni Dola za Marekani 1,000 hivyo kufanya usafiri huo kuwa wa watu wenye uwezo mkubwa kifedha. Baada ya kuongezeka wimbi la viongozi kutoka nchi jirani ya Kenya wanaofika Samunge na habari zao kuandikwa, sasa vigogo wengi wa huko wamebuni njia nyingine ya kufika kijijini hapo bila kujulikana. Vigogo hao sasa wanafika Samunge kupitia mpaka wa Narock ambako huenda moja kwa moja hadi Loliondo na kukodi magari ya wenyeji ili kuwapaleka Samunge. Kwa takriban wiki mbili sasa, viongozi kadhaa wa Serikali ya Kenya, wakiwamo maofisa wa Ikulu ya Kenya, mawaziri na wabunge wamekuwa wakitua Samunge. Babu: Wagonjwa waruhusiwe Mchungaji Mwasapila ameomba vituo vinavyoratibu magari yanayokwenda Samunge, kuruhusu magari zaidi kupeleka wagonjwa ili wapate huduma kutokana na kupungua kwa foleni.Msaidizi wa Mchungaji Mwasapila, Frederick Nisajile alisema jana kwamba kutokana na huduma kuboreshwa, idadi ya magari yanayopaswa kuingia Samunge kwa siku yanapaswa kuongezeka. "Tunaomba wawe na mawasiliano na sisi ya mara kwa mara kwani sasa kama unavyoona hakuna foleni, lakini kuna magari yamezuiwa maeneo ya vituo yasije huku," alisema Nisajile. Jana, zaidi ya magari 500 yakiwamo mabasi makubwa kutoka Mikoa ya Kigoma, Dodoma, Mwanza na Arusha yalifika Samunge na abiria kupata kikombe na kuondoka.Hadi majira ya tisa jioni jana, foleni ya magari ilielekea kumalizika kabisa. Bei ya kikombe iko palepale Mchungaji Mwasapila jana alitoa ufafanuzi kuhusu malipo ya kikombe akieleza kuwa hajawahi kupandisha gharama zake tangu mwanzo. Alisema Watanzania wanalipa Sh500 na wageni kutoka nje ya nchi, wanalipa Dola moja au Sh1,500. |
No comments:
Post a Comment