Monday, December 17, 2012

UKAHABA UDOM NI AIBU KWA TAIFA LA TANZANIA

by Alex Nicholaus Thomas Mushi .


Kwa dhati ya moyo wangu nimesikitishwa sana na taarifa zilizozagaa kwenye vyombo vya habari kuhusu kujiuza kwa dada zetu wa UDOM. Wasomi ambao wana Dodoma na watanzania kwa ujumla walitegemea kujifunza kutoka kwao. Taarifa hizi zimenichochea kukaa chini na kuandika waraka huu huku nikizingatia ukweli kwamba UDOM ndipo nilikosomea masomo yangu ya shahada ya kwanza; mbali na matatizo yote yaliyonikumba katika safari hiyo ya kukamilisha shahada hiyo lakini nalazimika kusema kitu kwa faida yetu wote.

Ikumbukwa moja ya mategemeo ya jamii ya wana Dodoma kutoka kwenye chuo cha UDOM kilipo anzishwa mwaka 2007 ilikuwa ni kujionea jamii staarabu iliyoelimika na yenye kila sifa ya kuigwa, na pia jamii ya Dodoma ilitegemea watoto wao wangejionea namna wasomi hawa wanavyoishi kwa kusadifu kwa vitendo elimu, maadili na mila za nchi yao. Zaidi waliamini mambo hayo yangekuwa chachu ya kuwachochea vijana wao kuzingatia masomo ili na wao siku moja wafikie elimu hiyo ya Chuo lakini hali imekuwa tofauti kabisa. Leo jamii hii ya wana Dodoma wanashuhudia wasomi wanaoshinda mitaani wakiranda randa na nguo za kuogelea na za kulalia kana kwamba walikotoka hakuna wazazi, wanashuhudia wasomi wanaojiuza kama njugu.

Kiukweli siwezi hata siku moja kuruhusu kulea au kuipamba tabia hizo hata kama kuna sababu za msingi ambazo zinaweza zikawa zimesababisha tatizo hili kutokea. Kinachofanywa na dada zetu hawa ni kitendo ambacho kila mungwana anapaswa kukikemea kwa nguvu, na zaidi ya yote ni wajibu wetu wote kama vijana kurudia maadili yetu kama watanzania na kulaani kwa nguvu haya. Kama tutaruhusu tabia hii ikaota mizizi tutaandaa wasomi wasio waadilifu na wasio jiamini, tutandaa wasomi wenye shahada za kwenye chupi (nisamehewe kwa hiyo lugha lakini nimekosa neon linalokidhi ninachomaanisha),tutandaa wasomi walioathirika hivyo kupoteza nguvu kazi ya taifa, tutaandaa taifa la wavivu na wasifikiri kwa ufanisi.

Tukumbuke kuruhusu tabia hii kubobea ni kuruhusu kuporomoka kwa elimu ambayo ni msingi wa taifa lolote duniani. Na sidhani kama ni busara kuangalia umauti wa taifa letu kwa kuruhusu tabia hii kuota mizizi, kwani dhambi hiyo haitaishia chuoni tu, itaingia makazini na hapatakuwa na kazi zaidi ya uzinzi tu, baada ya hapo dhambi hii itasambaaa hadi kwa watoto na wajukuu wetu na hatimaye itakuwa ndio mfumo wetu wa maisha. Lakini mbali na yote niliyoeleza hapo juu ninayo yangu kwa serikali yangu, vijana hawa wa UDOM ni watoto wenu na wengine wameingia pale wakiwa hawana hata elimu ya kimaisha au ya kujitegemea, wengine wanakutana na kila aina ya tabia pale.

Mimi nilisha kuwa kiongozi wa mikopo UDOM-HSS kwa karibu miaka yote ya masomo yangu ya shahada ya kwanza, naelewa kiasi sababu na wakati dada zetu hawa wanapojiuza. Kipindi ambacho dada zetu hawa hujiuza huwa ni pale Bodi ya mikopo inapochelewesha mikopo ya wanafunzi, hali huwa mbaya kiasi dada zetu hawa ufika mahali wanalazimika kujidhalilisha ilimradi wapate chochote cha kujikimu. Na ukizingatia majumbani kwao hawa msaada wowote wanaoupata.

Mfano mzuri wa ucheleweshaji wa mikopo kwa wanafunzi wa kozi ya Uhusiano wa Kimataifa (BA IR) hawajapewa mikopo yao mpaka leo, na wanatakiwa kula, kunywa, kuwasiliana na kununua vitini vya masomo ili hali familia walizotoka ni masikini wa kutupwa. Haya yote ni mazingira hatarishi kwa dada zetu hawa. Serikali kama mzazi nakuomba mliangalie kwa umakini sana suala hili ili tuwaepushie wale wanajihusisha na tabia hii ya kuuza miili yao kutokana na kuishiwa au kukosa fedha za kujikimu Muda mwingine unaweza kusema serikali inafanya makusudi kuwacheleweshea mikopo yao wa sababu wanaonufaika sana na tabia hiyo ya dada zetu kujiuza ni wabunge wanapokuja kwenye vikao vyao vya bunge.

Kujiuza kwa dada zetu hawa ni dhahiri ni matokeo ya mambo kadhaa ambayo serikali haina budi kuyafuatilia kwa kina na hatimaye kutatua kwa ustawi wa tafa letu la Tanzania. Hatupaswi kufurahia tabia hii hata kidogo kwan kufanya hivyo kunaweza liathiri taifa letu kwa ujumla wake siku za usoni.

……………“ukiona panafuka moshi ujue kuna moto”…………

MTOTO KUMKOSOA BABA HARDHARANI INA MAANA GANI?WATENDAJI WA SERIKALI WAMEWEKWA NA CCM, HIVYO KUSHIDWA KWAO NDIO KUSHIDWA KWA CCM





Viongozi wa CCM mkoa Njombe wakishirikiana na makamu mwenyekiti wa CCM Taifa Phili Mangula ( wa pili kulia ) kuwaongoza wanachama wapya wa CCM zaidi ya 600 waliojiunga na CCM jana wakati wa mapokezi ya makamu huyo wa kwanza kulia ni mbunge wa jimbo la Njombe kusini na spika wa bunge Anne Makinda wa tatu kutoka kulia ni mwenyekiti wa CCM mkoa wa Njombe Deo Sanga ambae ni mbunge wa jimbo la Njombe kasikazin na anayefuatia ni katibu wa CCM mkoa wa Njombe Hosea Mpangike




Deo Filikunjombe miongoni mwa wananchi









Msafara wa pikipiki kwenye mapokezi ya Mangula Njombe

Picha na Said Ng'amilo wa Mjengwablog







Habari na Francis Godwin


MBUNGE wa jimbo la Ludewa mkoani Njombe Deo Filikunjombe awakuna wapiga kura wa jimbo la Njombe Kaskazini Linaloongozwa na mbunge wake Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Njombe Deo Sanga Kwa kuwalipua watendaji wabovu serikalini ,mbele ya makamu mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi ( CCM) Tanzania bara Philip Mangula.


Filikunjombe ambea alipewa nafasi ya kusalimia katika mkutano huo mkubwa wa mapokezi ya Mangula mkoani Njombe alisema kuwa masikitiko ya wananchi juu ya serikali ya CCM yanatokana na baadhi ya viongozi wabovu ndani ya Chama na serikalini ambao wamekuwa wakifanya kazi chini ya kiwango na kupelekea wananchi kukichafua Chama tawala.


" Ndugu zangu wananchi wa Makambako na mkoa wa Njombe Chama chetu CCM ni Chama kizuri sana na safu hii ya sasa chini ya Rais Kikwete ,Kinana na Mangula ni safu ya uhakika na itakiwezesha Chama chetu kuendelea kuaminiwa zaidi na watanzania ...ila tatizo ni viongozi wachache wa serikali wasiowajibika katika nafasi zao"kauli iliyowakuna wananchi na kushindwa kujizuia kushangilia huku wakiimba wewe ni Jembe .


Hata hivyo Filikunjombe alisema kuwa ili Chama kuendelea kupendwa na akina Mangula na Kinana wanapaswa kusaidiwa na watanzania wote kwa kuombewa zaidi ili kuendelea kuifanya kazi hiyo bila woga ndani ya chama.


Kwa Upande wake Mangula mbali ya kusifu mapokezi makubwa ya kihistoria Katika mji wa Makambako na Njombe mkoani Njombe aliweza kutoa ya Moyoni kuhusu Kati yake na Rais Jakaya Kikwete kwa Madai kuwa yeye alikuwa hajui chochote juu ya uteuzi wake na kuwa alisitaajabu kupokea simu ya Kikwete kuhusu kusudio la uteuzi wake.


" Kweli Mimi nilikwenda Dodoma katika mkutano mkuu wa CCM Kama mualikwa ila Nikiwa Hotelini nilipokea simu ya mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Kikwete akiomba kuniteua kuwa makamu mwenyekiti na baada ya kwenda Ukumbini wajumbe wote walinipa kura zote za ndio...kweli namshukuru sana mwenyekiti wangu na wanachama wote na sasa ni kazi zaidi na sitawaangusha"


Hata hivyo aliwataka wana CCM kufanya vikao bila kuchota na kuwa wasizingizie kukosa ajenda kwani hata kukosa ajenda ndani ya CCM ni ajenda Kukosa agenda pia ni agenda ndani ya CCM pia yaweza kuwa ajenda.


Aidha amehimiza nidhamu na taratibu ndani ya CCM kuendelea kuzingatiwa ili kukiwezesha Chama kuwa na amani na kuwa iwapo taratibu ndani ya Chama hazitazingatiwa upo uwezekano wa Amani ndani ya nchi kutoweka.


Alisema kuwa haitapendeza kuona Tanzania inafika mahali inaendeshwa bila Chama iwapo tutaruhusu wasiopenda Amani kuendelea kuvuruga Amani yetu iliyopo...