Saturday, April 16, 2011

PAMBAMOTO KUWANYIMA ULAJI WAMILIKI WA MAGAZETI HURU

RAIS Jakaya Kikwete ameombwa kuminya kiuchumi vyombo vya habari binafsi ili kuimarisha vijarida vitakavyoanzishwa na umoja wa vijana wa chama chake (UV-CCM), MwanaHALISI limegundua.
Mawasiliano kati ya viongozi wa umoja huo yanaonyesha kumwomba rais Kikwete  kumuagiza katibu mkuu kiongozi (Philemon Luhanjo), kuelekeza taasisi na mashirika ya umma, kutoa kipaumbele cha matangazo kwa vijarida vya CCM na umoja wake.
Aidha, mawasiliano hayo yanataka Luhanjo, kwa ushirikiano na mkurugenzi wa mawasiliano (ikulu), kuelekeza makatibu wakuu wa wizara zote za serikali na wasemaji wote wa wizara/maafisa uhusiano kuhakikisha wanafanikisha mradi huo wa kunyonga vyombo huru vya habari.
Kwa mujibu wa mawasiliano kati ya Kaimu Mwenyekiti wa UV-CCM, Benno Malisa na katibu msaidi wa chama hicho, wilayani Iringa, Charles Charles, njama hizo zitadhoofisha vyombo huru vya habari na kuimarisha vijarida vya CCM ili “kufanya propaganda zenye maslahi kwa CCM.”
Katika mawasiliano hayo ya imeili ya 30 Machi 2011, saa 9:14 asubuhi, Charles anasema vyombo vingi vya habari nchini maandishi yake yanakwenda kinyume na malengo ya CCM.
Anasema, ”…magazeti ya Uhuru na Mzalendo yamefikia mahali hayana tena mvuto kwa wasomaji na yamekosa utaalamu wa kuyaboresha kutoka pale yalipo hivi sasa na kubadilika; naamini kwamba hatimaye sasa kuna umuhimu wa lazima wa kuwa na gazeti na, au magazeti mbadala…kama sehemu ya mkakati wa kuelekea mwaka 2014 na 2015.”
Charles anashauri gazeti hilo kuchapishwa haraka kutokana na kile alichoita, “hali mbaya ya kihabari dhidi ya CCM na serikali yake inayofanywa na vyombo vingi vya habari hivi sasa na hasa televisheni na magazeti binafasi.”
“Kwa muda mrefu sasa, magazeti ya watu binafsi nchini yameungana kufanya mashambulizi makubwa dhidi ya CCM, jumuiya zake na serikali,” anasema Charles na kuongeza, “Kadri muda unavyokwenda ndivyo hali inavyozidi kuwa mbaya maradufu.”
Waraka wa Charles unamshawishi Malisa kutoa Sh. 11.3 milioni kila mwezi ili kuendesha gazeti la PAMBAMOTO linalomilikiwa na UV-CCM.
Malisa alipoulizwa kuhusu mawasiliano na Charles alisema umoja wake haujafanya “uamuzi wowote kuhusu ufufuaji gazeti la Pambamoto kutokana na hali ya uchumi kutokuwa nzuri.”
Amesema, hata hivyo, akiwa kiongozi, anapokea ushauri na maoni yoyote kutoka kwa wanaotakia mema UV-CCM.
Charles anasema, “Kwa kuwa asimia 75 ya mapato ya vyombo vya habari duniani hutegemea matangazo na mauzo huingiza asilimia 25 tu, nashauri kwamba pindi gazeti hili likianza basi ufanyike utaratibu wa makusudi wa kulipatia matangazo kutoka wizara na taasisi zote za serikali yakiwamo mashirika ya umma kama TTCL (kampuni ya simu) na TANESCO (shirika la umeme la taifa).”
Mashirika mengine ambayo anataka yatoe matangazo kwa gazeti hilo, ni Sumatra, Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Shirika la Viwango la Taifa (TBS), Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), Mamlaka ya Bandari (THA), Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
“Hili lifanyike kwa kuiomba serikali kupitia kwa mwenyekiti wa taifa wa CCM, Rais Kikwete,” ameeleza katika ujumbe wenye sauti ya kulialia.
Lengo la mkakati huo ambao Charles anasema atasimamia mwenyewe, ni kulipa uwezo gazeti kwa kupunguza utegemezi wa ruzuku kutoka vyanzo vingine ambavyo vitakuwa vinatoa fedha.
Gazeti ambalo wahusika wamepanga kumhusisha Rais Kikwete kama “meneja wa matangazo,” kwa mujibu wa waraka, litatoka kila wiki chini ya usimamizi wa Charles anayesema ana “uzoefu… wa muda mrefu wa shughuli hizi.” Litachapwa nakala 5,000 kila wiki.
Charles ambaye yuko Iringa, anamuomba Malisa kusaidia kumrejesha Dar es Salaam ili aweze kufanya kazi yake hiyo kwa urahisi. Hata hivyo amesema atafanya uhariri wa gazeti kutokea nje ya chumba cha habari. 
Ofisa huyo wa CCM anasema wimbi kubwa la vijana, akina mama na makundi mengine limeunga mkono kwa nguvu nyingi “upande wa washindani wetu kisiasa na kuzidi kuimarika, hali ambayo kwangu naamini kwamba itaendelea kuwa mbaya zaidi katika siku zijazo.”
Akiandika kama anayesisitiza kupewa kazi, Charles anasema, “ …ni lazima nilisimamie kuliko kazi hiyo kufanywa na mtu mwingine kwa sababu anaweza kuingiza matakwa yake, kinyume na kazi maalum tunayopanga kuifanya.”
Charles amepanga kujilipa Sh. 440,000 kama mhariri mkuu na mhariri wa habari. Naye mwenyekiti wa bodi ya uhariri atapewa Sh. 300,000. 
Charles anaambatanisha “gharama halisi” za uendeshaji wa gazeti hilo, “fedha ambazo naamini kuwa zitapatikana bila tatizo kama utakuwapo utashi wa kufanya hivyo,” anaeleza.
Katika waraka huo, pamoja na fedha, anaomba vitendea kazi kama kompyuta aina ya laptop. Anasema fedha ambazo zitatumika kuendesha gazeti hilo “ambalo tayari limesajiliwa na serikali, zitatokana na mradi mkubwa wa jengo la kitegauchumi cha UV-CCM.”
Katibu huyo wa CCM aliyewahi kuandikia gazeti la Tazama anamweleza Malisa kuwa “gazeti la kila wiki la Tazama Tanzania ndilo pekee ambalo ni pro-CCM na serikali yake kwa asilimia 100. Lakini yaliyobaki yote yakiwemo hata ya makada wenzetu hayana msimamo wowote,” anaeleza.
Viongozi na makada wa CCM wanaomiliki vyombo vya habari ambao Charles anadai hawaisadii CCM, ni pamoja na wamiliki wa magazeti ya Rai, Mtanzania, The African, Bingwa na Dimba. Vyombo hivi humilikiwa na Rostam Aziz, mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya CCM.
Wamiliki wengine wa vyombo vya habari ambavyo Charles anawagombanisha na Kikwete kuwa wanahujumu serikali yake, ni Anthony Diallo anayemiliki Radio Free Afrika na Star TV na magazeti ya serikali ya Habari Leo na Daily News.
Nalo gazeti la Tazama ambalo Charles anasema linafanya kazi za CCM kwa asilimia 100, limewahi kutuhumiwa na mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela kwa kutumikia “genge la watuhumiwa wakuu wa ufisadi nchini.”
“Kama gazeti anasema hilo linatumikia CCM, basi labda si hii CCM ninayoijua mimi. Huyo Charles Charles ninayemfamu, amekuwa akiwaandika vibaya wajumbe wa Kamati Kuu (CC) wa chama chetu. Sasa hao CCM anaosema wanatetewa na gazeti la Tazama ni wepi,” anasema Christopher ole Sendeka, mbunge wa Simajiro CCM.
Anasema, “Mimi mwenyewe na makada wenzangu, akiwamo ndugu yangu Nape Nnauye, tumeandamwa na gazeti hilo mara kadhaa. Hata mheshimiwa Sitta amelalamikia Tazama mara kadhaa,” anaeleza Sendeka alipoulizwa anavyolifahamu Tazama.
MwanaHALISI lilipowasiliana na Charles kwa njia ya simu ili kupata maoni yake kuhusu kile alichoandika kwa Malisa, alijibu haraka, “Mimi sijui.

No comments:

Post a Comment