Sunday, June 10, 2012

NAPE ASHIDWA KUKANUSHA MADAI YA CHADEMA KTK VIWANJA VYA CHADEMA-SQUARE

Saturday, 09 June 2012 08:13
0digg
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye
Dotto Kahindi na Leon Bahati
KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye amesema chama chake hakina mpango wa kuutumia mkutano wake wa leo kwenye Viwanja vya Jangwani kujibizana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na badala yake, kitajikita zaidi katika kutoa somo kwa wajumbe wapya wa mashina na viongozi wa matawi Mkoa wa Dar es Salaam.

Kauli hiyo ya Nape inatoa mtazamo tofauti na tetesi kwamba  CCM kitatumia mkutano huo kukijibu chama hicho kikuu cha upinzani ambacho nacho kilifanya mkutano kwenye viwanja hivyo hivi karibuni.
Katika mkutano huo ambao Chadema kilizindua Mpango wake wa Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) mwishoni mwa mwezi uliopita, kiliorodhesha shutuma nyingi dhidi ya Serikali ya CCM zikiwemo za kusababisha maisha magumu kwa Watanzania.

Nape alisema mkutano huo uliandaliwa na CCM Mkoa wa Dar es Salaam hata kabla ya huo wa Chadema na lengo lake ni kuwakutanisha viongozi wapya wa chama hicho tawala na viongozi wa juu wa chama na Serikali, wakiwemo mawaziri watakaofafanua shughuli zao za kiutendaji.
“Mkutano huu unalenga kuwafundisha wajumbe wa nyumba kumi na viongozi wa mashina waliochaguliwa hivi karibuni namna ya utendaji wa Serikali, kwa kuwa wao bado ni  wapya kiuongozi na wanahitaji kupewa somo,” alisema Nape.

Alipoulizwa kama mkutano huo ni moja ya hatua za kufuta nyayo za Chadema hasa baada ya kuzindua M4C, Nape alisema: “Mkutano huu tuliuandaa mapema kabla hata ya Chadema hawajafanya mkutano wao. Ila kilichochelewesha ni Mkutano wa Halmashauri Kuu (Nec) ya CCM,” alisema Nape na kuongeza:

“Mkutano huu awali, ulikuwa ufanyike ndani ya ukumbi lakini kwa kuwa watu wengi walipenda kushiriki tumeamua kuufanyia Jangwani ambako wanachama na viongozi wa CCM watapata fursa ya kusikia sera za viongozi wa chama na watendaji wa Serikali.”

Aliwataja mawaziri ambao watakuwa katika mkutano huo kuwa ni pamoja na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ambaye atazungumzia masuala ya usafiri wa reli, bandari na anga na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli ambaye atazungumzia masuala ya miundombinu na barabara.

Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira ambaye atazungumzia hatima ya Watanzania katika masuala ya ajira na vijana na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba ambaye atazungumzia mipango ya wizara yake.

M4C
Mei 25 mwaka huu, Chadema kilizindua mkakati wake mpya wa ‘Movement For Change-M4C’ ukiwa na lengo la kukiandaa chama hicho kushinda Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliwataka wanachama na wananchi kwa ujumla kukichangia fedha chama hicho ili kufanikisha kampeni aliyoielezea ni ya kukiondoa CCM madarakani mwaka 2015.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa alisema maisha ya Watanzania si mazuri, vyakula vinaongezeka bei kutokana na Serikali ya CCM kutokuwa makini hivyo akawataka wabunge wa chama hicho kuibana kupitia Bunge lijalo la Bajeti.

Aliilaumu Serikali kwa kutotumia vizuri kodi za Watanzania kwa ajili ya shughuli za maendeleo kwa kuwalipa watumishi ambao nafasi zao hazina manufaa kwa wananchi.
Dk Slaa alilalamikia kitendo cha kuongeza kodi katika mafuta ya taa ili watu wasichakachue mafuta ya dizeli akisema ni mwiba kwa Watanzania.

R.I.P BOB MAKANI, TUTAUENZI MCHANGO WAKO KATIKA KUPIGANIA DEMOKRASIA NA MAENDELEO NCHINI TANZANIA


 Send to a friend
Sunday, 10 June 2012 09:38
0digg
Mzee Bob Makani
Na Mwandishi Wetu
MWASISI wa Chadema na Mwanasheria mkongwe nchini Bob Makani, amefariki dunia usiku katika hospitali ya Aga khan, jijini Dar es Salaam.

Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe, Makani alizidiwa ghafla saa 3: 00 usiku wa kuamkia leo na kukimbizwa katika Hospitali ya Aga Khan ambako alifariki dunia saa 4.15 usiku.

“Amekuwa anaumwa muda mrefu, mara kadhaa akipelekwa hospitali na baada ya muda anaruhusiwa, lakini hii ya sasa alikua nyumbani akazidiwa ghafla wakampeleka hospitali na ilipofika saa 4.15 wakasema amefariki,” alisema Zitto.

Zitto alisema kuwa, suala la wapi utakapozikwa Makani ambaye ni Katibu Mkuu wa Kwanza na Mwenyekiti wa pili wa Chadema, litajulikana baada ya kujadiliana na familia ya marehemu.

“Suala la wapi atazikwa kama ni Shinyanga ama Dar es Salaam, litajulikana baada ya kuzungumza na familia yake, kwa sasa tunashughulika kwanza na kuhifadhi mwili wa mzee wetu,” alisema Zitto.
Zitto alisema msiba wa utakuwa nyumbani kwa marehemu eneo la Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.

Kwa siku za hizi karibuni afya yake imekuwa ikizorota na kumfanya kuripotiwa kuanguka mara kwa mara alipokuwa akifanya shughuli zake.

Januari 17 mwaka huu katika msiba wa aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum wa Chadema Regia Mtema, Makani alianguka muda mfupi baada ya kuuaga mwili wa marehemu.

 Baada ya tukio hilo, alibebwa na kupelekwa pembeni ambako alipepewa kwa takriban dakika tano kisha kurejea katika hali yake ya kawaida na kurudi kwenye kiti chake

Alikuwa Katibu Makuu wa kwanza wa Chadema kati ya mwaka 1993 hadi 1998, alikuwa Mwenyekiti wa chama hicho kuanzia mwaka 1998 hadi 2004 na amegombea ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini kwa mara tatu kati ya mwaka 1995 na 2000 na mwaka 2005.

Kazi ambazo amewahi kuzifanya serikalini; alikuwa naibu mwanasheria mkuu wa serikali, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) mwaka 1966 na elimu yake ana shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu Cha Makarere nchini Uganda.

Ni mzaliwa wa Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga akitokea kwenye ukoo wa kichifu wa Makani.