Monday, June 6, 2011

KWANINI WATANZANIA WASINUFAIKE NA UTAJIRI WA MADINI WALIOPEWA NA MUNGU?

Hoja Binafsi ya kuunda kamati teule ya Bunge kuchunguza mkataba mpya wa madini ambao Waziri wa Nishati na Madini Karamagi ameusaini bila kuzingatia ma
Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe (Mb) Kigoma Kaskazini

MHESHIMIWA Spika, kwanza napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa kunipatia fursa ya kuleta hoja hii hapa kwenye Bunge lako tukufu kwa mujibu wa kanuni zetu za Bunge. Kuletwa kwa hoja hii, bila kujali maamuzi ya kuhusu hoja yenyewe, ni ishara tosha ya ukomavu wa demokrasia yetu ambayo inakuzwa na mijadala ya Bunge lako tukufu. Nakupongeza kwa dhati kabisa kwa juhudi zako za kuliimarisha Bunge letu na kujenga muhimili imara wa ulinzi wa demokrasia ya vyama vingi nchini kwetu.
Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 16/7/2007 mara baada ya hoja ya Waziri wa Nishati na Madini kuamuliwa na Bunge lako tukufu, nilisimama mahala pangu na kutoa taarifa ya kukusudia kuleta hoja ya kuunda kamati teule ya Bunge. Nilisema kama ifuatavyo (kwa mujibu wa kumbukumbu sahihi za mijadala ya Bunge), ninanukuu ‘…naomba kutoa taarifa rasmi… kwamba nakusudia kuleta hoja ya kuunda kamati teule kuchunguza mkataba mpya wa madini ambao Waziri wa Nishati na Madini ameusaini bila kuzingatia maagizo ya rais (wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) ya kupitia mikataba ya madini aliyoyatoa mbele ya Bunge lako tukufu tarehe 30 Disemba, 2005.’ Mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Spika, nimeshawasilisha hoja yangu hii kwa maandishi kwa Katibu wa Bunge na sasa nawasilisha rasmi katika kikao hiki cha Bunge kwa uamuzi. Nimezingatia kanuni 104 (2) katika kuwasilisha hoja yangu.
Mheshimiwa Spika, katika maelezo yangu niliyowasilisha bungeni wakati wa mjadala wa hotuba ya Waziri wa Nishati na Madini siku ya tarehe 16/7/2007, nilihitaji maelezo kutoka serikalini katika masuala makuu mawili yafuatayo:
  1. Kuondolewa kwa kipengele katika sheria ya kodi ya mapato ya mwaka 1973 kuhusiana na asilimia 15% ya ‘capital allowance on unredeemed qualifying capital expenditure’ bila ya kibali cha Bunge lako tukufu.
  2. Kusainiwa kwa mkataba mpya wa madini wa mgodi (mradi) wa Buzwagi kati ya serikali na Kampuni ya Barrick na sababu za mkataba huo kusainiwa nje ya nchi, London, Uingereza, na vilevile kwa nini mkataba huo umesainiwa wakati bado serikali inafanya durusu (review) ya mikataba kufuatana na maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndugu Jakaya Mrisho Kikwete.
Mheshimiwa Spika, wakati akijibu hoja zangu Waziri wa Nishati na Madini alijenga hoja zake kama ifuatavyo:

A. Kuhusiana na asilimia 15% ya ‘capital allowance on unredeemed qualifying capital expenditure’

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini amenukuliwa na kumbukumbu za majadiliano ya Bunge akisema, ninanukuu: “…kwa hiyo pamoja na kwamba ninamheshimu sana Mheshimiwa Kabwe Zitto na sote tunamheshimu ni msomaji mzuri, lakini wakati mwingine lazima kuangalia vitu gani unasoma. Ni kwamba kipengele hiki cha sheria kililetwa hapa bungeni mwaka 2001 kwenye bajeti kikabadilishwa…” Mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Spika, katika kuandaa hoja yangu hii, ilinibidi kupitia upya kumbukumbu za majadiliano ya Bunge ili kujiridhisha na maelezo ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini, maelezo ambayo mimi nililitaarifu Bunge lako tukufu tarehe 16/7/2007 kuwa sio sahihi.
Mheshimiwa Spika, Kumbukumbu hizo zinaonesha kwamba, sheria ya fedha ya mwaka 2001 (Finance Act. No.14 ya 2001) ilifanyiwa marekebisho kadhaa ikiwemo marekebisho ya sheria ya madini kifungu cha 87 ambapo kifungu kidogo cha (3) cha kifungu cha 87 kiliongezwa. Kifungu kidogo hicho kinasema, ninanukuu:
‘(3) The provisions of subsections (1) and (2) shall not apply to any person who, immediately before the first day of July, 2001 was not the holder of a mineral right granted under this Act.’
Mheshimiwa Spika, kifungu cha 87 cha Sheria ya Madini ya mwaka 1998 (No.5/1998) kinazungumzia mrahaba wa madini (Remission and deferment of royalties). Hivyo, kama sheria ya fedha ya mwaka 2001 haikubadili kipenge hiki, Mheshimiwa Waziri ametoa wapi jibu aliloliambia Bunge?
Mheshimiwa Spika, suala hili linahusu haki, kinga na madaraka ya Bunge kwa mujibu wa sheria namba 3 ya 1988.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo katika hotuba ya Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Basil Mramba, akiwasilisha hotuba ya Bajeti mwaka 2002, tarehe 13 mwezi Juni, alizungumzia kipengele hiki. Ninaomba kunukuu sehemu ya hotuba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Basili Mramba.
“Amendment to the Income Tax structure, (44) Mr. Speaker, in this area I propose to take the following measures:
(v) I propose to reinstate the additional 15 percent capital allowance on unredeemed qualifying capital expenditure as set out in the Mining Act. No. 5 of 1998.” Mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Spika, nilipopitia sheria ya fedha ya mwaka 2002, nimekuta sehemu ya 8 inazungumzia mabadiliko katika kodi ya mapato ya 1973. Na hata katika ukurasa wa kwanza wa sheria hii (Arrangement of Contents), sheria ya madini haitajwi.
Mheshimiwa Spika, maelezo haya ya Waziri wa Fedha ya mwaka 2002 yanaonesha dhahiri utata wa kipengele hiki. Ni kwa vipi kifungu cha sheria ambacho hakijafutwa kirejeshwe?
Mheshimiwa Spika, tuchukulie kuwa maneno ya waziri ni ya kweli. Je, kwa nini makampuni ya madini ambayo yameingia mkataba na serikali kuanzia Julai mosi 2001 hayajaanza kulipa kodi ya mapato?
Mheshimiwa Spika, utata huu ambao umegubika sekta hii ya madini, unaweza kufafanuliwa na Bunge lako tukufu kupitia Kamati Teule. Kamati Teule ya Bunge ichunguze upitiaji wa mikataba hii na kuona kama kuna vitendo vyovyote vya uvunjifu wa sheria za nchi na kupotea kwa mapato ya serikali na ufisadi.

B. Kusainiwa kwa Mkataba wa Mgodi (Mradi) wa Buzwagi.

Mheshimiwa Spika, wakati akijibu hoja yangu kuhusiana na suala la mkataba mpya wa mgodi wa Buzwagi, Waziri wa Nishati na Madini amenukuliwa na kumbukumbu za majadiliano ya Bunge akisema kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Spika, katika tathmini ya migodi, mgodi wa Buzwagi ni marginal mine ambao uhai wake si wa muda mrefu. Bila ya kutumia fursa ya sasa ya bei ya dhahabu, uwekezaji wake usingeweza kuwa wa faida. Hata hivyo, mkataba wa Buzwagi hauna mapungufu yaliyokuwamo kwenye mikataba ya zamani.’ Mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Spika, mapitio ya mikataba ya madini ni mchakato ambao mwisho wake ni kuletwa kwa sheria ya madini hapa bungeni na kuifanyia marekebisho ili kuiboresha na kuondoa mapungufu. Hivyo, mpaka hapo sheria itakaporekebishwa, ndipo tutasema tumemaliza zoezi la kupitia mikataba ya madini na hivyo kusaini mikataba mipya na makampuni yote ya madini yaliyopo nchini na yatakayokuja kuwekeza.
Mheshimiwa Spika, suala ambalo linanipelekea kuomba kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kuchunguza mkataba huu mpya, ni kuhusu uharaka uliopelekea Waziri wa Nishati na Madini kusaini mkataba huu. Sheria ya Madini bado haijarekebishwa, je, waziri anatumia vigezo gani kusema mkataba mpya wa Buzwagi aliousaini London hauna mapungufu?
Mheshimiwa Spika, Waziri wa Nishati na Madini aliliambia Bunge lako tukufu kuwa Buzwagi ni marginal mine. Vile vile waziri anasema kuwa Kampuni ya Barrick inamiliki migodi mitatu tu kupitia kampuni zake tanzu ambazo ni Bulyanhulu Gold Mine, North Mara Gold Mine na Pangea Minerals Limited Tulawaka. Kwa maelezo haya ya Waziri Karamagi, Buzwagi sio mgodi.
Mheshimiwa Spika, hoja hii ya kuwa Buzwagi sio mgodi inashabihiana kabisa na hoja ya Kampuni ya Barrick kwamba Buzwagi ni Project. Taarifa ya kampuni hii ya Barrick Gold Corporation-Global operations-Africa- Buzwagi, inaonesha kuwa Buzwagi ni mradi. Taarifa hii ninaiambatanisha katika hoja hii.
Mheshimiwa Spika, taarifa ya Barrick, Annual Review 2006 inasema ifuatavyo katika ukurasa wa 23, ninanukuu. ‘A major milestone was reached in February 2007 when we signed a mineral Development Agreement (MDA) with the Tanzanian government. In 2007, we expect to complete a detailed construction design and receive EIA approval.’
Mheshimiwa Spika, suala ambalo vile vile linanisukuma kuomba Bunge lako tukufu kuunda Kamati Teule ni kwamba, iwapo Buzwagi sio mgodi bali ni mradi, ni kwa nini tumesaini Mineral Development Agreement (MDA) mpya? Kwa kuwa Pangea Minerals Tulawaka ndio inaonekana kumiliki mradi huu, je, serikali imefanya marekebisho tu ya MDA na Kampuni ya Barrick? Naomba Kamati Teule ichunguze ni nini kilichosainiwa, marekebisho ya mkataba wa Tulawaka au MDA mpya ya Buzwagi?
Mheshimiwa Spika, Buzwagi inashika nafasi ya pili kwa uwekezaji wa Barrick katika migodi hapa nchini. Wakati kampuni hii inawekeza dola za Kimarekani 400 milioni katika Buzwagi, imewekeza dola za Kimarekani 600 katika Bulyanhulu. Je, ni kwa vipi Buzwagi iwe marginal mine wakati uwekezaji wake unashinda uwekezaji wa Tulawaka na North Mara?
Mheshimiwa Spika, chini ya kifungu cha 47 cha Sheria ya Madini ya Mwaka 1998 (Na.5/98), pamoja na mambo mengine kinataka leseni yoyote isitolewe mpaka taarifa ya mazingira iwe imetolewa na kuruhusu mgodi kuendelea na kazi.
Mheshimiwa Spika, wakati Waziri wa Nishati na Madini ameweka saini mkataba wa Buzwagi juma la mwisho la mwezi Februari 2007, Baraza la Mazingira nchini limetoa kibali (Environmental Impact Assessment- EIA approval) tarehe 11 mwezi Mei 2007. Ni kwa nini Waziri wa Nishati na Madini, Mheshimiwa Nazir Karamagi alisaini MDA ya Buzwagi na Kampuni ya Barrick kabla Baraza la Mazingira la Taifa (NEMC) halijatoa ruhusa?
Mheshimiwa Spika, sheria ya madini, niliyoitaja hapo awali, imeunda Kamati ya Ushauri ya Madini (Mining advisory Committee). Kabla ya waziri kusaini mkataba wowote ni lazima apate ushauri kutoka kamati hii. Kwa taratibu za kiserikali, kama kamati ikimshauri waziri na waziri akakataa ushauri huo, inampasa waziri atoe sababu ni kwa nini anakataa ushauri. Je, waziri alifuata ushauri wa Kamati ya Ushauri ya Madini kuhusiana na wakati mwafaka wa kusaini mkataba huu?
Mheshimiwa Spika, inawezekana kabisa MDA ya Buzwagi kusainiwa Uingereza sio tatizo. Kwa mfano, mwaka 2006 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilisaini mikataba kadhaa. Ni mingapi kati ya mikataba hii imesainiwa nje ya nchi? Nini madhara ya kisheria kwa mkataba kusaniwa Uingereza? Je, mkataba umeandikwa “signed in London...” au “signed in Dar es Salaam...? Kamati Teule ya Bunge ndio chombo pekee kitakachoweza kutoa majibu ya maswali haya.
Mheshimiwa Spika, suala hili ni suala la kitaifa. Halina hata chembe ya itikadi za kivyama. Ninaamini wabunge wataamua kwa maslahi ya taifa letu. Uundwaji wa Kamati Teule ya Bunge kuchunguza mapitio ya mikataba ya madini na mazingira ya kusainiwa kwa mkataba mpya wa Buzwagi yatatoa msaada mkubwa kwa azma ya Rais wetu ndugu Jakaya Mrisho Kikwete ya kuona rasilimali za madini zinafaidisha nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, ninaomba kutoa hoja

No comments:

Post a Comment