Tuesday, May 17, 2011

MAFISADI NI KAA LA MOTO?

RAIS Jakaya Kikwete ameonyesha kutokuwa na uwezo wa kufukuza wenzake ambao wametuhumiwa ufisadi kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), MwanaHALISI limeelezwa.
Uchambuzi wa hotuba yake wakati wa kufunga vikao vya chama – Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) mjini Dodoma wiki tatu zilizopita, ndio umedhihirisha udhaifu huo.
Badala ya kuwa wazi, thabiti na elekezi, mwenyekiti Kikwete aliongea kwa njia ya kubembeleza huku akijaribu kumtwisha mzigo kila mmoja ukumbini.
Katika hotuba yake ya kufunga, ambayo MwanaHALISI ina nakala yake, Kikwete anang’angania maneno mawili yanayoonyesha, ama woga au kutokuwa tayari kuchukua hatua.
Rais Kikwete alirudia neno “Kukubaliana” mara 18 na neno “Tufanye” mara saba, katika hotuba fupi ya karibu dakika 30. Maneno hayo yametumika pale ambako alitegemewa kutoa kauli inayouma.
“…tuliyokubaliana mnayajua…nikiyarudia nitakuwa nawasumbua kwa sababu tumekubaliana,” alisema bila kutaja kilichokubaliwa.
Tumekubaliana. Hakuna wa kumtumia meseji (sms) mwenyekiti, kwamba hawa jamaa wamekutukana na wewe jibu…Haya tumekubaliana wote. Tukafanye kama tulivyokubaliana” alisema Kikwete akionyesha kutwisha kila mmoja jukumu ambalo yeye angetekeleza mara moja – kufukuza mafisadi. 
Kikwete aliwaambia wajumbe wa NEC Dodoma, “Lakini ni matumaini yangu kwamba tuondoke hapa bila unyonge. Tukafanye kama tulivyokubaliana.
“Nafurahi tumefanya uchambuzi kwa kina na kwa kituo. Kila pendekezo moja baada ya jingine tumelijadili vizuri. Ni kwa sababu, tumejipa muda wa kutosha,” alisema.
Kikwete alisisitiza, “Hakuna atakayetoka hapa na kusema, nilitaka kusema, lakini mwenyekiti ameninyima nafasi. Yupo?” aliuliza Kikwete na sauti zikasikika zikisema, ‘Hakunaa…!’
“Kila aliyetaka kusema nimempa nafasi kwa sababu ya uzito wa jambo lenyewe (hataji jambo). Sisi ni chama cha siasa, kazi yetu ni kushinda uchaguzi; na tunapofanya tathmini ya uchaguzi uliopita, ndipo tunapojijengea nguvu ya kushinda uchaguzi mwingine.”
Kwa kauli hii, wachambuzi wanasema Kikwete alikuwa anawapiga kijembe akina Edward Lowassa, Andrew Chenge na Rostam Aziz ambao walituhumiwa lakini hawakuamsha mkono kujitetea; kwa maana kwamba sasa wanakubaliana na yaliyoamuliwa.
Tumefanya tathimini ya uchaguzi uliopita, ili tupate kujenga misingi ya kushinda uchaguzi mwingine. Tumezungumza kwa kina yote yenye udhaifu kwa upande wetu na tuliokubaliana tunayajua. Twende tukafanye yale tuliotaka tuyafanye sasa; yale ya muda wa kati na yale ya muda mrefu. Na tunapozungumzia muda mrefu hapa, tunakusudia kabla ya mwaka 2014.
Tufanye mageuzi. Tujenge upya chama chetu. Mkimaliza uchaguzi mnafanya tathimini na kwa muono wangu, chama chetu kinatakiwa kufanya mageuzi.
“Tumekuwa na mapendekezo mengi. Tumeletewa tabu (kitabu kikubwa) kubwa lenye kurasa 58. Tumechambua pendekezo moja baada ya jingine kwa utulivu, kwa kituo na kwa kina na tuliyokubaliana tunayajua sote.
“Na kwa kuwa mjadala ulikuwa mkali, safari hii watu walikuwa hawatoki nje, tofauti na vikao vingine. Tumekubaliana ya kuyafanya, twende tukayafanye.
Tumekubaliana mambo ya msingi ya tawi na shina; tumekubaliana kwenye muundao wa chama chetu; tuitishe mkutano mkuu wa taifa ili kurekebisha katiba ili sasa wajumbe wa NEC wapatikane kupitia wilaya ili kupanua uwakilishi.”
Kinachoonyesha kuwa Kikwete, ama anakwepa kusema hoja yenyewe anayojadili au hana dhamira ya kutenda, ni pale anapotaja waziwazi mabadiliko ya Katiba ili kupata wajumbe kutoka wilayani; lakini linalohusu kufukuza au kutenga watuhumiwa wa ufisadi, analizunguka kwa maneno “kukubaliana” na “kufanya” au “kutenda.”
Alisema, “Tumekubaliana kuchambua mazingira ya nchi yetu… Tumezungumza kwa ukali, kwa kina na kwa undani, suala la maadili kwa viongozi wetu. Tuliokubaliana mnayaelewa, lakini la msingi ni kwamba utovu wa maadili, miongoni mwa wanachama na viongozi ni mambo ambayo yamepunguza haiba ya chama chetu mbele ya wananchi.
Tumekubaliana, tusionekane kuwa lichama ambalo vitendo vya rushwa, hatuchukizwi navyo. Wanaofanya vitendo vya rushwa hatuwachukii. Tumekubaliana vizuri. Tumeanza kuchukua hatua na hizo hatua tulizoanza ni sehemu ya yale tuliokubaliana. Kwamba wenzetu tunaowatambua, tusiwaonee haya.
Tumekubaliana hatua mbili: Kwanza, kuwabana ili waamue wenyewe kuwajibika, lakini pili, wanapokataa, tusichelee kuwawajibisha. Maana kuendelea hivi, chama kinasemwa, lakini sisi tunakaa kimya kama vile hakuna kinachofanyika, kunakitokomeza chama chetu,” alieleza Kikwete.  
Ilipofikia CCM hivi sasa, hakuna uwezekano wa kusalimika. Kwa kufukuza watuhumiwa wa ufisadi au kwa kuwaacha katika chama, CCM haiwezi kurejesha hadhi yake.
“Imebakia njia moja tu: Chama chetu kijiandae kukaa pembeni na kujipanga upya; hatimaye kijitahidi kurejea madarakani,” ameeleza kiongozi mstaafu wa ngazi ya juu katika CCM.
Hata hivyo, katika kile kinachoonekana “kurejesha majeshi nyuma,” katibu mkuu mpya wa chama hicho, Wilson Mukama aliwaambia waandishi wa habari wiki iliyopita, “…hakuna mahali popote katika maazimio ya NEC panapotaja siku 90” za kufukuza mafisadi.
Mukama alisema, “Kama ni muda basi ni pale mwenyekiti wetu aliposema NEC ijayo. NEC hukutana kila baada ya miezi minne na kwa hiyo, kama ni siku, basi ni 120 na siyo 90.” Alikuwa akijibu swali la mmoja wa waandishi waliotaka kufahamu lini chama hicho kitaandika barua na kukabidhi watuhumiwa.
Katika mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari, Mukama alisema, “NEC ilitoka na maazimio 26. Azimio mojawapo linasema chama kiendelee na mapambano yake dhidi ya ufisadi na kwamba watuhumiwa wajitafakari, wajipime na kuchukua hatua.”
Taarifa zinanukuu mjumbe mmoja wa NEC ambaye hakupenda kutajwa gazetini akisema Kikwete alipitisha azimio la kuwafukuza Lowassa, Rostam na Chenge kwenye chama kwa staili ya kuviziana ili kuzuia kile alichoita, “hofu ya kujipanga na kurejesha mapigo.”

NDUGU YANGU NAPE JIPYA ULILONALO NI LIPI KAMA ULITAKA KUIASI CHAMA KWA UBABAISHAJI WAKE?

Vita ya Chadema, CCM sasa yafika patamu  Send to a friend
Sunday, 15 May 2011 11:01
0diggsdigg
Edwin Mjwahuzi, Ruvuma
VITA ya maneno kati ya Chadema na CCM jana imechukua sura mpya baada ya Fred Mpendazoe kumtaja Katibu Mwenezi na Itikati wa CCM, Nape Nauye kuwa miongoni mwa vigogo sita walioanzisha Chama cha Jamii (CCJ) .Mpendazoe alitoboa siri hiyo jana alipokuwa akituhubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Mbamba Bay kilichopo katika wilaya mpya ya Nyasa mkoani Ruvuma.

Mpendazoe alijitoa CCM Machi 30, mwaka jana akiwa Mbunge wa Kishapu na kujiunga na CCJ Aprili 16, mwaka huo kabla ya kuhamia Chadema, baada ya CCJ kukosa sifa na kufutwa na Msajili wa Vyama vya Siasa.Akihutubia mkutano wa hadhara katika mji wa Mbamba Bay, mkoani Ruvuma jana, Mpendazoe alisema ameamua kuliambia taifa ukweli kuhusu Nape, ili umma uepuke kudanganywa na propaganda za kijana huyo

.“Kelele zote anazopiga Nape kuitetea CCM ni za kinafiki kwani aliwahi kukigeuka chama hicho na kushiriki katika mipango yote ya kuanzisha CCJ”.Hata hivyo, Nape alipoulizwa na gazeti hili jana kuhusiana na madai hayo ya Mpendazoe, hakukataa wala kukubali kushiriki kuanzishwa CCJ, badala yake alisema, "Cha msingi waeleze (Chadema) CCJ ilikufaje, wasiseme ilizaliwaje, maana kuzaliwa ni sherehe na kufa ni kilio.” Nape ambaye hakusema lolote kama kombora la Mpendazoe ni la kweli aliwageuzia kibao Chadema akisema, "Pamoja na hayo yote, waache (Chadema) kubaka demokrasia."

Alifafanua akisema "Watanzania walipiga kura kuichagua CCM iwaongoze kwa miaka mitano ijayo, sasa wanaposema tutaandamana nchi nzima ili serikali iondoke kabla ya muda huo, huku ni kubaka demokrasia na ni uhaini."Mpendazoe alisisitiza kuwa Nape alishiriki katika kuandaa na kuandika katiba na miko ya uongozi ya CCJ, kutafuta fedha za kukuza chama na jengo la kuweka ofisi za chama hicho.

Alisema: “ Huyo Nape anayepiga kelele za kuitetea CCM ni mnafiki mkubwa pengine kuliko wanafiki wote hivi sasa. Mimi na yeye pamoja na wanaCCM wengine wanne, ndio tulioamua kuanzisha CCJ.“Nape ndiye aliyepewa jukumu la kutafuta nakala za katiba za vyama tawala vya nchini za Afrika, ili kupata katiba nzuri ya itakayoigwa katika kuandika katiba ya CCJ.”

Alisema Nape alilitekeleza vizuri jukumu hilo na kufanikiwa kuipata katiba ya chama tawala cha Afrika Kusini cha ANC, ambacho ndiyo kilitumika kwa kiasi kikubwa kuandaa katiba ya CCJ.Alisema yeye, Nape na vigogo wengine aliosema atawataja muda ukifika walifanya vikao vyote vya siri hadi wakaanzisha chama hicho cha CCJ.

“Tulifungua mtandao maalumu wa kuwasiliana kwa internet, ambao baadaye wenzangu waliufuta baada ya kubadili mawazo dakika za mwisho. Lilipotulazimu kukutana mimi na Nape tulipendelea kukutana katika eneo la vinywaji pale Mlimani City, jijini Dar es Salaam”.Alisema walifanya hivyo ili wasitiliwe shaka na maafisa usalama wa taifa waliopewa kazi ya kupeleleza wanaCCM waliohisiwa kutaka kuanzisha chama kipya.

“Nape alibadili mawazo ya kutaka kuihama CCM baada ya Rais Jakaya Kikwete kumteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Masasi, kwa kuwa alikuwa na uchu wa madaraka ,” aliongeza. Alisema Nape aliisaidia CCJ kwa kukipa siri nyingi ikiwamo mambo yaliyokuwa yakijadiliwa kwenye mikutano ya Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) na hata vikao vilivyokuwa vikifanyika katika Ofisi Ndogo ya CCM iliyopo Lumumba.“Nape pia alitupa siri kwamba baadhi ya walioanzisha CCJ walikuwa wanakaribia kufukuzwa kwani katika mkutano wa NEC, majina ya baadhi yao yalitajwa na kujadiliwa kwenye kikao hicho.'

Tuhuma za Chadema dhidi ya Nape na majibu ya Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi wa CCM, ni mwendelezo wa siasa za jino kwa jino za kurushiana makombora yaliyobeba tuhuma nzito ndani yake.

Mei 12 mwaka huu Nape alimtaka Dk Slaa kuliomba radhi Bunge, huku Chadema nayo ikimtaja Nape kwamba ni mtuhumiwa wa ufisadi wa EPA uliofanyika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambapo Sh133 bilioni zilikwapuliwa. 
Tuhuma hizo kutoka kila upande, zimekuja baada ya Nape kutaja alichokiita unafiki wa Dk Slaa kwa kushinikiza kulipwa mshahara wa Sh7.5 milioni na Chadema, wakati alikataa mshahara wa Sh7 milioni alipokuwa mbunge akidai ni mkubwa na uliwanyonya Watanzania.

Katika mkutano wake wa hadhara siku hiyo Nape alimtaka Dk Slaa kuliomba radhi Bunge na wabunge kwa kile alichoeleza kuwa alipokuwa Mbunge wa Karatu, alichochea chuki kwa wananchi dhidi ya taasisi hiyo.
"Najua Chadema watakuwa wanajibu, lakini nasema msimamo wangu uko mbele zaidi kwamba Dk Slaa aliombe radhi Bunge na wabunge, kwani alichochea chuki kwa wananchi dhidi ya Bunge, halafu yeye anakuja kuchukua mshahara zaidi ya ule aliojidai kuukataa. Huu ni unafiki," alisisitiza Nape.

Nape alisema Dk Slaa ni Padre hivyo pia alipaswa kuungama kwa Mungu kwa kutokuwa mkweli ndani ya dhamira yake."Bahati nzuri Dk Slaa ni Padre, namshauri pia amwombe radhi Mungu, kwani amekuwa akipita mitaani kupandikiza chuki miongoni mwa Watanzania kumbe naye hana maadili yoyote," aliongeza Nape.

Wakati Nape akitoa shutuma hizo dhidi ya Dk Slaa, siku hiyo Mei 12, Chadema aliitisha mkutano na waandishi wa habari ambako licha ya kufafanua kuhusu mshahara wa Katibu Mkuu huyo na ununuzi wa magari, ilimwita Nape kuwa ni 'Vuvuzela' na kwamba hana sifa ya kuinyooshea kidole Chadema.

“Tuna ushahidi wa kutosha kuwa mmoja wa watu walionufaika na fedha za EPA kupitia kwa Jeetu Patel ambaye ameeleza vizuri jambo hili katika maelezo yake mbele ya kamati ya Rais,” alisema Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Chadema, Anthony Komu

AMAZING,WAS SITA THE FOUNDER OF CCJ?

Mpendazoe aanika walioanzisha CCJ  Send to a friend
Monday, 16 May 2011 21:39
0diggsdigg
Kada wa Chadema, Fred Mpendazoe akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa National Housing mjini Njombe.Picha na Edwin Mjwahuzi
Waandishi Wetu
KADA wa Chadema, Fred Mpendazoe amewataja mawaziri wawili wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, mbunge mmoja wa CCM na makada wengine wawili wa chama hicho tawala kuwa ni miongoni mwa watu waliokuwa katika harakati za kukihama na kujiunga na CCJ.Mpendazoe ambaye alikuwa kada wa kwanza wa CCM kuhamia CCJ wakati huo akiwa Mbunge wa Kishapu, aliwataja waanzilishi hao wa CCJ kuwa ni pamoja na Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Naibu Waziri mmoja na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye.

Kwa mujibu wa Mpendazoe, katika kundi hilo pia wamo kada wa Jumuia ya Umoja wa Vijana wa CCM na mbunge mmoja kutoka Mkoa wa Mbeya. Hatukuandika majina ya baadhi ya viongozi waliotajwa kwa sababu hatukufanikiwa kuwapata kujibu tuhuma hizo.Hata hivyo, Sitta alipipogiwa simu alisema asingeweza kuzungumza lolote kuhusu madai hayo akisema anasubiri kusoma alichosema Mpendazoe.

Mpendazoe aliwataja makada hao jana wakati akihutubia umati uliokusanyika kwenye Viwanja vya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Njombe Mjini katika mkutano wa hadhara wa Chadema."Nilipoondoka CCM mimi nilikuwa ni mmoja wa waanzilishi wa CCJ, lakini wengine walikuwa hawajulikani na leo nitawataja hao wengine kwa kuwa CCM inajidai kujivua gamba ili kuwadanganya wananchi," alisema Mpendazoe.Alisema hao aliowataja ndiyo waliotaka kukihama CCM, lakini walibaki si kwa ajili ya maslahi ya Taifa, bali ni kwa maslahi yao binafsi.

"Sitta na (makada wengine) wameingia katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, lakini ni wasaliti na Serikali ya CCM ya sasa haiwezi kuwasaidia Watanzania," alisema na kuongeza:
"Wamevaa ngozi ya kondoo kwa kupinga ufisadi kwa maslahi yao, lakini leo bado wako pale."
Akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema viongozi wa CCM ni wanafiki na ndiyo maana, hawaelewi wanachokifanya zaidi ya kuwadanganya wananchi.

Aliitaka serikali kuacha ubabaishaji na kuchukua hatua zinazoweza kuwaletea wananchi maendeleo na kuliinua Taifa.
Dk Slaa alitumia nafasi hiyo kumshambulia Spika wa Bunge, Anne Makinda. Aliwahoji wakazi wa Njombe waliohudhuria mkutano huo kama uspika wake unawasaidia chochote na wao wakajibu kwa kupiga kilele: "Hakuna chochote."

"Nilipokuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, niliwahi kukagua Njombe na miradi yenu nikagundua kuwa hakuna maendeleo yoyote ikiwamo kituo cha basi cha Njombe ambacho hakifai," alisema Dk Slaa.
Alisema kutokana na kuendelea kumpigia kura kwa muda mrefu, wananchi hao wataendelea kunyanyasika na familia ya mbunge wao itaendelea kuneemeka kwa kutumia mgongo wao.

Mukama: Chadema kiache ubabaishaji
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilson Mukama amekitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuacha kile alichodai kuwadanganya wananchi kwamba CCM kujivua gamba si kitu akisema hatua hiyo imefikiwa kukiimarisha chama baada ya kutambua kuwa bila hivyo nchi itayumba. Mukama alisema hayo kwa nyakati tofauti juzi na jana katika Kijiji cha Kibara, wilayani Bunda na katika Kijiji cha Kaburabura, wilayani Musoma katika mikutano ya hadhara, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku nane mkoani Mara.

Alisema CCM kimetumia dhana hiyo ya kujivua gamba ili kiweze kurudi kwenye misingi imara, ikiwa ni pamoja na kufanya mabadiliko makubwa, hali ambayo itakiweka kwenye mstari unaotakiwa ambao lengo lake ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata maendeleo na huduma zote muhimu.
Alisema anawashangaa wapinzani wanaotumia muda mrefu kujadili falsafa ya kujivua gamba na kuhoji uwezo wao katika kutekeleza miradi ya maendeleo.

Alisema amesikitishwa na kauli ya viongozi wa Chadema kwamba kuna uwezekano Rais Kikwete kuondoka madarakani kabla ya 2015 kwa kutolea mfano wa Waziri Mkuu wa Japan aliyeondolewa madarakani.
Alifafanua kuwa viongozi wa Chadema wanatakiwa kufanya uchunguzi kabla ya kutoa matamko kwa maelezo kuwa Waziri Mkuu wa Japan hawezi kufananishwa na Rais Jakaya Kikwete kwa vile aliwekwa madarakani na Bunge wakati Rais alichaguliwa na wananchi.

Alisema kuwa, hata Mwalimu Julius Nyerere enzi za uhai wake aliwahi kutamka kuwa, bila CCM ya kweli nchi itayumba na kwamba ndiyo maana chama hicho kimeamua kutumia dhana hiyo ya kujivua gamba ili kiweze kuwa imara na kinachoweza kusimamia maendeleo ya wananchi.

"Tunakiweka katika misingi ya kukiimarisha ili kiwe chombo imara ambacho kweli kinaweza kusimamia maendeleo katika maeneo yetu tunayoishi. Sasa hawa Chadema wameichukua dhana hiyo ya kujivua gamba visivyo kabisa," alisema.

Alisema hiyo inatokana na viongozi wa Chadema kuwa na tabia ya kurukia mambo bila kuyafanyia uchunguzi na kwamba wameichukua dhana hiyo visivyo na kuendelea kuwarubuni wananchi ili wakichukie CCM na serikali yao... "Hawa wanataka kwenda Ikulu kwa maneno ya udanganyifu kabisa na maandamano yasiyokuwa na msingi wowote."
Pia alisema kuwa CCM haiwezi kufa kama upinzani wanavyoendelea kuwaambia wananchi, kwani ni chama kikubwa, taasisi na si kampuni ya kibiashara.

Aidha, Mukama amekiponda Chadema ambacho kimekuwa kikidai kwamba CCM imekumbatia wafanyabiashara na kueleza kuwa Chadema ndicho kinayofanya hivyo."Sasa watu wanaokumbatia sera ambazo mwalimu alikuwa anazipinga, eti ndio wanakwenda kwenye kaburi pale wanasema tunakuomba leo utusikilize tuweze kutawala nchi hii kidogo," alisema.

Alisema CCM kina matajiri wachache ambao wanataka kukitumia kwa ajili ya kujinufaisha na kuonya kuwa wafanyabiashara ambao maadili yao hayaendani na chama chao wataondolewa na kuwekwa pembeni mara moja.

Amewataka wakuu wa wilaya nchini na viongozi wa CCM, kusimama imara na kuhakikisha fedha za miradi mbalimbali zinazoletwa na Serikali katika halmashauri husika, zinafanya kazi iliyokusudiwa na si kuishia kwenye mikono ya wajanja wachache.
Alisema kuwa ni lazima wakuu wa wilaya pamoja na viongozi wa chama hicho watekeleze wajibu wao ipasavyo wa kusimamia fedha za Serikali zinazopelekwa kwenye  halmashauri.Habari hii imeandaliwa na Boniface Meena, Njombe; Ahmed Makongo na Christopher Maregesi, Bunda na Beldina Nyakeke, Musoma Vijijini.