Wednesday, March 16, 2011

WASICHANA WALOICHANA PAPER WAPATA NAFASI SHULE ZA A-LEVEL

WASICHANA WALOICHANA PAPER WAPATA NAFASI SHULE ZA A-LEVEL  Send to a friend
Thursday, 17 March 2011 07:52
0diggsdigg
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa
Fredy Azzah
WASICHANA wote waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2010 na kufaulu kwa kupata daraja la I mpaka la III (Division One mpaka Three), wamepata nafasi za kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya Serikali, huku wavulana waliopata nafasi hiyo wakiwa ni asilimia 97. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alisema wanafunzi wote hao wanatakiwa kuripoti katika shule walizopangiwa Aprili tatu mwaka huu kuanza masomo.
Kwa mujibu wa Dk Kawambwa, wanafunzi waliokuwa
na sifa za kuchaguliwa kujiunga na kidato cha tano pamoja na vyuo vya ufundi ni 36,990 wakiwamo wasichana 11,210 na wavulana 25,780.
“Wanafunzi 36,366 ambao ni asilimia 98.31 ya waliokuwa na sifa stahili wamepangwa kidato cha tano na vyuo vya ufundi, kati yao wasichana ni 11,210 sawa na asilimia 100 ya wenye sifa na wavulana ni 25,156 ambao ni asilimia 97.58 ya wanafunzi wenye sifa,” alisema Dk Kawambwa.
Wanafunzi wa kike waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano pamoja na vyuo vya ufundi ni asilimia 30.83 ya wanafunzi wote 36,366 waliopangwa.
Mwaka 2010 wanafunzi wa kike 12,638 walichaguliwa kuendelea na masomo, ikiwa ni asilimia 42.33 ya wanafunzi wote.
Kutokana na hali hiyo, idadi ya wanafunzi wa kike waliochaguliwa kuendelea na kidato cha tano na vyuo vya ufundi mwaka huu, ni pungufu ya wanafunzi 1,428 ukilinganisha na ile ya mwaka jana.
Kwa ujumla, wanafunzi waliopangiwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ufundi mwaka jana, walikuwa 33,662. Wasichana walikuwa 12,638 na wavulana 21,024.
Hata hivyo, Dk Kawambwa alisema mwaka 2010 wanafunzi waliochaguliwa walikuwa asilimia 83.52 ya wenye sifa, hivyo mwaka huu kuna ongezeko la asilimia 12.63, kwa awamu ya kwanza.Alisema wavulana 624 sawa na asilimia 2.42, hawakuchaguliwa kuendelea na masomo ya kidato cha tano na vyuo vya ufundi kutokana na sababu mbalimbali.
Alizitaja sababu hizo kuwa ni kutokuwa na uwiano wa alama za masomo (credits), alama kutotimia na baadhi kuwa na umri wa zaidi ya miaka 25.
Alisema wanafunzi 29 walikuwa na umri uliozidi miaka 25 ambao kisheria hauwaruhusu kuchaguliwa kujiunga na kidato cha tano kwa shule za Serikali.
Wanafunzi wengi wa kike wamepangwa kusoma masomo ya Historia, Jiografia na Kiingereza (HGL), kati ya wote waliochaguliwa wanafunzi 1,610 sawa na asilimia 14.4 walichagua masomo hayo.
Alisema wanafunzi 1,593, watasoma CBG; 1,574 watasoma HKL, 1,472 watasoma PCB, 1,108 watasoma HGK na wanafunzi 1,035 watasoma HGE.
Kwa upande wa wavulana, wanafunzi wengi wamechaguliwa kusoma masomo ya sayansi. 4,307 sawa na asilimia 17.1 watasoma PCM; 4,177 sawa na asilimia 16.6 wakichaguliwa kusoma PCB, 3,079 HGL, 2,722 HGK, 2,504 HKL na wanafunzi 2,249 wakichaguliwa kusoma CBG.
Wanafunzi 916, wasichana wakiwa 55 na wavulana 861 wamechaguliwa kujiunga na mafunzo ya vyeti katika vyuo vya ufundi vya Mbeya (MIST), Dar es Salaam (DIT), Arusha (ATC) na Chuo Maji Dar es Salaam.
Kutokana na hali hiyo, wanafunzi wa kike waliochaguliwa kusoma masomo ya sayansi na vyuo vya ufundi mwaka huu ni  4,357 ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 195, ikilinganishwa na wanafunzi 4,162 waliochaguliwa kusoma masomo hayo mwaka jana.
Kwa upande wa wavulana, idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kusoma masomo hayo mwaka huu imeongezeka kwa asilimia 25.9, kutoka wanafunzi 12,664 waliopangiwa kusoma masomo ya sayansi ikilinganishwa na mwaka jana ambapo wanafunzi 10,057 ndio waliochaguliwa kusoma masomo hayo.
Pia idadi ya wanafunzi hao waliopangiwa kusoma sayansi ni asilimia 50.3 ya wanafunzi wote wa kiume waliochaguliwa kuendelea na kidato cha tano na vyuo vya ufundi.
Katika hatua nyingine, Waziri Kawambwa alisema wanafunzi 624 wenye sifa ambao hawakuchaguliwa kujiunga na kidato cha tano au vyuo vya ufundi, bado wana nafasi za kuendelea na masomo hayo kwa kujiunga na shule za sekta binafsi.
Dk Kawambwa pia alieleza kuwa wanafunzi ambao bado Baraza la Taifa Mitihani (Necta), halijatangaza matokeo yao, pindi yatakapotoka na kama watakuwa na sifa zinazotakiwa, watachaguliwa kujiunga na shule au vyuo vya ufundi.
Dk Kawambwa aliwataka wakuu wa shule zisizokuwa za Serikali kuwasilisha majina ya wanafunzi wa kidato cha tano waliojiunga na shule zao ili kuiwezesha  wizara yake kuwa na kumbukumbu sahihi.
Waziri huyo alitoa angalizo kuwa mtindo wa wazazi kuomba uhamisho wa watoto wao kabla ya kuripoti katika shule walizopangwa, safari hii hautakubaliwa kwa kuwa wizara hiyo imewapanga wanafunzi katika shule walizoomba.

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
Last Updated on Thursday, 17 March 2011 08:05
 

Comments 

 
0 #1 ANOLD MADANDI 2011-03-17 08:42
ushauri toeni nafasi kwa wavulana na wasichana wafanye mitihani tena ili waweze kuongezwa ktk vyuo vya ufundi vilivyoko hapa inchini kwani wanahitajika sana nchini iwe na wataalam wengi ahsante
Quote
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!

No comments:

Post a Comment