Thursday, March 17, 2011

HOJA ZA ZITTO KABWE KUHUSU UGUMU WA MAISHA TANZANIA

Zitto airarua serikali
•  Abeza Rais kulalamikia matatizo badala ya kuyatatua

na Bakari Kimwanga

MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Zitto Kabwe, ameitaka serikali ichukue maamuzi ya haraka ya kulinusuru taifa na tatizo la umeme nchini, kwani uzoefu unaonyesha ndiyo imekuwa ikichelewesha na wakati mwingine kukwamisha uwekezaji wa miradi mikubwa ambayo ingeweza kulipatia taifa umeme wa uhakika.
Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni (CHADEMA), aliyasema hayo wakati akisoma ripoti ya mapendekezo ya kamati yake kuhusu tatizo la umeme, ambayo kwa kiasi kikubwa imeonyesha kuwa uzembe na urasimu ndani ya serikali umechangia kwa kiasi kikubwa taifa kukosa umeme wa uhakika na kujikuta likiingia gizani mara kwa mara.
Akisoma maazimio hayo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, alilitaka Baraza la Mawaziri chini ya Rais Jakaya Kikwete kufanya maamuzi ya haraka ili kukamilisha miradi ya umeme wa makaa ya mawe ya Liganga na Mchuchuma, aliyosema ina uwezo wa kuzalisha umeme wa kutosha na wa uhakika.
Alisema wakiwa katika ziara ya siku tano ya kukagua mradi wa Liganga na Mchuchuma, walibaini kuwa ipo haja ya haraka kwa serikali kutimiza wajibu wake kufanikisha utekelezwaji wa haraka wa miradi hiyo na kwamba wanaunga mkono hatua zilizofanywa na Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) kwa kukamilisha hatua za kumpata mbia kutoka nchini China.
Alisema kukamilika kwa miradi hiyo kutaifanya nchi inufaike kwa kupata umeme wa Megawati 1500 KV ndani ya kipindi cha miaka mitano na kuendelea, ambao unaweza kuzalishwa kwa takriban miaka 150 kabla ya makaa ya mawe kwisha.
“Hatuwezi kuwa na taifa la walalamikaji kila mara…. rais, wabunge na wananchi wote sasa tumekuwa walalamikaji lakini muhimu ni kwa baraza la mawaziri kufanya uamuzi wa haraka ili kuinusuru nchi na tatizo la umeme.
“Hata kampuni tanzu itakayoundwa ili kuendesha miradi hii ifuate taratibu zote za uchimbaji ikiwamo kusainiwa kwa mkataba wa uendelezaji wa mgodi kwa madhumuni ya kulinda masilahi ya taifa na watu wa Ludewa,” alisema Zitto.
Alisema NDC wameingia ubia na Kampuni ya Atomic Resources ya Australia na kuunda Kampuni tanzu ya TANCOAL Energy wilayani Mbinga kwa lengo la kuzalisha umeme wa megawati 450, ambapo shirika hilo litakuwa na hisa ya asilimia 30 na uwekezaji wake utakuwa ni dola za Marekani milioni 350.
“Mkataba wa ubia kati ya NDC na Kampuni ya Sichuan Honga kutoka nchini China ili kuendeleza mradi wa Mchuchuma na Liganga ni vema ukasainiwa haraka na serikali,” alisisitiza Zitto.
Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), alisema Wizara ya Nishati na Madini inatakiwa kuharakisha utoaji wa leseni ya uchimbaji wa makaa ya mawe kama ilivyokuwa imeombwa na Kampuni ya TANCOAL ambayo inamilikiwa kwa ubia na NDC ili uchimbaji huo uanze na umeme uzalishwe.
Kwamba, umefika wakati kwa TANESCO kuanza kuwekeza katika msongo wa kusafirisha umeme kuelekea kwenye miradi hii ili iwe ya maana, ikiwa ni pamoja na suala la msongo wa umeme kuwa chini ya TANESCO.
Akifafanua kuhusu mradi wa umeme wa makaa ya mawe wa Kiwira, alisema kamati yake inaunga mkono hatua ya mashirika ya umma kuwekeza katika sekta ya uzalishaji wa umeme na Shirika la Hifadhi ya Jamii nchini (NSSF), kujitokeza kuendesha mgodi huo.
“Kamati yetu mwaka 2009 ilikwenda nchini Malaysia na kukuta mashirika ya mifuko ya hifadhi za jamii yamewekeza na kuzalisha umeme megawati 27,000 huku wakiwa na akiba ya megawati 12,000 ya umeme katika nchi yao, je, Tanzania tunasubiri nini?” alihoji Zitto.
Alisema kamati hiyo itakuwa na mkutano na wadau wa kujadili miradi ya umeme ambapo mkutano huo utawakutanisha NDC, STAMICO, TANESCO,NSSF na CHC pamoja na makatibu wakuu wa wizara na wenyeviti wa kamati za Bunge za Viwanda, Biashara, Nishati na Madini ili kujadiliana kwa pamoja na kupata njia mbadala zaidi.
Akijibu maswali, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Deo Filikunjombe, alisema kamati yao imefuatilia na kubaini kuwa mchakato wa kurejesha umiliki wa mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira na kubaini kuwa mchakato huo bado haujakalimika kama ilivyokuwa imeelezwa awali.

No comments:

Post a Comment