Saturday, March 19, 2011

KANISA KATORIKI HAIFUSIANI NA CHADEMA

KANISA KATORIKI HAIFUSIANI NA CHADEMA  Send to a friend
Saturday, 19 March 2011 09:37
0diggsdigg
Israel Mgussi, Dodoma
RAIS wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Mkuu Yuda Thadeus Ruwa'ichi amewaponda wanasiasa wanaotaka kuwafumba mdomo viongozi wa dini nchini wanaokemea rushwa, ufisadi na ukiukwaji wa maadili unaofanywa na baadhi ya viongozi waandamizi wa Serikali na vyama vya siasa.Ruwai'chi ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Kanisa Katoliki, Mwanza pia amewajia juu wanaolihusisha kanisa hilo na ustawi wa Chadema akisema kuwa huo ni uzushi na kuwanyooshea kidole baadhi ya wanaCCM na baadhi ya waandishi wa habari aliosema hawapendi kuchanganua mambo na kuwa na uhakika nayo.

Askofu Ruwai`chi (pichani) alisema Kanisa Katoliki halikiteulii chama chochote cha siasa mgombea na akakipa angalizo CCM akitaka kijidodose juu ya sababu zilizomfanya Dk Willbrod Slaa kukihama na sasa kuonekana kama ni mtu anayekichanganya akili na kutaka iache alichokiita propaganda zenye malengo ya kuwagawa watu katika misingi ya dini.

“Kama Slaa (Dk Willbroad Slaa) alikuwa mwanaCCM akaikimbia. Sasa jifunzeni na kukumbuka historia, CCM wana mchango gani katika hilo la Dk Slaa kuikimbia, wakijibu swali hilo itakuwa vizuri sana," alisema akisisitiza.Askofu Ruwai'chi alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Parokia ya Kibaigwa, Dodoma muda mfupi baada ya kumpokea Askofu mteule wa Jimbo Katoliki la Dodoma, Mhashamu Gervas Nyaisonga ambaye atasimikwa rasmi leo mjini Dodoma.

Kuhusu Kanisa Katoliki kudaiwa kuwa limekuwa likikiunga mkono Chadema, Askofu Ruwai'chi alisema kuwa hakuna ukweli wowote kuhusu uvumi huo na kwamba kauli hizo zimekuzwa na baadhi ya wanaCCM ambao wamekosa sera na kukurupuka kutoa kauli zisizo za msingi.

“Hizo ni kauli danganya toto, Kanisa halina chama, ila likibidi kuzungumza litazungumza kama lilivyokuwa likifanya kwa maslahi ya watu wote. Viongozi wa dini wasipozungumza watakuwa hawalitendei haki taifa, wanapaswa kusimamia haki pale inapoonekana kupotoshwa, kanisa halina chama," alisema Askofu huyo.Alisema Chadema ni chama chenye mkusanyiko wa watu wa dini na madhehebu yote, hivyo watu watumie akili zao kutafuta ukweli wa uvumi huo aliosema ni wa kupotosha.

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki nchini alisema kila mtu ana wajibu wa kuhakikisha kwamba Tanzania inakuwa njema. Akaeleza kushangazwa kwake na wachache wanaotaka kupandikiza mbegu ya udini ambayo alisema kimsingi haipo nchini.

Alisema kauli kama hizo alizoziita za kichochezi pia zinajenga swali kuwa, huenda CCM ni chama cha watu fulani, lakini akasema kuwa wao viongozi wa dini na kanisa kwa ujumla kazi yao ni kuhakikisha maslahi ya taifa hayachezewi wala hayaendi kiholela, akisisitiza kuwa ni haki ya kila mtu kuwa na mtazamo tofauti wa kisiasa muhimu asivunje sheria.
Huku akisisitiza kuwa Tanzania haiendeshwi katika misingi ya falsafa za kidini wala madhehebu, Askofu Ruwai'chi alisema kuwa viongozi wa dini zote nchini wanapaswa kuzungumza na kukemea dosari za kiutendaji na kiuwajibikaji zinazofanywa na baadhi ya viongozi na watumishi wa umma na kwamba bila hivyo itakuwa ni kutowatendea haki Watanzania.

Alisema viongozi wa dini wanapaswa kuzungumzia matatizo yaliopo nchini, kuhamasisha haki, ukweli, amani na kushughulikia maendeleo ya watu wote bila kuogopa wanaowabeza na kutaka kuwaziba midomo kwa kisingizio kuwa wanaingilia Serikali.

“Kuzungumza siyo kuingilia, viongozi wa dini wana wajibu wa kutoa kauli na kuwashuhudia watu mambo mbalimbali yanayotokea katika nchi, wasipoongea watakuwa hawalitendei haki Taifa,” alisema Askofu Mkuu Ruwai'chi.
Askofu Ruwaichi alisema kuwa viongozi wa dini mbali na kutunza dini, lakini wana wajibu mkubwa wa kusimamia mustakabali wa taifa kwa kuhakikisha wanakemea na kusemea mienendo ya kiovu ambayo kwa namna moja au nyingine, inaweza kuvuruga amani na umoja wa kitaifa.

Askofu mteule Nyaisonga atasimikwa leo katika Kanisa Kuu la Paulo wa Msalaba Mjini Dodoma na Rais Jakaya Kikwete pamoja na Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa na viongozi wengine wa dini na madhehebu mbalimbali wanatarajiwa kuhudhuria.
Juzi, mamia waumini wa Kanisa katoliki walijitokeza na kuandamana kwa ajili ya mapokezi ya askofu huyo mteule aliyewasili majira ya saa 7:00 mchana Kibaigwa, Dodoma akitokea Mbeya ambako alikuwa akitumika katika shughuli za kitume akiwa Padri Daraja la Pili.


Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
Last Updated on Saturday, 19 March 2011 09:46
 

Comments 

 
0 #7 elibariki yerald 2011-03-19 11:01
umenena baba askofu..nawapenda viongozi wa dini kama ninyi mnaochana ukweli bila kumung'unya,,na akija leo mhuyo jamaa.mumwambie kwa msisitizo zaidiiiiiiiiiii iii
Quote
 
 
+1 #6 yamasoft 2011-03-19 11:01
Naam, askofu umesema kweli, nafikiri umefika wakati wananchi kutanzua kwa akili zetu bila kuyumbishwa na wanaopandikiza mbegu ya udini katika mambo mbalimbali. Kwa mtazamo wangu CCM wanapaswa kutambua ndani ya vyama vya siasa kikiwamo chenyewe kuna watu wana imani zao tofauti lakini hoja ni kutenganisha shughuli za dini na siasa! Shughuli za siasa zikifanya na mtu mwenye imani furani ni wajibu wao kutambua anasimama pale kama mwanasiasa na si mwana dini furani! Tukumbuke ikiwa tutasahau hili na nje ya hapo hata CCM nayo itakuwa na udini! Watanzania wenzangu akili za kuambiwa tuchanganye na za kwetu! Haipaswi kuliruhusu swala la udini liwe chanzo cha watu wachache kuficha uozo wao wakitutaadhalis ha tukisema tutakuwa na udini! Maendeleo ni matam kwa watu wa dini zote, hivyo pale yanapoitaji kuyapigania ni wajibu wetu sote tukemee hata kama wanaofanya uozo ni wafuasi wa dini zetu!
Quote
 
 
+1 #5 J.G.Z 2011-03-19 10:55
tutafika tu tunapotaka kwenda, lakini sharti la kwanza lazima tumalize hizi changamoto zilizopo mbele yetu.
Quote
 
 
0 #4 Katiba TANGANYIKA 2011-03-19 10:45
Angalau tutapumua sasa!

Tulichoka na mambo ya loliondo. Haya ndio mambo yenyewe, tuendelee na ujenzi wa taifa tuwabane MAFISADI
Quote
 
 
+3 #3 itondo 2011-03-19 10:26
Yangu ni machache tu: Kwa hii hoja ya udini iliyopandikizwa na CCM dhidi ya CHADEMA wakitegemea support ya wananchi kiukweli itawamaliza wao CCM; ni suala la muda tu. CCM hawakujua unaposema CHADEMA (au chama kingine chochote) kina udini, unamaanisha wewe (CCM) pia una-suuport ya hao wa dini nyingine. Hii inaonesha jinsi viongozi wa CCM wanavyokurupuka na kutoa kauli bila kupima athari za kauli hizo. Wao ni ku-focus short term political success. Hii ni hatari.
Quote
 
 
+3 #2 mtanzania hai 2011-03-19 09:59
Hapo ni ukweli Padri anachosema; CCM waache kumtafuta mchawi kwa kuingiza udini kama kimbilio la kukiandama CHADEMA; sera zao za kubebana, undugu, ufamilia, ufisadi, kujuana, urafiki etc katika kuendesha serikali ndio unaowafanya washindwe kufurukuta kwa CHADEMA. Watanzania wa sasa sio wale wa mwaka 1977 wana upeo tofauti sana, wanataka kuona na sio kusimuliwa; MKAPA alionyesha na kuboresha nchi mbona haya mambo hayakuwepo yamekuwa tata hivyo? Maisha yamezidi kuwa ghali na hakuna chochote huku mfumuko wa bei na ufisadi vikizidi kushika chati; Tunaelekea wapi Watanzania? Tuchape kazi na serikali iwajibishwe!
Quote
 
 
+5 #1 mabuwe 2011-03-19 09:58
Mhashamu Askofu Yuda , hapo umenena, rudia tena kuwapasha hayohayo kwenye sherehe maana huko cream yote ya viongozi wenye propaganda chafu itakuwepo.
Quote
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!

No comments:

Post a Comment