Sunday, June 5, 2011

NATUMAINI MAFANIKIO UNAYOYASEMA SIO KUPANGA CHUMBA KIMOJA USWAHILINI NA KUMILIKI BALOON 2ND HAND

ELIAS BARNABAS: THT imenifikisha hapa nilipo  Send to a friend
Saturday, 28 May 2011 18:05
0diggsdigg
Furaha Maugo
MAFANIKIO ya wasanii wanaopikwa ndani ya nyumba Nyumba ya Vipaji Tanzania (THT), tangu kuanzishwa kwake yanathibitisha  kazi nzuri inayofanywa na wasimamizi wa  nyumba hiyo.

Mmoja wa wasanii walitoka THT ni Elias Barnabas, maarufu kwa jina la Barnaba ambaye amefanikiwa kushinda tuzo ya Wimbo bora wa Zouk, katika tuzo za muziki za Kilimanjaro mwaka 2010/11.
Alijiunga na THT, mwaka 2006 kutokana na msukumo kutoka kwa rafiki yake waliyekuwa wanaimba, kupiga vyombo na kusali naye kanisani.

Tangu ameingia katika nyumba hiyo ya kuzalisha,  kutengeneza na kukuza vipaji, Barnaba ametawala sana midomoni mwa wapenzi wa muziki wa kizazi kipya.
Hii ni kutokana na baadhi ya nyimbo zake alizoimba na kufanya vizuri katika anga la muziki wa kizazi kipya hapa nchini.
Licha ya kuimba, Barnaba ana uwezo mkubwa wa kutumia ala mbalimbali za muziki kama vile gita na ‘keyboard’. Pia ana uwezo wa kupangilia sauti yake kwa ustadi na kutawala jukwaa vyema anapokuwa kukwaani.

Ni kutokana na uwezo wake huo, Barnaba amepewa jukumu la kufundisha wasanii wenzake katika kundi la THT.
Mafanikio ya baadhi ya nyimbo za kizazi kipya, zinazofanya vizuri hivi sasa zimetungwa na Barnaba, nyimbo hizo ni pamoja wimbo wa Mwasiti (Kisa Pombe), wimbo wa Ray C, (Watanionaje), ‘Kizunguzungu’ ulioimbwa na Rachel, ‘Najua’ ulioimbwa na Linah na ‘Shukurani’ ulioimbwa na Nakaaya.
Nyingine ni ‘Wrong number’ aliyoimbwa na Linah  na ‘Milele daima’, wimbo ambao unaofanya vizuri katika chati za vituo vingi vya redio na televisheni.


 “Ninashukuru Mungu sasa hivi  uwezo wangu ni mkubwa kwenye kuimba, kutumia vyombo na hata kuingiza sauti studio,” anasema Barnaba alipozungumza na Mwananchi Jumapili.
Kuonyesha kuwa anakipaji cha hali ya juu na anafanya kazi yake kwa umakini ilimchukua takribani miaka miwili (2008-2010)kukamilisha  albamu yake  ya  ‘Njia Panda’,  ambayo  alishirikiana na Amini iliyokuwa na jumla ya nyimbo 14.
Baadhi ya nyimbo zinazopatikana katika albamu hiyo ni ‘Njia panda’ aliyoimba na  Pipi, ‘Muongo’ , ‘ ‘Robo saa’,  na ‘Mbala mwezi’  zote ameimba akishirikiana na Amini, Wrong Number aliyoimba  na msanii bora wa kike mwaka 2011, Linah.
Nyingine ni ‘Kodi Mangasubi’ ,  ‘Nivumilie’, ‘Nimelimiss’,   ‘Baby I Love’, ‘mdomo’, ‘ Mwongo’, ‘Dukuduku’ na ‘Huruma’.
Barnaba anasema ingawa hakusoma sana,  mafunzo aliyopta THT  ndiyo yaliyomfikisha hapa alipo na kufafanua:  “Niliweka juhudi kubwa kwenye mafunzo nilipokuwa darasani na kuyafanyia kazi mambo yote niliyofundishwa na mwalimu wangu.
“Matunda ninayopata yametokana na heshima na uvumilivu niliokuwa nao kipindi chote cha mafunzo. Hivi sasa ninaweza kukidhi mahitaji yangu binafsi na nimehama nyumbani sasa nakaa kwangu na ninapata kila ninachohitaji,” anasema Barnaba.
Barnaba anasema  anavutiwa sana na kazi za wanamuziki wengine wa Afrika, kama vile Fally Ipupa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Barnaba anampamgo wa kurudi shule kujiendeleza.  “Kwa kuwa sikubahatika kumaliza elimu yangu vizuri nina mpango wa kurudi tena shule, nafikiria kuendelea na elimu ingwa sijajua nataka kusomea kitu gani,” anasema.
Wasifu
Alizaliwa Agosti 8, 1990 mkoani Morogoro, alipata Shule ya Msingi Kinondoni, Dar es Salaam mwaka1998 – 2004, alijiunga na Mikoji Sekondari na kuishia kidato cha tatu.
Ni mtoto wa kwanza katika familia ya watoto watatu. Kabla ya kuingia katika muziki alikuwa akifanya biashara ya kuuza genge nyumbani kwao na alikuwa akipiga vyombo mbalimbali vya mziki kanisani kwao.
Mbali na muziki Barnabas, anamiliki duka la kuuza nguo lililopo maeneo ya Kinondoni na siku za mwisho wa juma hupenda kutembelea ufukweni.

HATIMAYE EDWARD LOWASA NA ANDREW CHENGE WAWEKWA KITIMOTO

CCM yakiri kuwahoji na Rostam, Lowassa na Chenge  Send to a friend
Saturday, 04 June 2011 10:17
Mwandishi Wetu
CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimethibitisha kwamba kimewahoji Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge ikiwa ni moja ya hatua ya kutekeleza maazimio ya Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho uliofanyika Aprili 10 hadi 11 mjini Dodoma.

Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa CCM, Willison Mukama ilisema kuwa hiyo ni moja hatua za awali zilizochukuliwa na kuongeza kuwa nyingine zitafuata baadaye.

Alisema hatua hiyo ya awali, Makamu Mwenyekiti CCM (Bara), Pius Msekwa alikutana na wanaotajwa katika tuhuma hizo katika sura mbili, kwanza ya nafasi yake ndani ya chama na pia kama mzee wa CCM.

Mukama alisema Mei 26, mwaka huu Msekwa alikutana na Rostam ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na siku Iliyofuata alikutana na Lowassa ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa.

Alisema siku hiyo hiyo ya Mei 27, mwaka huu alikutana na Mjumbe mwingine wa Halmashauri Kuu, Chenge."Kwa vile Msekwa alikutana kwa faragha na viongozi hao mmoja mmoja, hakuna anayejua kilichozungumzwa. Ni Mzee Msekwa na wao peke yao," alisema katika taarifa hiyo.

Alisema hatua itakayofuata baada ya hapo ni kufikisha kwenye vikao vya chama taarifa ya mambo yaliyojiri wakati wa mazungumzo baina ya Msekwa na viongozi hao."Endapo vikao husika vitaamua lolote kuhusiana na taarifa hiyo, umma utajulishwa," alisema.

Katika mkutano huo wa Halmashauri pamoja na mambo mengine, uliwataka viongozi wa CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi kutafakari, kujipima na kuchukua hatua wenyewe kwa maslahi ya chama na kwamba wasipofanya hivyo chama kitawawajibisha

POLISI WATENDEENI HAKI WBUNGE WA VYAMA VYOTE VYA SIASA,MBONA KAMATAKAMATA IPO KWA WAPINZANI PEKE YAO?

Mbowe, Zitto mbaroni  Send to a friend
Saturday, 04 June 2011 22:08
0diggsdigg
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
Waandishi Wetu
MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe jana alitiwa mbaroni na Jeshi la Polisi baada ya kujisalimisha katika kituo Kikuu cha jijini Dar es Salaam.Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe, jana alikamatwa na polisi mjini Singida kwa kosa la kuzidisha muda wa kuhutubia mkutano wa hadhara.Habari zilizopatikana kutoka Singida na kuthibitishwa na Zitto mwenyewe, zinaeleza kuwa polisi walimkamata jana jioni kwa madai kuwa alihutubia mkutano wa hadhara mpaka zaidi ya saa 12:00. Muda wa mwisho kisheria kuhutubia mkutano wa hadhara ni saa 12:00 jioni."Mpaka sasa bado nipo polisi wanaendelea kunihoji," alisema Zitto kwa kifupi.

Hadi tunakwenda mitamboni, Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini alikuwa bado ameshikiliwa katika Kituo cha Polisi mjini Singida.Kukamatwa kwa Mbowe kunafuatia amri ya mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kuamuru akamatwe  popote alipo na kufikishwa mahakamani kwa kutotii amri ya kufika mahakamani katika kesi yake.

 Juni 2 mwaka huu, Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Charles Magesa,  alikubaliana na hoja ya wakili upande wa Serikali kuitaka mahakama kutoa amri ya kukamatwa kwa Mbowe kwa sababu ya kutotii amri ya kufika kortini au kumtuma mdhamini wake.Alisema sababu iliyotolewa mahakamani hapo kwamba mshtakiwa huyo ni mbunge na yupo kwenye vikao vya Kamati za Bunge haina uzito kwa kuwa hiyo ni moja ya shughuli zake kama ilivyo shughuli nyingine kwa watumishi wa Serikali.

Hakimu Magesa akitoa agizo hilo alisema kuwa inachokumbuka ni kwamba mahakama hiyo ilipokea maelezo ya kuwa washtakiwa hawatahudhuria mahakamani hapo Mei 27, mwaka huu na kwa sababu ya kuwapo vikao vya kamati za Bunge iliagiza wafike wadhamini wao kesi inapotajwa. Ndiyo maana Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini, alimpeleka mdhamini.Katika kesi hiyo iliyopangwa kuendelea kusikilizwa kesho, Mbowe na wenzake wanashtakiwa kwa kosa la  kufanya kusanyiko lisilo halali Januari 5, mwaka huu jijini Arusha.

Mjumbe wa Kamati Kuu na Mwanasheria wa chama hicho, Mabere Marando alithibitisha jana kukamatwa kwa Mbowe saa 9:00 alasiri kutokana na amri ya mahakama."Ni kweli amekamatwa saa moja iliyopita kwa sababu ni amri ya mahakama na chama hakiwezi kumwombea dhamana itabidi apelekwe Arusha," alisema Marando.

 Pamoja na Marando kuthibitisha kukamatwa kwa Mbowe, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limesema halina taarifa zozote za kukamatwa kwa mwenyekiti huyo.Jeshi hilo limesema halina taarifa zozote juu ya mwenyekiti huyo kujisalimisha katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam. Mei 27, mwaka huu, mahakama hiyo ilitoa hati ya kukamatwa na kufikishwa mahakamani hapo kwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa na Mwenyekiti wake, Mbowe.

Pamoja na viongozi hao, mahakama hiyo pia iliamuru wabunge wawili wa chama hicho, Phillemon Ndesamburo (Moshi Mjini) na Godbless Lema (Arusha Mjini) wakamatwe na kufikishwa mahakamani baada ya kushindwa kuhudhuria mara kadhaa . Lakini, viongozi hao waliwasiliana na mahakama hiyo.
 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile, alipotafutwa ili kutoa ufafanuzi wa suala hilo hakupatikana kutokana na simu yake ya mkononi kuita bila ya kupokelewa.
Awali asubuhi, akizungumza na gazeti hili ofisini kwake, Kamanda Shilogile alisema kuwa hana taarifa zozote za Mbowe kukamatwa au kujisalimisha katika kituo hicho.

 “Sina taarifa zozote kuhusiana na kukamatwa kwa Mwenyekiti cha Chadema. Taarifa hizi ndiyo nazisikia kwenu waandishi wa habari. Mimi wala uongozi wangu hauna taarifa hizo,”alisema Shilogile na kuongeza;
“Angekuwa amekamatwa au amekuja kujisalimisha mkoa wangu ndiyo ungekuwa wa kwanza kupata taarifa hizo, labda mtafute Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kama ana taarifa hiyo anaweza kukwambia.”Kova alipotafutwa kwa njia ya simu alisema yuko Zanzibar na kwamba hana taarifa zozote za kukamatwa kwa Mbowe.

Marando, Tundu Lissu
Mapema asubuhi Marando na  Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu walionekana wakiingia katika Ofisi ya Mpelelezi wa Mkoa wa Ilala (RCO),  Diwan Nyanda.Alipoulizwa ujio wake katika ofisi hizo, Marando alisema kuwa alikwenda katika ofisi hizo kwa shughuli zake binafsi na kwamba hana taarifa za kukamatwa kwa Mbowe.

Akizungumza na Mwananchi Alhamisi wiki hii baada kutolewa amri ya kukamatwa kwake, Mbowe alisema anatarajia kutoa tamko kuhusu suala hilo Ijumaa jijini Dar es Salaam.“Nitatoa tamko kesho, lakini nasikitishwa na tafsiri hii ya Mahakama kwamba mimi nimekaidi amri ya kufika katika vikao vya mahakama...,” alisema Mbowe

Mnyika
Katika hatua nyingine Mbunge wa  Ubungo, John Mnyika (Chadema) amesema chama hicho kitaandika barua rasmi katika Ofisi za Bunge kueleza jinsi wabunge wa vyama vya upinzani wanavyokamatwa bila kufuata kanuni na taratibu, wakati wana kinga ya kibunge inayowazuia kukamatwa bila kibali.

Alisema mpaka sasa wabunge wa upinzani ambao wamewahi kukamatwa bila kuombwa kwa kibali chochote kutoka kwa Spika wa Bunge ni pamoja na Godbless Lema (Arusha Mjini), Phillemon Ndesamburo (Moshi Mjini), Joseph Selasini (Rombo), Meshack Opulukwa (Meatu)Wengine ni Tundu Lissu (Singida Mashariki), Esther Matiko (Viti Maalumu-Chadema) na Magdalena Sakaya (Viti Maalumu-CUF) ambaye mpaka sasa yuko mahabusu mkoani Tabora huku kesi yake inatarajiwa kutajwa Juni 6 mwaka huu.

Imeandikwa na Hadija Jumnne, Fidelis Butahe na Edward Qorro